The House of Favourite Newspapers

Ali Kiba, Sallam Wametoka Mbali

kibaWiki mbili zilizopita, Ali Kiba alikuwa mmoja kati ya mastaa wa muziki waliopafomu kwenye Tamasha la Rock lililofanyika Viwanja vya Golf, Mombasa.
Katika tamasha hilo lililokuwa na staa kutoka Marekani, Christopher Maurice ‘Chris Brown’ na Ayodeji Balogun ‘Wizkid’ kutoka Nigeria liligeuka kuwa na sintofahamu baada ya Ali Kiba kupanda na kupafomu nyimbo mbili tu, ikiwemo Mac Muga kisha kuzimiwa kipaza sauti.
Malalamiko ya Ali Kiba (pichani juu) juu ya tukio hilo aliyaelekeza moja kwa moja kwa meneja wa Diamond Platinumz, Sallam Sharaff ambapo alisema;
“Mkataba waliokubaliwa ulikuwa Chris Brown apafomu kwa dakika 80 na pale muda ulikuwa umekwenda sasa sijajua kitu gani kimefanyika mpaka imekuwa hivyo. Kuna vitu sikuvielewa yaani sikufurahishwa navyo, nilimuona meneja wake Diamond, Sallam. Yeye alifuata nini backstage. Japo watu wanafikiria sina bifu na Diamond, sasa yeye alikuwa kafuata nini? Kuna watu wengi walikuja kwenye shoo na kuna hadi VIP, yeye alifuata nini backstage?”
Alichojibu Sallam, alikuwepo hapo kwa sababu ya ukaribu na Meneja wa Wizkid, Sunday.
“Meneja anayesimamia kazi (connection) za Diamond Afrika Magharibi ni Mr Sunday. Kwa Afrika Mashariki anayesimamia kazi za Wizkid ni mimi. Kuja hapa (Mombasa) ni kitu cha kawaida kabisa. Wakati anapafomu mi sikuwepo kabisa eneo lile.
“Tushirikiane, tuache kujenga chuki, kama niliwakwaza watu wote wa Kenya na walinichukulia kama nilimfanyia nia mbaya Ali Kiba wanisamehe. Naomba na yeye Kiba awaombe msamaha mashabiki wote wa Kenya. Nachosema pole Kiba, shoo yako haikuwa nzuri, ukaona lawama umpe f’lan.”
Ingawa kumekuwa na madai ya kuwepo kwa bifu kati ya mastaa wawili, Diamond na Ali Kiba, wote wawili kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikanusha. Kuna timu zimeundwa, kuna wadau wamegawanyika, lakini wenyewe kila mara wanasema no bifu kati yao.
Hata hivyo, yapo baadhi ya matukio yanayoonyesha chembechembe za ukweli juu ya sintofahamu baina ya mastaa hao wawili. Lakini kwa umakini, kinachoendelea kati ya Sallam, mtu anayetajwa kuwa nyuma ya mafanikio ya Diamond na Ali Kiba, siyo kitu cha kubeza, kwani ‘mvutano’ baina yao unaanzia mbali.

sallam

Sallam Sharaff.

Januari, 2015
Katika shoo iliyofanyika Januari 2015, Viwanja vya Leaders jijini Dar ambayo iliandaliwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ikitambulika kama Tigo Kiboko Yao, mastaa mbalimbali wa Bongo Fleva walialikwa kutumbuiza akiwemo Diamond na Ali Kiba.
Kiba hakutumia mlango maalum wa VIP kuingia ndani, bali kwa sababu anazozijua mwenyewe aliruka ukuta na kuingia backstage. Alipotua, watu wa karibu kabisa walikuwa ni MwanaFA na Shaa ambao kwa anachojua mwenyewe pia, akawakaushia, akapitiliza moja kwa moja jukwaani na kuanza amsha-amsha.
Ni usiku huohuo ambao Diamond alizomewa na kurushiwa chupa za maji na mashabiki. Pengine kwa kujua namna ya kuwatuliza, mkali huyo wa kibao cha Kidogo, aliwarushia noti za shilingi elfu mbilimbili, akafanikiwa kuwanyamazisha mazima.
Kesho yake, Sallam kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika maneno yaliyoonyesha kumlenga King Kiba;
“Umeruka ukuta, wametupa chupa, zikawaishia, umemzuia @mwanaFA @Shaa_tz wasikusalimie, uliowalipa wakarushiwa buku mbilimbili WAKAKUSALITI.”

Agosti, 2015
Katika msimu wa tatu unaowashirikisha wasanii wa mataifa mbalimbali kujumuika pamoja na kufanya kolabo ya nyimbo zao, Coke Studio ilimualika Ne-Yo pamoja na wasanii kutoka Afrika wakiwemo Wangechi (Kenya), Ali Kiba (Tanzania), Victoria Kimani (Kenya), Maurice Kirya (Uganda), Dama Do Bling (Mozambique) pamoja na Ice Prince (Nigeria).
Mbali na Ali Kiba kufanya kolabo ya Coke Studio na Ne-Yo, pia alifanya naye kolabo nje ya shoo hiyo. Kiba akiwa bado yupo nchini Kenya kwa shoo hiyo huku nyuma Diamond, Prodyuza Sheddy Clever pamoja na Sallam walitimba nchini humo na kufanya kolabo na Ne-Yo kimyakimya na meneja huyo akatupia picha mitandaoni jambo linalotafsiriwa kuchochewa na Sallam kujibu mapigo.

Septemba, 2016
Sherehe ya kutimiza miaka 10 ya Chama cha Orange for Democratic Movements (ODM) cha Raila Odinga, iliwaalika wakali Ali Kiba na Diamond bila kujuana katika Viwanja vya Mama Ngina, Mombasa.
Diamond alitangazwa kama msanii rasmi atakayetumbuiza bila kujua kama Kiba naye alikuwa ameingia nao ubia wa kulipwa kufanya shoo hiyo.
Diamond alipomaliza kupafomu, Kiba naye aliingia kama msanii sapraizi jambo lililofanya shangwe kuzidiana na kuonekana kama mmoja amefunikwa.
Kupitia ukurasa wa Instagram, Sallam aliandika maneno yaliyotafsiriwa hakufurahishwa na shoo ya kushtukiza iliyofanywa na Kiba ambapo alisema;
“Diamond ndiye msanii mkubwa aliyealikwa, nyomi ile haikuvutwa na msanii sapraizi (Ali Kiba). Asanteni Mombasa”
Pia akaweka picha na kuandika posti nyingine kuwa;
“Tumemaliza kufanya shoo Mombasa kinachofuatia ni ziara ya Afrika, hivyo kama kuna yeyote unamfahamu ni msanii sapraizi mtaje hapa.”

Oktoba 22, 2016?
Katika Tuzo za MTV (MAMA) zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 22, mwaka huu, Ali Kiba amepangwa kutumbuiza. Tayari katika mahojiano aliofanyiwa, Sallam hivi karibuni ameweka wazi lazima atakuwepo backstage na Kiba asiogope kwani yeye ni mtu wa kawaida sana.

Comments are closed.