Alt name

Amani ni bora kuliko mtu kuipata ikulu

2. Umati wa watu waliohudhuria mkutano wa CCM, Usa River janaMWANAFUNZI wa Nabii Yesu aliyeitwa Petro alimtetea mwalimu wake asionewe kwa kutumia makali ya upanga; imeandikwa hivi katika Kitabu cha Yohana 18: 10-12.

“Basi Simoni Petro alikuwa na upanga akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume na yule mtumwa jina lake ni Marko.

“Basi Yesu akamwambia Petro, rudisha upanga alani mwake… Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga.”

Nabii Yesu anafundisha somo kubwa katika mistari hiyo kwamba amani ilikuwa ni jambo muhimu katika nchi kuliko uhai wake, unabii wake na utumishi wake wa Neno la Mungu.

Ndiyo maana alimkanya Petro aache kutumia silaha, akome kumwaga damu kwa kisingizio cha kupigania haki na zaidi ya yote alitumia uwezo wake kumponya mtumwa wa Kuhani Mkuu kwa kumrudishia sikio lake.

Unyenyekevu huu wa Yesu ulileta matunda makubwa; Ukristo aliokuwa anaupigania kila mtu anaona ulivyoenea hata baada ya kifo chake. Ni matarajio yangu kuwa kipindi hiki cha vuguvugu la kuelekea uchaguzi mkuu nchini, wanasiasa wetu watakuwa waungwana kwa kuwakataza wafuasi wao waache kumwaga damu, wakome kutumia silaha kwa madai ya kutetea haki zao kwa sababu haki hujipigania yenyewe.

Kwangu mimi mwanasiasa, mgombea wa nafasi yoyote, muhimu kwake ni kulinda amani na siyo kukata watu sikio kwa lengo la kupata utukufu, kumwaga damu za wananchi ili aingie ikulu au apate ubunge au udiwani kwa kuwa amani ni bora siyo tu zaidi ya cheo bali hata uhai wa mgombea mwenyewe.

Yesu alijua kuwa akiruhusu mapigano baina ya wafuasi wake na wapinzani wao mafaniko ya Neno la Mungu yasingepatika. Aliamini akijenga uadui fursa ya kueneza Neno la Mungu ingekosekana! Naam, hata wagombea wetu hasa wa urais wanafahamu ikulu hakukaliki kama wananchi wanamwagana damu mitaani.

Mifano iko wazi, mahali ambapo ikulu ilitafutwa kwa damu vyeo vililetwa kwa makali ya upanga nchi zimeandika historia ya kusikitisha; Nenda Libya, Misri ukajionee.

Penye mapigano hakuna mama lishe, hakuna wachuuzi, hakuna maendeleo na hakuna utu, sote tunajua.

Kwa msingi huo, rai yangu kwa wanasiasa ni kuhakikisha kuwa taifa linapewa kipaumbele kuliko harakati za kutaka madaraka. Msingi wa maendeleo wanayoyanadi majukwaani kuwa watayaleta uko kwenye amani; amani ikikosekana hakuna kitakachofanyika zaidi ya tabu kuongezeka mara mbili.

Niwashauri wanasiasa wetu, kila wanaposhuhudia akina Petro wakitoa mapanga yao na kuwakata watumishi wa ‘kuhani’ sikio, wawe wa kwanza kuwakemea na kuwaamuru warudishe mapanga yao alani na wasiishie hapo wachukue jukumu la kuwatibu wajeruhiwa.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, machafuko siyo kitu cha kufurahia, si jambo la kunyamaziwa hivihivi kana kwamba hatuoni hatari ya kuvunja misingi ya amani ya nchi yetu.

Juzi mkoani Mara zimetokea vurugu zilizochochewa na ushabiki wa kisiasa, mtu mmoja amepoteza maisha na wengine kujeruhiwa; sikuwasikia wanasiasa wakiwakemea wafuasi wao na kuchukua jukumu la kuwaponya waliojeruhiwa; mambo yameachwa yaende, nijuavyo; ‘chachu kidogo huchachua donge zima.’

Tukiacha kuchukua hatua mapema za kuwafanya wafuasi wa mfano wa Petro wasione kutoa upanga alani ni dhambi na kumwaga damu ni jinai, watajitokeza wengine na kufanya mabaya zaidi.

Huu ni wakati wa kuwaambia watumia upanga kwa madai ya kutetea haki zao, wakome kufanya hivyo kwa sababu ya masilahi ya taifa.Nawaomba wananchi wote; tuwapuuze wanaopuuza amani.

Leave A Comment

Related Posts