The House of Favourite Newspapers

Anakunyima ‘chakula cha usiku’ bila SABABU-2

INAPOTOKEA mwenzi wako akawa na tatizo kama tulivyoanza kujadiliana wiki iliyopita, jambo muhimu la kwanza unalotakiwa kulifanya, ni kutafuta chanzo cha tatizo. Kwa bahati mbaya mno, wanaume wengi hawajui kwamba wao wanaweza kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha wenzi wao kukosa hamu ya tendo la ndoa. Na kama nilivyosema, kwa kutojua namna ya kulishughulikia tatizo hili, wanandoa wengi hujikuta wakiishia kutengana au kupeana talaka moja kwa moja. Kwa kuzingatia uzito na unyeti wa suala lenyewe, ndiyo maana nataka tujadiliane mbinu za kujinasua inapotokea umenasa kwenye tatizo hili. Hakuna mgogoro ambao humalizika bila pande mbili zinazovutana, kukaa chini na kuzungumzia tatizo lililosababisha wakafikia kwenye mgogoro.

Hata hivyo, ni wachache wanaoelewa nini cha kuzungumza na kipi cha kutozungumza katika kusaka suluhu. Mbinu ya kwanza kabisa, unatakiwa uanze kujiuliza wewe mwenyewe, mwenendo wako wa kimaisha umekuwaje mpaka mwenzi wako amebadilika? Pengine umekuwa ni mtu unayeendekeza ulevi sana, pengine umekuwa ukichepuka hovyo na mkeo anao ushahidi wa matendo unayoyatenda nyuma ya mgongo wake.

Yawezekana humjali tena kama zamani, hata fedha za matunzo yake binafsi, achilia mbali matumizi ya familia humpi tena. Upo utamaduni wa baadhi ya wanaume kwamba hata kama anao uwezo wa kifedha, anachompa mkewe ni mahitaji ya familia tu. Haoni kama kuna umuhimu kwa mkewe kuvaa nguo nzuri, kuwa na mafuta mazuri au kuwa na mahitaji muhimu au hata kuwa na fedha za akiba kwa ajili ya matumizi yake binafsi.

Yawezekana pia kwamba huishi vizuri na ndugu zake au ndugu zako ‘hawam-treat’ vizuri, iwe ni wazazi au wifi zake. Nimekutajia mambo haya ili uelewe kwamba yawezekana ukawa unaliona tatizo kuwa ni dogo na halina uzito, lakini lisipopatiwa ufumbuzi wa kutosha, mwisho wake huwa mbaya mno. Zipo sababu nyingi, ukiachilia mbali hizo nilizozitaja hapo juu, nyingine ni za kimwili na nyingine ni za kisaikolojia.

Maudhi ya mara kwa mara, usaliti, vipigo, kushindwa kumjali au kushindwa kumfanya ajisikie amani anapokuwa na wewe, ni miongoni mwa sababu nyingi zinazoweza kumfanya mwenzi wako akachukia kukutana na wewe faragha na kama nilivyoeleza kuanzia mwanzo, hapa ninawazungumzia zaidi wanawake.

Ipo sababu nyingine kubwa ambayo wengi wanaifumbia macho! Je, unamuandaa kwa kiasi gani mwenzi wako kabla ya chakula cha usiku? Wanaume wengi wanachojua ni kurukia kama wanaendesha baiskeli na kuanza kupiga pedeli, jambo ambalo husababisha maumivu makali kwa wenzi wao na kuwafanya wayachukie kabisa tendo la ndoa.

Hebu tenga muda wa kutosha wa kumuandaa mwenzi wako ili na yeye aone raha ya mchezo, jifunze, hata kwa kusoma vitabu vinavyohusu sanaa ya mapenzi na uhusiano. Pia muoneshe kwa vitendo kama unampenda, hebu msaidie kumaliza matatizo madogomadogo yanayomkabili, mfanye ajisikie amani anapokuwa na wewe, hakika hataweza kukunyima haki yako.

Suala la msingi, kama tayari upo ndani ya tatizo, tafuta muda wa kuzungumza na mwenzi wako, mbembeleze kwa maneno ya upole, akueleze kosa lako ni nini na atakapokueleza, badala ya kukimbilia kujitetea, muombe msamaha na anza kumuonesha kwa vitendo mabadiliko, rekebisha kasoro zote mpaka afurahi, ukifanya hivyo utalifanya penzi lenu lirudi kuwa jipya kabisa. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Makala:Hashim Aziz

Comments are closed.