The House of Favourite Newspapers

Athari za vidonge vya uzazi wa mpango

VIDONGE vya uzazi wa mpango, ni moja ya njia inayopendekezwa na wataalamu wa mpango wa uzazi katika kuzuia mimba.  Hadi sasa kuna aina kuu mbili tu za vidonge vya uzazi vinavyotumiwa na wanawake katika mpango huo, ingawa aina zote hizo zina vichocheo (hormons). Aina hizo kitaalamu zinaitwa Estrogen na Progesteron. Estrogen ni aina ya kichocheo kinachotengenezwa na uterasi/kizazi, kinachosaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi, kwa kuongoza ukuaji wa kuta za uterasi kwenye sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi.

Kwa upande wake, Progesterone, hiki ni kichocheo cha kopasi luteamu ya ovari, kinachosaidia kuanzisha mabadiliko katika endometriumu baada ya kurutubishwa mayai.

Ingawa katika aina hizo mbili za vidonge, kuna vingine vina kichocheo cha aina moja tu, kwa maana ya ama Estrogen au Progesterone, huku vingine vikiwa na vichocheo vyote viwili. Lakini vidonge vyote hivyo ni salama, na vinafanya kazi kwa kufanya ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na kuzuia kupevuka kwa yai, hivyo kuzuia mimba kwa kiwango cha asilimia 99.

Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza pia kutumika kama tiba ya kuweka sawa mzunguko wa hedhi, kuzuia maumivu makali wakati wa hedhi, kutibu chunusi pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa katika via vya uzazi, ambayo hayatokani au kusababishwa na magonjwa ya ngono.

Hata hivyo, pamoja na usalama wa vidonge hivyo katika kufanya kazi yake hiyo ya kuzuia mimba na tiba kwa magonjwa hayo, vidonge hivyo vinaweza kumsababishia athari za kiafya mwanamke kama havitatumika katika mpangilio sahihi. Athari kuu 10 zinazoweza kusababishwa na vidonge hivyo ni pamoja na kutokwa na damu ukeni baada ya hedhi ya kawaida. Athari hiyo huweza kuwapata asilimia 50 ya wanawake wote wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango.

Hali hii huweza kuwatokea ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza matumizi ya dawa hizi. Kwa ujumla, hali hiyo huweza kukoma kwa zaidi ya asilimia 90, pindi mwanamke anapoanza kutumia pakti ya tatu ya dawa hizo katika kipindi hicho cha hedhi. Mwanamke anapotokewa na hali hiyo kwa mfululizo wa siku tano au zaidi baada ya kumaliza siku zake za kawaida za hedhi, anashauriwa kuwasiliana na mhudumu wa afya wakati akiendelea kutumia dawa hizo.

Athari ya pili, ni kujisikia kichefuchefu. Mara nyingi hali hii humtokea mwanamke mwanzoni tu baada ya kuanza kumeza vidonge vya uzazi wa mpango, ingawa hali hii inaweza kukoma baada ya siku chache. Inashauriwa pia kwa mwanamke anayepatwa na hali hii ya kichefuchefu kuwasiliana na mhudumu wa afya kama ataona hali hiyo inazidi.

Matiti kujaa au kuwa na maumivu, ni athari nyingine inayoweza kusababisha na matumizi ya vidonge hivyo. Hali hii huweza kumpata baada ya kuanza kutumia vidonge hivyo, na huweza kukoma ndani ya wiki moja tu. Hata hivyo, inashauriwa kwamba ikiwa matiti hayo yatatokwa na uvimbe au maumivu yasiyoisha, ni muhimu kutafuta tiba kwa wahudumu wa afya, ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya kinywaji chenye kafeini (caffeine) na chumvi na kuvaa brauzi isiyobana matiti.

Maumivu ya kichwa ni athari nyingine inayoweza kumtokea mwanamke, ingawa pia kuumwa kichwa kunaweza kuwa na dalili za magonjwa mengine. Hata hivyo, kama itatokea maumivu hayo ya kichwa yakaanza tu mara baada ya kumeza vidonge hivyo, hiyo itakuwa ni dalili ya athari mojawapo na ni vyema kutoa taarifa kwa mhudumu wa afya.

Vidonge vya uzazi wa mpango huweza pia kuongeza uzito wa mtumiaji, ingawa tafiti nyingine zimeshindwa kuthibitisha uhusiano uliopo kati ya vidonge hivyo na mabadiliko ya uzito wa mtumiaji. Mabadiliko ya hisia huweza pia kumtokea mwanamke anayeanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango. Inashauriwa kwamba kipindi mwanamke anapoona dalili hii, ni muhimu kumjulisha mhudumu wa afya ili kuweza kujadili ni jinsi gani ataweza kutumia dawa hizo, kwa sababu dalili hii ni mbaya kiafya kwa mtu mwenye historia ya ugonjwa wa kushuka moyo (Depression).

Itaendelea wiki ijayo.

Na Dk. Marise Richard

Comments are closed.