The House of Favourite Newspapers

Bibi Dar alia, msiniue mimi si mchawi!

1

bibi (3)Bibi Zainabu Salum.

Waandishi wetu, Amani

DAR ES SALAAM: Hatari! Bibi mwenye umri mkubwa, mkazi wa Tandika wilayani Temeke, Zainabu Salum, amewalilia majirani zake na kuwataka wasichukue hatua ya kumtoa roho, kwani yeye siyo mchawi kama wanavyodai, Amani lina mkanda kamili.

Kilio hicho kinafuatia wananchi hao jirani, kuvamia nyumbani kwake na kumtuhumu kuwa ni mwanga, kutokana na kile walichodai, mateso na mauzauza ya mara kwa mara yanayowatokea, ikiwa ni pamoja na vifo vya kushangaza vinavyotokea.

bibi (1)Badhi ya mashuhuda w tukio hilo.

Bibi huyo alisema yeye hajapata kuwa mchawi hata mara moja na endapo kuna mtu anayetambua wachawi, basi apelekwe ili ukweli upatikane, badala ya watu kutaka kumdhuru kwa hisia zisizokuwa na kichwa wala miguu.

Majirani hao katika tuhuma zao, walisema kichanja kimoja kilichojengwa pembeni ya nyumba anayoishi bibi huyo, ndicho kinachohifadhi uchawi wake, na hivyo kumtaka kukivunja, vinginevyo watachukua sheria mkononi. Bi Zainabu alisema kichanja hicho kilijengwa na marehemu mumewe aliyekuwa mganga wa kienyeji na kumtaka anayehisi kinatumika kichawi, akakivunje!

Wakati majirani wote wakisita kukivunja kichanja hicho, mtoto mkubwa wa bibi huyo, Juma Omari alidai kama kweli mama yake ni mchawi, watu wachange pesa na kuleta mtu ambaye atamthibitisha na kwamba ikiwa hivyo, yu tayari mama yake auawe.

bibi (2)Mtoto wa Bibi Zainabu.

“Mimi naanza kutoa mchango wangu huu hapa shilingi elfu tano, wengine watoe pia, kama kweli mama ni mchawi mimi niko tayari auawe hadharani,” alisema huku majirani hao wakishindwa kuungana naye kuchanga.

Baadhi ya majirani na wapita njia waliozungumza na gazeti hili kuhusu kadhia hiyo, walishangazwa na majirani hao kuendelea kuamini ushirikina katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

“Haya mambo ungeyategemea miaka mingi iliyopita, tena maeneo ya mbali kabisa vijijini, siyo hivi sasa halafu Dar es Salaam, unamtuhumu mtu kuwa mchawi, angekuwa mchawi si angemaliza kwanza watoto wake, tunavyojua wanga huwala aliozaa mwenyewe,” alisema mpita njia aliyejitambulisha kwa jina la Cosmas.

Jabir Njambu, aliyejitambulisha kama jirani, alisema dunia tuliyopo, siyo ya kutukuza mambo ya giza, kwani hayo ndiyo yanawaongoza watu kuwaua vikongwe sababu ya macho yao mekundu au kuamini viungo vya binadamu wenzao vinaweza kuwapatia utajiri.

“Tunapoendekeza mawazo kama hayo, ndiyo sawasawa na kuamini kuwa unaweza kupata utajiri kwa nguvu za giza au viungo vya mwenzako, jambo ambalo halipo. Lazima tubadilike, tena wakati mwingine viongozi wa serikali wanapaswa kuwachukulia hatua watu wanaoamini katika wanga, ndiyo wanaturudisha nyuma kimaendeleo,” alisema Njambu.

Waandishi: Boniphace Ngumije na Gabriel Ng’osha.

1 Comment
  1. Great Thinker says

    Majirani wasifanye haraka kuchukua hio hatua ya kumuua huyo bibi kizee, kwa nn wasimwambia ahame mtaa wao huo kwa muda wa miezi kadhaa na ndipo itajulikana kama yy ni mchawi au sio, kwa kuhama kwake pasipotokea hayo mauzauza ndipo ptajulikana ukweli wake, na ikiwa yataendelea mauzuza basi wana haki ya kumfukuza mtaa wao huo akaishi pengie porini kabisa kuliko kuchukua hatua ya kumuua.

Leave A Reply