The House of Favourite Newspapers

BONGA YAI: PUNCTUATION (MATUMIZI YA ALAMA KATIKA SENTENSI)

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, ni wakati mwingine ninapokukaribisha darasani, leo tutazungumzia kitu muhimu ambacho wengi hukipuuza, katika matumizi ya lugha, hasa Kiingereza. Nimelazimika kurudia kuhusu somo hili kutokana na maombi mengi kutoka kwa wasomaji.

 

Punctuation, linatamkwa ‘pankchuesheni’, ni somo linalofundisha kuhusu matumizi sahihi ya alama mbalimbali katika sentensi, zikiwemo herufi kubwa (capital letters), nukta (full stops), mkato (comma), mabano (brackets), nukta pacha (full colon), viulizo (question marks), mshangao (exclamation marks) na nyingine nyingi.

Makosa wanayoyafanya watu wengi wakati wa kuandika, iwe ni Kiswahili, Kiingereza au lugha yoyote, ni kutozingatia matumizi ya alama hizi.

 

Ni rahisi kumgundua mtu asiyejua matumizi sahihi ya alama hizi pale unapompa kazi ya kujieleza kwa maandishi na wengi hujikuta wakifeli kwenye maombi ya kazi au sehemu nyingine nyingi, kutokana na kushindwa kuandika kwa kuzingatia matumizi ya alama hizi.

Kushindwa kutumia alama hizi, pia huharibu maana au kufikisha ujumbe tofauti kabisa na ule uliokusudiwa na mtu anayeandika. Ili kuepusha mkanganyiko huu, ili pia kuepusha kudharauliwa pale unapoandika, ni vyema ukazingatia matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na herufi.

 

CAPITAL LETTERS (HERUFI KUBWA)

Herufi kubwa hutumika kwa matumizi mbalimbali lakini yafuatayo ni muhimu zaidi

-Mwanzo wa sentensi. Unapoandika sentensi yoyote, iwe kwa Kiswahili au Kiingereza, lazima neno la kwanza liwe la kwa herufi kubwa.

-Unapotaja majina ya watu au sehemu ni lazima uanze na herufi kubwa, kwa mfano Juma, Asha, Dodoma, Msumbiji na kadhalika.

-Katika majina ya vitabu, filamu, taasisi na kadhalika, pia lazima utumie herufi kubwa.

-Katika majina ya dini au madhehemu, sikukuu za kidini au kiserikali, kwa mfano Krismasi, Pasaka, Ukristo, Uislamu, Wakatoliki na kadhalika.

Pia herufi kubwa hutumika unapoandika vifupisho vya maneno, kwa mfano USA (United States of Amerika), BBC (British Broadcasting Corporation) na kadhalika.

 

FULL STOP (NUKTA/KITUO)

Full stop is the simplest punctuation marks to use. Maana yake ni kwamba nukta au vituo ndiyo alama nyepesi zaidi kuitumia. Kila sentensi utakayoiandika, ili kuonesha kwamba umefika mwisho ni lazima uweke alama ya nukta mwishoni.

Kuandika sentensi na kuiacha bila kuweka kituo, kutamfanya anayesoma akudharau kwa sababu atagundua haraka kwamba uelewa wako katika matumizi ya lugha ni mdogo sana.

Hupangiwi urefu wa sentensi unatakiwa uweje, ni wewe ndiye unayechagua kwamba sentensi hii iishie hapa na nyingine ianzie wapi. Hata katika mazungumzo, mzungumzaji mzuri ni yule anayeweza kuweka vituo katika mazungumzo, huwezi kuanza kuongea mfululizo kama chiriku, ni dhahiri wanaokusikiliza hawawezi kukuelewa.

Pia ukiwa unasoma maandishi na ukakutana na alama ya nukta, maana yake ni lazima upumzike kwanza kwa sekunde kadhaa kabla ya kuendelea na sentensi inayofuata. Jambo la msingi la kulitambua ni kwamba kila unapoweka alama ya full stop, lazima neno linalofuatia lianze kwa herufi kubwa.

 

COMMA (MKATO)

Mkato ni alama yenye matumizi mengi katika lugha ya Kiingereza lakini ambayo unatakiwa kuwa makini sana kwenye matumizi yake kwani huweza kubadilisha maana kabisa katika sentensi kama usipokuwa makini.

Nitajitahidi kurahisisha ili unielewe vizuri zaidi.

-Comma hutumika kutenganisha orodha ya vitu vinavyotajwa katika sentensi. Kwa mfano:

Juma likes to play football, basketball and volleyball. (Juma anapenda kucheza mpira wa miguu, mpira wa kikapu na mpira wa wavu.)

 

Ukitazama vizuri katika sentensi hiyo, utaona kwamba aina mbili za mwanzo za mpira zimetenganishwa kwa comma lakini aina ya tatu, imetenganishwa kwa neno ‘and’. Kwa lugha nyepesi, unapotaja orodha ya vitu kadhaa, neno la mwisho huwezi tena comma badala yake unaweza neno ‘and’.

Sir Hashpower teaches English, French, Spanish and Chinese. (Mwalimu Hashpower anafundisha Kiingereza, Kifaransa, Kispaniola na kichina), litazame vizuri neno ‘and’ lilivyotumika.

-Comma pia hutumika kutenganisha maana katika sentensi na hapa ndipo panapohitaji zaidi umakini kwani unaweza kubadilisha maana nzima ya sentensi. Kwa mfano, tazama sentensi hizi mbili:

 

  1. Kill him don’t, let him live.
  2. Kill him, don’t let him live.

Rudia tena kuzitazama vizuri sentensi hizo! Umegundua kwamba maneno ya sentensi ya kwanza ndiyo yaleyale kwenye sentensi ya pili? Umeona mahali comma ilipowekwa kwenye sentensi ya kwanza? Umeona pia ilipotumika kwenye sentensi ya pili?

Basi kwa taarifa yako, kitendo cha kuhamisha comma kutoka baada ya neno don’t na kuiweka kabla ya neno hilohilo (don’t), kimebadilisha kabisa maana ya sentensi.

Tafsiri ya sentensi ya kwanza, ni kwamba: ‘Usimuue, muache aishi’ lakini sentensi ya pili inamaanisha kinyume chake, ‘Muue, usimuache aishi’. Kwa hiyo utagundua kwamba kosa hilo dogo tu la kutozingatia sehemu comma inapotakiwa kuwekwa, linaweza kusababisha mtu akauawa.

 

-Comma pia hutumika kutenganisha tarehe, hasa pale unapotaja siku, tarehe, mwezi na mwaka. Kwa mfano,

Abel arrived on Wednesday, May 15, 2018. (Abel aliwasili Jumatano, Mei 15, 2018). Ukitazama kwa makini, utagundua kwamba comma imetumika kutenganisha siku, lakini pia imetumika mwisho kutenganisha mwaka, katikati ya mwezi na tarehe hakuna comma.

Hiyo ni kanuni, kwa hiyo unapaswa kuichukua jinsi ilivyo, kama hutaji siku basi itabaki kuwa May 15, 2018. Lakini pia kama hutaji tarehe, bali mwezi na mwaka tu, huna haja ya kuweka comma, kwa mfano May 2018.

 

BRACKETS (MABANO)

Mabano hutumika kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu jambo fulani lililoelezewa katika sentensi, ambalo hata kama lisipofafanuliwa, haliwezi kuharibu maana ya sentensi.

Brackets are used within a sentence to include information that is not essential to the main point. Zipo aina nne za mabano, curved brackets (…), square brackets […], curly brackets {…} na angle brackets <…> lakini kwa ‘level’ yetu tutazungumzia aina moja tu, curved brackets au mabano ya kawaida.

 

Mabano ya kawaida, kama nilivyoeleza, hutumika kuongezea maelezo kuhusu jambo fulani. Kwa mfano:

Magufuli (The President of Tanzania), visited Dar es Salaam Port and talked to citizens. Magufuli (Rais wa Tanzania) alitembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na wananchi.

Maneno yaliyowekwa kwenye mabano, yamefafanua tu kuhusu Magufuli lakini hata kama yasingewekwa, bado sentensi inaeleweka vizuri.

 

FULL COLON (NUKTA PACHA)

Full colon au colon (:), ni nukta mbili zinazotumika katika sentensi, kwa matumizi mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni kutambulisha orodha ya vitu unavyotaka kuvitaja.

Colon (:) is a punctuation mark that is used to a series of items. Pia hutumika kutofautisha vitu viwili visivyofanana kwenye sentensi.

Kwa mfano: You may be required to bring many things: sugar, cooking oil, soaps and maize flour.

(Utatakiwa kuja na vitu vifuatavyo: sukari, mafuta ya kupikia, sabuni na unga wa mahindi).

 

QUESTION MARK (KIULIZO)

Matumizi ya alama hii kama inavyojieleza, ni mepesi kabisa! Hutumika mwisho wa sentensi yenye swali la moja kwa moja.

Kwa mfano: Where is my car? (Gari langu liko wapi?)

  • Why are you looking at me? (Kwa nini unanitazama?)

 

EXCLAMATION MARK (ALAMA YA MSHANGAO)

Alama ya mshangao, si tu hutumika kwenye sentensi zinazoonesha mshangao bali pia hutumika kuonesha msisitizo kuhusu jambo fulani, kuonesha mshtuko au hisia za ndani kama furaha, huzuni, hasira na kadhalika.

  • Wow! She is very beautiful.
  • Oh! God help me.
  • Congratulation!

 

Mifano ni mingi lakini kwa leo tuishie hapa. Zipo alama nyingine ambazo hazitumiki sana kwenye uandishi, lakini hizi tulizojadiliana ndizo muhimu unazopaswa kuzielewa. Nakusisitiza, kusoma hapa peke yake hakutoshi, lazima ujenge utaratibu wa kuwa unarudia kujisomea tena mara kwa mara kile tulichojifunza.

NA MWALIMU HASHIM AZIZ

Maoni | Ushauri 0719401968

Comments are closed.