The House of Favourite Newspapers

Bosi Azam, Lyon nusura wazichape

0

AZAM (5)

Kocha wa Azam akifanya mazoezi na wachezaji wake. 

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam
KATIKA hali ya kushangaza mmiliki wa Klabu ya African Lyon, Rahim Zamunda na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba juzi Jumamosi nusura warushiane makonde kufuatia matokeo ya timu zao ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara uliopigwa usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
Mchezo huo ulionekana wazi kuwa mgumu kwa kocha mpya wa Azam, Mhispania, Zeben Herenandez kutokana soka la hali ya juu lililoonyeshwa na African Lyon iliyopanda daraja msimu huu ikiwa na kocha mpya Bernardo Tevares.

Championi lilimshuhudia mmiliki huyo wa African Lyon akianza kulalamika kufuatia kuongezwa kwa dakika sita za nyongeza katika mchezo huo huku wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Hood Mayanja kwa njia ya faulo, hali Iiliyozua sintofahamu kwa upande wa timu hiyo kwani walidai kuonewa kutokana na kuongezwa kwa dakika nyingi.

Hali ilizidi kuwa mbaya kwa bosi huyo baada ya Azam kusawazisha bao lao kupitia nahodha John Bocco wakati mshambuliaji wa African Lyon akiwa ameumia hali iliyolazimu kwenda chini ya jukwaa kuu na kuanza kuwatuhumu viongozi wa Azam wanabebwa, kitendo kilichomkera Kawemba ambaye alianza kumjibu kabla hajashuka chini kabisa mpira ulipoisha kisha kuanza kujibizana kisharishari na kiongozi huyo.

Ugomvi wa viongozi hao ulikuwa mkubwa walipokutana katika eneo la kubadilishia nguo ‘dressing room’ za wachezaji kutokana na kila mmoja kumtolea maneno ya kashfa mwenzake kabla ya polisi na baadhi ya viongozi wengine kuingilia kati kuwatuliza kwa kuwaondoa kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, hakuna kiongozi ambaye alikuwa tayari kuliongea hilo mara baada ya kuachanishwa.

Leave A Reply