The House of Favourite Newspapers

Chanzo cha maradhi ya moyo kwa watoto

KABLA ya kubeba ujauzito ni muhimu mwanamke ajiandae kwa miezi sita. Katika kipindi hicho, anapaswa kula vyakula bora.  Mwanamke anapaswa kuwa makini katika kipindi cha wiki 12 za kwanza za ujauzito. Ni muhimu kwani ndipo ambapo viungo vya mwili wa mtoto huanza kuumbwa.

Viungo vya mtoto huanza kuumbwa katika kipindi cha wiki 12 za kwanza za ujauzito. Mama anapokuwa amejiandaa kubeba ujauzito miezi sita kabla, anatakiwa kuachana na ulaji usiofaa, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na mambo mengine kama hayo.

Hii husaidia kumuepusha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo. Kama mama hajajiandaa katika kipindi cha miezi sita kabla, ni hatari kwa mtoto aliyembeba tumboni kwani ataendelea na maisha yake ya kawaida, mfano ulaji usiofaa, uvutaji sigara na unywaji pombe hivyo kumuathiri mtoto.

TATIZO LA MOYO KWA WATOTO

Asilimia 10 tu ndiyo tunajua sababu ya mtoto kuzaliwa na tatizo hili la ugonjwa wa moyo na mara nyingi chanzo huwa ni matatizo anayoyapata mama katika kipindi cha miezi mitatu ya ujauzito.

Huenda mama alipata homa kali wakati wa ujauzito, virusi vya rubella, shinikizo la damu, kisukari au alikuwa anakunywa dawa bila ushauri wa daktari. Lishe duni; yaani mama asipopata virutubisho vya folic acid, uvutaji sigara, unywaji pombe na sababu nyinginezo ikiwemo kurithi ingawa si kwa asilimia kubwa, mtoto hupata matatizo ya moyo.

Mjamzito anashauriwa kuhudhuria kliniki kwa kipindi chote ili wataalam wafuatilie afya ya mtoto.

Katika kipindi hicho, mama hupewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa rubella ambao unaweza kumsababishia mtoto magonjwa ya moyo. Magonjwa ya moyo kwa watoto yapo ya aina mbili; yale ya kuzaliwa nayo na yasiyokuwa ya kuzaliwa nayo. Haya ya kuzaliwa nayo, chanzo ni iwapo mama hatapatiwa baadhi ya chanjo ikiwemo ya rubella na ulaji usiofaa.

DALILI

Watoto waliozaliwa na tatizo la moyo huwa wanaonesha dalili tofautitofauti ikiwemo kuzaliwa na uzito mdogo. Wengine wanabadilika rangi isiyokuwa ya kawaida na wengine wakinyonya huchoka haraka na kutokwa jasho kwa wingi.

Mtoto akinyonya kidogo na kutokwa jasho jingi ni ishara kwamba ana tatizo la moyo. Kuchoka haraka ni dalili kubwa na unaweza kukuta wengine hawakui vizuri kama watoto wa rika lao. Kwa mfano ikiwa amezaliwa na kilo mbili baada ya wiki mbili unaweza kukuta ana kilo hizohizo au zikiongezeka ni kidogo mno.

Mtoto akiumwa kifua mara kwa mara, wazazi na walezi hudhani ni tatizo la nimonia, lakini kumbe ni ugonjwa wa moyo. Mzazi anapoona mtoto anahema harakaharaka au anapata homa ya mapafu mara kwa mara, hizo zote ni dalili za magonjwa ya moyo.

KUHUSU MAFINDOFINDO

Kama mtoto ataugua mafindofindo (tonsillitis) na asitibiwe ipasavyo, huwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Ipo dhana mtoto akiugua mafindofindo wazazi wanamtibu kienyeji, wanakwenda dukani na kununua dawa za kumtibu au wanampatia maji ya moto anywe, hiyo si sahihi.

Vipo vyanzo vya aina mbili ambavyo husababisha tezi kuvimba, chanzo kikubwa kikiwa ni virusi na kwa asilimia ndogo husababishwa na bakteria. Hatumaanishi kwamba tezi zote zikivimba lazima upate dawa, isipokuwa ipo tezi ambayo ikivimba, lazima upewe dawa kutibu na hiyo aina ya tezi usipopata dawa ndipo unaishia kupata tatizo la moyo.

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yanapaswa kugundulika mapema ili kuokoa maisha ya mtoto. Katika kundi hili kuna magonjwa yapatayo saba, haya yanapaswa kugundulika mapema ingawa yapo mengine si magonjwa ya kuzaliwa nayo ambayo yanapaswa nayo kugundulika mapema kabla mtoto hajafikisha mwaka mmoja.

TIBA

Mtoto akizaliwa na magonjwa ya moyo, upasuaji hufanyika haraka. Kwa kuwa watoto wengi huwa hawagunduliki mapema na matokeo yake asilimia 25 hufariki dunia kabla ya kufikisha mwaka mmoja.

Asilimia nyingine 25 wakibahatika kufikisha mwaka mmoja na nusu hufariki dunia na wakifikisha miaka miwili hadi mitatu asilimia 80 hadi 90 hufa.

Watoto huchelewa kugundulika mapema kwani hucheleweshwa hospitalini kwa sababu magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo dalili zake hufanana na magonjwa mengine kama malaria, nimonia na utapiamlo.

Kwa kuwa zile dalili zinafanana na magonjwa mengine, wakati mwingine huchukua muda mrefu hadi mtu anayemuona mgonjwa ahisi kwamba mtoto anasumbuliwa na tatizo la moyo, wengine hufikishwa hospitalini wakiwa kwenye hatua mbaya.

Kuna aina ya magonjwa ya moyo ambayo mtoto huzaliwa nayo, hivyo anatakiwa afanyiwe upasuaji akiwa na mwezi mmoja, mitatu au mwaka mmoja, akizidi umri huo haiwezekani.

USHAURI

Uonapo dalili tulizozitaja hapa kwa mtoto wako, muwahishe hospitalini akapimwe ili apewe dawa sahihi.

Comments are closed.