The House of Favourite Newspapers

Chongo!-13

Ilipoishia wiki iliyopita
Wakati wakirejea, Noel akiwa kwenye usukani, walienda vizuri hadi walipofika njia panda ya Mbuyuni, wakitaka kuingia katika Barabara ya Bagamoyo. Lori moja kubwa, ghafla lilionekana kupoteza mwelekeo, likalifuata gari dogo la akina Noel na kuliparamia.Sasa endelea…

Watu waliokuwa jirani walijiziba nyuso na wenye mioyo midogo wakageukia upande wa pili huku wakipiga kelele za woga. Lori lile lililizoa na kusababisha kishindo kikubwa gari lile hadi upande wa pili kulikokuwa na korongo. Gari dogo likiwa mbele, lori lilifuatia nyuma.

Kishindo cha kutua kwa magari hayo mawili kilisababisha ukimya mkubwa eneo hilo. Ghafla, vumbi jingi likatanda, kiasi cha watu kushindwa kuona upande ule wa tukio. Mashuhuda walianza kusogea taratibu wakiwa na hofu kubwa. Kishindo kile hakikuonesha kama kungekuwa na mtu wa kupona.

Vumbi lilipotulia, watu wakasogea na uzuri zaidi, difenda ya polisi nayo ilisogea eneo hilo, gari dogo la akina Noel lilionekana limepinduka matairi yakiwa juu, wakati lori nalo lilikuwa limepinduka, kichwa chake kikiwa kimefinyangwa.

Kwa kutazama, ndani ya gari dogo hakukuonekana kama kulikuwa na mtu, lakini katika lori, watu wawili walionekana wakining’inia. Lilikuwa ni tukio la kutisha sana.

Kazi ya kutafuta majeruhi ikaanza mara moja. Baada ya dakika kama kumi hivi, miili ya watu wawili waliosadikika kutoka katika gari dogo ilikuwa imelazwa kwenye vitenge huku wakishindwa kujua kama walikuwa wamefariki au la. Mara moja polisi waliagiza watu hao kupandishwa kwenye difenda haraka kwa ajili ya kuwawahisha hospitali.

Kazi hiyo ilifanyika haraka na mara moja wakapelekwa katika hospitali ya karibu ya IMTU. Katika lile lori, watu nako wakaanza kushughulika kukata mabati ili kuwatoa watu wawili waliokuwemo ndani. Kwa jinsi walivyokuwa wametulia, hakukuwa na dalili kama walikuwa bado wazima.

Ilichukua kama nusu saa kumaliza kukata mabati ya kichwa cha lori hilo na kuwatoa watu hao wawili, ambao kwa kuwatazama kwa macho ya kawaida, walionekana kama walishafariki dunia.

Kipaza sauti cha polisi kikasikika; “Kama kuna mtu yeyote aliyeona idadi ya watu waliokuwa katika magari haya mawili kabla hawajapata ajali tafadhali, tunataka kujua kama tumewapata wote au la.”

Mtu mmoja ambaye gari lake lilikuwa nyuma ya gari dogo aliwafuata polisi na kuwaambia alikuwa nyuma ya mwenzake huyo kwa muda mrefu, aliwaona watu watatu wakiwa garini. Kwa maana hiyo, mtu mmoja alikuwa bado hajapatikana baada ya wale wanne.

“Ndugu wananchi, kuna mwenzetu mmoja hapa amekuja na kusema aliwaona watu watatu kwenye gari dogo, ina maana bado mtu mmoja, tuendelee kuhangaika, kila anayehisi sehemu ya kuweza kuwa na mtu atujulishe tafadhali,” tangazo la polisi lilirejea tena.

Pamoja na watu wote kushikwa na woga wa ajali hiyo ya kutisha, lakini alikuwepo kijana mmoja maarufu sana mitaa hiyo ya Mbuyuni kama Stan, alijulikana kwa tabia yake ya udokozi na mara nyingi alifanya hivyo kwenye matukio yote ya ajali yaliyotokea eneo hilo.

Kama mara tatu, alishalizunguka lori akitafuta kisanduku cha vifaa vya akiba maarufu kama Tool Box. Alikuwa na uzoefu wa kuuza kwa bei nzuri vitu hivyo, kwani kama mara mbili tatu alizofanikiwa kuondoka navyo, alipata hela nzuri iliyomfanya kila siku aombe ajali ya magari makubwa itokee.

Baada ya tangazo hilo, bila kujali wingi wa watu waliokuwa wamezunguka eneo hilo la ajali, akaanza kufunua kila palipojificha. Katika eneo la katikati ya lori hilo, ambapo palionekana kama pamekatika, turubai lilikuwa limeziba na kitu kama boksi likionekana kuvimba. Akafunua.

Alipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kuona mguu wa mtu eneo hilo, akapiga kelele na kuwaambia watu kuwa kuna mtu amemuona. Watu wakakimbilia eneo hilo na kuanza kufunua taratibu. Ni kweli, alikuwa mtu, lakini ambaye hakuonekana vizuri kama ni mtu mzima au mtoto na tena haikujulikana kama alikuwa hai au amekufa.

Wakafanikiwa kumnasua, hakuonekana kuwa na majeraha, lakini alikuwa amefumba macho na kwa haraka, ilikuwa vigumu kujua hali yake. Ni Bata.

Wakambeba na kumkimbiza katika gari la polisi lililokuwa linasubiri majeruhi. Mara moja, dereva akapiga moto na safari ya hospitalini ikaanza.
Je, nini kitawasibu Bata, Noel na Mzee Masta? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Comments are closed.