The House of Favourite Newspapers

Chongo!-23

0

Ilipoishia wiki iliyopita
Wakati watatu hao wakimaliza mazungumzo yao kwa maazimio hayo, Bata alikuwa na kikao akiwa na mpenzi wake Elina, pamoja na shemeji yake Jully, sehemu moja katikati ya Kariakoo.
Sasa endelea…

Kikao hicho kilihusu namna ya kufanya baada ya kutambua kuwa wabaya wa Bata walikuwa mjini. Bata mwenyewe alisisitiza nia yake ya kuwaangamiza wote, bila kuhitaji chochote kutoka kwao.
“Kwa jinsi ulivyotuonesha pale wanapoishi, sioni ni vipi tunaweza kuingia kirahisi na kufanikisha dhamira yako,” Jully alisema akimwangalia Elina, akihitaji sapoti yake.

“Labda tumsikilize mwenyewe atueleze anafikiria ataingiaje pale,” Elina naye alisema na hivyo macho ya wasichana wote wawili yakawa kwa Bata, ambaye alikohoa, ishara ya kujiweka sawa kabla ya kuanza kuzungumza.

“Kuna mdada nilizungumza naye siku ile nilipomuona Ame pale kwenye ile nyumba, anaonekana anajua mambo mengi yanayowahusu wale watu, nafikiri nimtafute nizungumze naye ili nijue namna gani tunaweza kufanya,” Bata aliwaambia, kauli ambayo waliipinga, wakidai suala hilo halitakiwi kuliweka wazi kwa mtu mwingine zaidi yao.

“Hapana,” Bata aliendelea “Ninachotaka kufanya ni kumsikiliza kwa mara nyingine, tunaweza kupata kitu cha kutufanya kupata njia rahisi ya kuwaingia.”

Wakamuelewa. Bata alimtafuta msichana yule kwenye simu na baada ya kutambuana, wakakubaliana kukutana kesho yake mitaa ya Posta, jijini Dar mchana kwa ajili ya kupata chakula cha pamoja. Muda ulipofika, Bata alimuongoza hadi alipotokea kwenye kibanda chao cha chakula.

Wakakaa kwenye meza moja, wakaagiza chakula kilichopikwa vizuri na Elina, wakaendelea na mazungumzo yao. Walizungumza mambo mengi, ikiwa ni pamoja na msichana huyo, ambaye alishajitambulisha kwa Bata kama anaitwa Mwani, kuuliza kwa nini alikuwa haonekani tena kijiweni, kwani walishamzoea.

“Sikiliza Mwani, mimi niko na shida naomba unisaidie,” Bata alisema na kumpa mshangao Mwani, kwani muda wote tangu alipoitwa na kukutana, alijua Bata atakuwa anamhitaji kimapenzi na alishakubali ndani ya nafsi yake.

“Shida unataka nikusaidie? Kama sikuelewi hivi, kuwa muwazi tafadhali,” Mwani alimwambia, akiwa haamini kama suala hilo halitahusu mapenzi.

Mimi ni muwazi, nataka msaada wako, naomba uniambie nifanyeje ili nipate kazi kwenye ile nyumba ya yule Al Shabaab kule mitaa ya kwenu,” Bata alisema huku akimtazama kwa makini ndani ya miwani yake.

Mwani akashtuka. Kazi kwenye ile nyumba? Akamtazama kwa macho yaliyojaa maswali ambayo Bata alikuwa anayaona.“Sikiliza nikuambie kitu Mwani, kwanza nakuamini sana, halafu ingawa ni msichana mdogo bado, najua unajua namna mwanamke anavyopata uchungu anapojifungua,” Bata alimwambia binti huyo aliyezidi kuchanganyikiwa kwa maneno hayo.

“Huo ndiyo uwazi Bata? Kama huna cha kuniambia tubadili mazungumzo bwana, wewe ni mwanaume, sema kitu mtoto wa kike nikisikie, wee vipi, mbona hujiamini,” Mwani aliongea kwa madoido, akijua fika Bata alimhitaji kimapenzi.

Bata alijiumauma huku akifikiria namna ya kumshawishi mrembo huyo, kwa sababu alisikiliza ushauri wa wenzake kuwa halitakuwa jambo la busara kama angemweleza ukweli binti huyo.

“Kwa hiyo kwako, shida yangu ya kazi katika ile nyumba haikuwashi? Najua wewe ni sista duu mjanja, nikipata mimi ndo umepata wewe. Lakini pia kama hujui namna ya kunishauri basi poa,” Bata aliongea kwa sauti iliyoonesha kukata tamaa, lakini kwa lengo maalum.

“Kwanza, wewe Bata nani kakuambia mle ndani wanatafuta mfanyakazi?” aliuliza Mwani akiwa katika hali ya kawaida, kitu kilichomfurahisha sana Bata.“Hakuna mtu aliyeniambia, lakini inavyoonesha kwa vyovyote watahitaji shamba boy, nyumba inaonesha ina bustani ndani,” alisema Bata na kusababisha kicheko kikubwa kutoka kwa Mwani.

“Utakuwa unaumwa wewe siyo bure, badilisha stori bwana kama vipi niruhusu nisepe,” Mwani alisema huku akichukua vijiti na kuchokonoa meno yake akitoa vipande vya kuku aliowala na chipsi.

“Sikiliza Mwani, najua huamini ninachokuambia na mimi wala sikulaumu kwa sababu hata mimi nisingeamini vilevile, kama ni hivyo basi, lazima ujue nina kitu ninachokihitaji kwenye ile nyumba, nisaidie,” alisema Bata, sasa akiwa ameukunja uso wake kuonesha anamaanisha.

Kauli hiyo ilimtisha Mwani, akili yake ikamrudisha nyuma na kukumbuka jinsi siku ile Bata alivyomkazia macho yule dada kiasi kwamba akili yake ilionekana kama imepotea kwa muda. Akakumbuka pia jinsi alivyokuwa akifurahia alipokuwa akimzungumzia yule dada. Akaanza kupata woga!

Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply