Costech Yamwaga Milioni 320 kwa Vijana Wabunifu wa Dijitali
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH ), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark nchini, imekabidhi mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 320 kwa vijana washindi 24 ambao wameandaa mawazo bunifu ya kibiashara na kidijitali kwa lengo la kujiajiri.
Hatua hiyo imekuja baada ya Costech kupitia Kituo atamizi cha teknohama Dar es Salaam (DTBi) kuandaa programu ya uwezeshaji vijana wabunifu kupitia mfumo wa digitali kwa lengo la kuwapatia mafunzo namna kuandaa mawazo ya kibiashara.
Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi mtaji washindi nane wa awamu ya pili ya mashindano hayo jijini Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu alitoa wito kwa vijana kutokata tamaa kwa kuwa serikali inawatafutia fursa za kujikwamua kiuchumi kwa kutumia njia mbalimbali.
Alitoa wito kwa washindi ambao wamefanikiwa kupatiwa mitaji hiyo kufanya biashara kwa ari ili waweze kuwaajiri vijana wenzao.
Alisema vijana wanapoona kuna fursa yoyote wasisite kushiriki kwa kuwa penye ushindani ndipo mshindi hupatikana bila upendeleo.
“Lengo letu ni vijana kujiajiri na kutoa ajira kwa wenzetu kama sehemu ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.
Aidha, Mkurugenzi wa fedha na Utawala kutoka Atamizi ya Teknohama Dar es salaam (DTBi), Makange Mramba alisema katika program hiyo ya kuwapatia mafunzo vijana wabunifu wa vyuo vikuu, awamu ya kwanza ya mashindano hayo washindi 16 walipatiwa mitaji ya sh milioni 205 wakati katika awamu ya pili vijana nane wamepatiwa sh milioni 120.
Alisema licha ya washindi hao kupatiwa mitaji kulingana na mawazo yao ya kibiashara, washiriki wengine ambao hawakushinda pia walipatiwa mafunzo ya kuandaa maandiko bunifu ya kibiashara ambapo tangu programu hiyo ianzishwe mwaka jana tayari washiriki zaidi ya 1000 wamepatiwa mafunzo.
“Kwa hakika tumevuka hata malengo yetu tuliyojiweka kwa zaidi ya asilimia 130,” alisema.
Naye Meneja Biashara na Maendeleo (DTBi), Gasper Mdee alifafanua kuwa licha ya vijana wachache kupatiwa mitaji hiyo lakini mafunzo waliyopatiwa washiriki wote yanawawezesha kuandika maandiko bunifu ya kibiashara yenye ushawishi wa kupata mitaji katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha, Kiongozi wa Sekta ya Maendeleo kutoka Ubalozi Denmark, Jema Ngwale alitoa wito kwa taasisi mbalimbali zinatoa fursa kwa vijana, kuwapa kipaumbele vijana wa kike ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Pia nawashauri vijana kupanua wigo kwa kubadilishana uzoefu kwa kupitia kwa marafiki ili kukuza wazo lako na kuona namna gani unaweza kuvuka, ili usivuke peke yako,” alisema.
Mmoja wa washindi hao Othuman Waziri alisema; “Wazo langu ni kutengeneza Boxpesa ambayo ni progamu maalumu itakayowasaidia Watanzania kutunza fedha zao kwa njia ya mitandao kwa muda maalumu”.
Wakati Irene Sinare alisema wazo lake kutengeneza mifuko maalumu mbadala ambayo ina uwezo wa kupotea kwenye udongo ndani ya siku 180.
“Mifuko hii imetengenezwa kwa malighafi ambayo ni rafiki wa mazingira, na imekuja wakati maufaka ambao serikali imepiga marukufu matumizi ya mifuko ya plastiki kwani inachukua miaka 500 kupotea kwenye udongo,” alisema.
NA MWANDISHI WETU
Comments are closed.