The House of Favourite Newspapers

Dada wa Msuya Kuchinjwa… Mchezo ni Huu

1

7

Jeneza lenye mwili wa marehemu.

Na Waandishi Wetu, UWAZI

DAR ES SALAAM: Bado habari ni moto! Majonzi yanaendelea kutawala kwenye familia ya Bilionea Erasto Msuya (43) aliyeuawa kwa kupigwa risasi Agosti 8, 2013, Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) kufuatia safari hii, mdogo wake wa kike, Aneth Simon Msuya (30) naye kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana, Uwazi limebaini mchezo mzima.

1Marehemu Aneth Simon Msuya

Aneth (pichani) alifanyiwa ukatili huo, Mei 26, mwaka huu chumbani, nyumbani kwake, Block 16, Kibada- Kigamboni jijini Dar es Salaam akiwa na mtoto wake, Allan Kimario.

Mauaji hayo yaligunduliwa na jirani asubuhi baada ya mtoto wa marehemu, Allan kwenda kusema mama yake haamki na yeye anataka kwenda shule huku basi la shule likiwa limemwacha. Pia alisema anahisi njaa.

Erasto-11Feb2015Marehemu Erasto Msuya

Jirani huyo aliongozana na mtoto huyo hadi ndani na kuubaini mwili huo ukiwa umalala sakafuni kwenye dimbwi la damu na kisu kilichotumika kumchinjia kikiwa pembeni yake na hivyo kutoa taarifa polisi.

4NI TUKIO LA KUSIKITISHA SANA

Tangu kutokea kwa tukio hilo, vyombo mbalimbali vya habari nchini vimekuwa vikiripoti tukio hilo katika njia za kusikitisha sana kutokana na unyama aliofanyiwa Aneth na ndipo, Uwazi nalo likazama mitaani kuchimba kwa kina ili kuwapa wasomaji wake mambo mapya zaidi.

14.Dada wa marehemu akishindwa kujizuia na kulia kwa uchungu.KUNA WATU WAMEPANGA KUIFUTA FAMILIA HIYO

Madai yaliyosambaa ni kwamba, kuna kundi la watu limepanga mkakati mzito wa kuhakikisha familia ya Msuya inafutika kwenye uso wa dunia kutokana na kisasi cha kibiashara (bila kufafanuliwa).

“Ilivyo ni kwamba, baada ya kaka yao (Erasto) kuuawa, kwa kupigwa risasi, kuna kundi la watu limeamua kuifuta familia hiyo kwenye uso wa dunia. Ndiyo maana mbali na Aneth kuchinjwa, kuna akina Msuya wengine wameshakumbana na vitendo vya kuashiria kwamba, roho zao zinasakwa

13HAUSIGELI ATAJWA MTUHUMIWA MKUU

Kwa mujibu wa chanzo kimoja toka ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, msichana anayedaiwa kufanya kazi za ndani ‘hausigeli’ nyumbani kwa marehemu Aneth na kuondoka siku ya mauaji hayo, anapewa nafasi ya kwanza katika kuchunguzwa akisemekena kuujua mchezo mzima wa kifo cha bosi wake huyo na sasa jeshi hilo linamsaka kwa udi na uvumba.

“Kwanza nataka kusema kuwa, hausigeli ndiye mshukiwa wetu wa kwanza ndani ya jeshi la polisi. Huyu msichana wa kazi aliondoka mchana, usiku yakatokea yaliyotokea, akipigiwa simu hapatikani.

“Huyu tunamtuhumu kuujua mchezo wote. Kwa hiyo pa kuanzia kwetu tunafanya juu chini kumpata ili aisaidie polisi,” kilisema chanzo hicho huku kikiomba hifadhi ya jina kwa vile, si msemaji sahihi wa jeshi hilo.

ALIPANDIKIZWA?

Pia, chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, utafiti wa awali wa jeshi hilo unataka kukubaliana kwamba, kutokana na mlolongo unaotokea wa mauaji au kujeruhiwa kwa watu mbalimbali wa familia ya Msuya, kuna uwezekano msichana huyo wa kazi alipandikizwa na watu hao kufanya kazi kwa Aneth.

“Kuna wasiwasi yule dada wa kazi alipandikizwa. Kuna uwezekano alifika pale katika njia za mtego ili kumsoma Aneth na mazingira yake pamoja na mwenendo, sasa baada ya kukamilisha ndiyo akaamua kuondoka na usiku wauaji wakafika. Kwa hiyo hayo yote sisi polisi tunayachunguza,” kilisema chanzo.

WAUAJI WALIINGIAJE NDANI?

Kwa mujibu wa chanzo hicho, inaaminika kwamba, wauaji hao walifanikiwa kuzipata funguo halisi za geti kubwa la mlango wa kuingilia sebuleni kwa Aneth, wakaenda kuchongea nyingine ambazo siku walipofika, waliweza kufungua geti na kuingia kama kwao.

“Lile geti kubwa linafunga kwa nje na funguo, kwa ndani unavuta loki tu. Kwa hiyo wao waliingia ndani kwa kufungua. Walipomaliza kutenda ukatili wao, inaonekana walifunga geti kubwa kwa kuloki ambapo kwa mtu mwingine wa nje asingeweza kuingia ila yule mtoto (Allan) aliweza kutoka nje kwa sababu loki yake ni ya kubetua tu.”

KWA NINI WAUAJI WALIIBA TIVII TU?

Chanzo hicho kikasema kuwa, watuhumiwa hao hawakuiba kitu zaidi ya tivii (flat) lakini inaonekana kwamba waliamua kuichukua runinga hiyo kwa vile waliamini ni skrini kwa ajili ya kamera za ulinzi (Closed-Circuit Television au CCTV) ambapo walijua picha zao zilichukuliwa. Hata hivyo, tivii hiyo waliitupa mbele ya safari.

HAIKUWA RAHISI KUMCHINJA ANETH

Chanzo hicho kilisema kuwa, mazingira ya chumba yalionesha kuwa, kabla ya kuchinjwa, kulikuwa na purukushani kubwa kwani neti ilikutwa imechanwa, baadhi ya vitu vimepinduliwa, vingine vimezagaa kila mahali hali ambayo iliashiria kuwa, marehemu hakukubali kuchinjwa kirahisi.

MAISHA YA ANETH

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wakidai kumjua dada huyo, walisema kuwa, baada ya  kifo hicho wamebadili mawazo kuhusu yeye kuwa huenda alijua anawindwa.

“Awali tulijua ni dada anayeringa, kwani alikuwa akifika dukani, anaegesha gari jirani kabisa na mlango wa duka kisha anaagiza kitu anachokitaka, anapelekewa, analipa pesa anaondoka.

“Hata siku tatu kabla ya kifo, alifika kwenye kibanda cha chipsi, akaagiza na kufungiwa akiwa ndani ya gari. Alikuwa hana kawaida ya kushuka, huenda alijua anawindwa,” alisema mkazi mmoja wa maeneo ya Kibada huku akiomba hifadhi ya jina lake.

SIMU ZA KUULIZWA ALIPO

Mmoja wa watu waliodai kufanya kazi na marehemu wizara ya fedha, alisema kuwa, wiki chache nyuma, Aneth aliwahi kusema kuwa, kuna wanaume wamekuwa wakimpigia simu na kumuuliza; Aneth uko wapi?’ lakini akiuliza we nani? Simu inakatwa!

“Huenda wale watu nao si sehemu ya watuhumiwa hawa. Maana hali hiyo alisema hakuwahi kukumbana nayo siku za nyuma. Baada ya kusikia amechinjwa sasa nahisi huenda Aneth alifuatiliwa kwa siku nyingi nyuma lakini yeye alikuwa hajui,” mtu mmoja aliliambia Uwazi kwa kumkariri mfanyakazi mmoja wa wizara hiyo.

MAISHA YAKE NA MAJIRANI

Baadhi ya majirani na nyumba ya marehemu walisema kuwa, haikuwa rahisi kubaini mienendo ya watu wasioeleweka nyumbani kwa Aneth kwa vile maisha yake yalikuwa hayasomeki kwa mwanga wa kawaida.

“Alikuwa akikuona anakusalimia akiwa ndani ya gari, akiingia kwake ameingia. Sasa isingekuwa rahisi kumjua kwa undani yeye na wageni wanaofika kwake. Lakini mimi nimewahi kusikia kwamba, Aneth aliolewa ila kwa bahati mbaya ndoa yake ilivunjika mwaka mmoja na baba wa mtoto wake,” alisema jirani mmoja kauli ambayo pia ilithibitishwa na dada mmoja wa Aneth.

NDUGU WASHTUKA, WAWEKA MLINZI

Gazeti la Uwazi pia lilifanikiwa kufika nyumbani kwa marehemu ambapo lilikuta nyumba inalindwa na mlinzi ambaye alisema aliwekwa hapo baada ya mauaji hayo.

UWAZI OFISINI KWA RPC TEMEKE

Hayo yote yalikuwa maneno mbalimbali ya vyanzo vyetu, hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Gilles Mroto ili kumsikia kama ana mtiririko huo, lakini kwa upande wake, alisema kuwa, wapo katika msako mkali kuwasaka wauaji hao.

“Hata huyo hausigeli pia tunamsaka sana ili kulisaidia jeshi la polisi kwa vile uondokaji wake na mauaji kuna utata,” alisema Kamanda Mroto.

MATUKIO YA KUIANDAMA FAMILIA

Tangu kutokea kwa mauaji ya Erasto, kumekuwa na matukio mengi ya kuiandama familia hiyo kwa kutaka kuwatoa roho wahusika.

KUNA ALIYEMWAGIWA SUMU

Dada wa Aneth aliyetajwa kwa jina la Antuja aliwahi kumwagiwa kitu kinachosadikiwa kuwa ni sumu wakati akiwa amelala chumbani na mtoto wa Aneth, Allan hivyo kuathirika na sumu hiyo.

TUKIO LA HONGERA BAR

Desemba mwaka jana, dada mwingine aitwaye Ester na muwewe walipigwa risasi mgongoni na kifuani wakiwa katika Baa ya Hongera, Kijitonyama, Dar.

Mwili wa Aneth alisafirishwa jana kwenda Kijiji cha Kairo, Mererani, Simanjiro, Manyara kwa mazishi. Mungu aiweke pema peponi, roho yake. Amina.

1 Comment
  1. MARY says

    kwa kweli huyo mtoto aliniliza. hivi angefanikiwa kuliwahi gari la shule si angeondoka na angerudi asingeweza kufungua tena geti kwani lingejifunga. Marehemu mwili ungeendelea kuoza. Na mtoto pia angeenda shuleni na njaa kumbuka hakula tokea jana yake, pengine angepewa chai au uji saa nne. Real pain, ila Mungu naomba ukanene nao.
    Huyu mtoto amelala kwenye kochi tokea usiku yawezekana saa ilikuwa saa moj a au saa mbili kwani walikuwa bado hawajala chakula cha usiku. SPEECHLESS, GOD WILL JUDGE ON IT.
    Mtoto amemiss mapenzi ya mama na raha alizokuwa anapewa na mama yake………

Leave A Reply