The House of Favourite Newspapers

Dawa anazopaswa, asizopaswa kutumia mgonjwa wa selimundu

SELIMUNDU (Sickle cell) ni ugonjwa wa kurithi ambao hutokea baada ya mwili wa binadamu kuwa na upungufu katika umbile la seli hai nyekundu za damu, ambapo umbile la seli hubadilika na kuwa nusu duara au umbile la mundu badala ya umbile la mduara.  Hali hii ya umbile la seli kufanana na mundu kumefanya seli hizi kuitwa jina la selimundu au kwa kitaalamu sickle cell. Wastani wa kuishi kwa seli hai nyekundu za damu ni siku 120, lakini kwa selimundu wastani wa seli hai kuishi au kuzunguka katika mzunguko wa damu ni siku 10 hadi 20. Hii imekuwa sababu ya kwa nini mtu mwenye sikoseli anapatwa na upungufu wa damu mara kwa mara.

Hapa nchini, takwimu zinaonyesha kuwa watu wengi wanaugua ugonjwa huu. Katika makala haya ni vyema tukakumbushana juu ya dalili pamoja na dawa ambazo hutumika kutibu sikoseli. Seli hizi muda wake wa kuishi unapokuwa umefikia kikomo, zinapokuwa katika mzunguko wa damu husababisha damu kushindwa kufika katika baadhi ya viungo mwilini kama vile mapafu, figo na ini.

Damu hushindwa kufika katika maeneo hayo kutokana na seli hizo kuziba mishipa ya damu. Matokeo ya damu kushindwa kufika katika baadhi ya viungo ni kusababisha viungo hivyo kushindwa kupata hewa ya kutosha, sukari, virutubisho na hatimaye kuumia kwa viungo hivyo.

Hali hiyo ya kuumia kwa baadhi ya viungo kutokana na damu kushindwa kufika, na selimundu kuendelea kuwapo katika mzunguko wa damu, husababisha mtu apatwe na dalili mbalimbali zikiwamo hizi zifuatazo:

Dalili za mtu mwenye sikoseli ni pamoja na maumivu makali ya mwili, kuchoka, kuishiwa damu mara kwa mara, kuvimba au kujaa kwa miguu au mikono, kushindwa kupumua vizuri/ kubanwa na kifua, kupatwa na magonjwa ya kuambukiza, vidonda, magonjwa ya moyo na wakati mwingine huweza kusababisha matatizo katika maumbile ya mwanamume kwa kitaalamu huitwa Priapism.

Pamoja na kwamba sikoseli ni tatizo au ugonjwa unaohusu damu moja kwa moja, ni vyema tahadhari ikachukuliwa juu ya aina za dawa na matibabu yake kwa ujumla. Miongoni mwa dawa ambazo ni za kuchukua tahadhari katika matibabu ya sikoseli ni pamoja na zile ambazo ndani yake kuna mchanganyiko wa madini ya chuma (Iron supplements) mfano FEFO.

Dawa au virutubisho vyenye mchanganyiko wa madini ya chuma mara nyingi vimekuwa vikitumika katika matibabu ya kuongeza damu mwilini, lakini hizi ni dawa ambazo tahadhari kubwa inahitajika kuchukuliwa kwa mgonjwa wa sikoseli. Sababu kubwa ya mtu mwenye sikoseli kuepuka matumizi ya dawa zenye mchanganyiko wa madini ya chuma ni kwamba sikoseli haijasababishwa na upungufu wa madini ya chuma, hivyo mgonjwa kutumia dawa zenye madini hayo kutasababisha mwili wake kujenga ziada ya madini hayo yanayoweza kusababisha uharibifu katika viungo vyake vya mwili.

Dawa ambayo ni rafiki kwa mgonjwa wa sikoseli katika kusaidia mgawanyiko wa seli na kuwezesha damu kuongezeka ni Folic Acid.

Kwa kuwa moja ya dalili ya sikoseli ni maumivu makali ya viungo au mwili ambayo husababishwa na selimundu kuziba mirija midogo ya damu, matumizi ya dawa za kawaida za maumivu mfano paracetamol yamekuwa ni msaada kwa mgonjwa wa sikoseli, matumizi ya dawa yatazingatia hali ya kiafya ya mgonjwa kwa kuwa si kila dawa itakuwa bora kwa kila mtu, miili ya watu hutofautiana.

Mtu mwenye tatizo la sikoseli bado anao uwezo wa kushiriki shughuli zozote zile za kijamii kama ilivyo kwa watu wengine. Jambo la kufanya ni kuzingatia ushauri na kufuatilia matibabu anayopewa na wataalamu wa afya.

 

Comments are closed.