The House of Favourite Newspapers

Dunia uliyoiacha nyuma yako – 59

1

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Baadaye Magesa anagundua kwamba Grace ni jasusi wa kimataifa, akiwa amebadilisha jina na mwonekano wake, jambo linalompa hofu kubwa ndani ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo anamuelewesha hali halisi.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu.
Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinazidi kupamba moto lakini ghafla Mandiba anajikuta akiwa matatizoni baada ya kugundua kuna watu wanamfuatilia.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Gari lilizidi kuchanja mbuga, Mandiba akawa anabadili barabara kwa makusudi lakini kila alipokuwa akikata kona, wale watu waliokuwa kwenye bodaboda nao walikuwa wakikata na kumfuata. Akazidi kuongeza kasi, gari likawa linakwenda kwa kasi kubwa na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amekaribia nyumbani kwake.

Kama alivyokuwa ameagiza alipompigia simu mkewe, kwa mbali aliona geti likiwa limefunguliwa lakini katika kile ambacho hakutaka kukiamini, alishtuka kuona watu wengine wawili, waliokuwa kwenye bodaboda na kuvalia makoti meusi kama wale waliokuwa wakimfukuza kwa nyuma, wakiwa wamepaki bodaboda yao katikati ya barabara, mita kadhaa kutoka nyumbani kwake, huku mmoja akiwa ameshuka na kumnyooshea bunduki huku akimuamuru kusimama.
“Mungu wangu!” alisema Mandiba na muda mfupi baadaye, kishindo kikubwa kilisikika eneo hilo.

Vumbi jingi lililochanganyikana na moshi lilitanda pale getini, majirani wakaanza kufunua mapazia ya madirisha yao kuchungulia kuna nini huku wengine wakifungua milango na kutoka lakini gahfla, wote walishtushwa na milio mfululizo ya risasi iliyoonesha kuna watu walikuwa wakirushiana risasi.
Muda mfupi baadaye, mlio wa bodaboda iliyokuwa inaondoka kwa kasi eneo hilo ulisikika, ukifuatiwa na milio mingine kadhaa ya risasi. Majirani waliokuwa wameanza kutoka, wote walirudi ndani kwa hofu ya kilichokuwa kinaendelea kwani ilionesha kuna tukio zito linaendelea usiku huo.

Baada ya kuona maji yamemfika shingoni, Mandiba aliamua kuchukua uamuzi mgumu ambao kama isingekuwa roho yake ya kijasiri, asingeweza kuuchukua. Aliamua kunyoosha gari kuelekea pale wale watu wengine wawili walipokuwa wamesimama, akakanyaga mafuta na kufumba na kufumbua, akawazoa wote wawili pamoja na bodaboda yao.

Kutokana na kasi ambayo gari lilikuwa nayo, baada ya kuwagonga alishindwa kulimudu, likaruka na kwenda kugonga uzio wa nyumba yake na kusababisha ukuta ubomoke, vumbi jingi likatanda eneo hilo sambamba na moshi wa gari.
Wale majambazi wengine wawili waliokuwa wakilifuata gari lake kwa nyuma, walipoona amewagonga wenzao, walipandwa na hasira zaidi, wakaanza kulimiminia gari la Mandiba risasi kwa lengo la kummalizia.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kama walivyodhani kwani mafunzo ya kijeshi aliyopitia, ukichanganya na uimara wa gari alilokuwa akitumia, vilimfanya Mandiba anusurike kwenye ajali ile, harakaharaka akafungua mkanda wa siti aliokuwa amejifunga na kuingiza mkono kwenye ‘dashbord’ ya gari iliyokuwa imefunguka yenyewe kufuatia kishindo cha kugonga ukuta.

Harakaharaka akaikoki bastola yake na aliposikia mlio wa risasi kutoka kwa wale watu waliokuwa wakimfuatilia kwa nyuma, hakutaka kulaza damu, naye akawajibu kwa kuwafyatulia risasi.
Majibizano yaliendelea, wale majambazi walipoona Mandiba anaendelea kuwashambulia, tena akiwakosakosa risasi kwa karibu kabisa, waliamua kuondoka kwa kasi kubwa na bodaboda yao, wakaendelea kufyatua risasi ili kuwatisha watu wengine wasiwafuatilie.
Muda mfupi baadaye, magari mawili ya polisi yalifika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada kwa Mandiba kwani tayari mkewe alishatoa taarifa polisi muda mfupi baada ya kupigiwa simu na mumewe.

“Upo salama mkuu?” askari mmoja alimuuliza Mandiba baada ya kufanikiwa kumchomoa kutoka kwenye gari lake. Mandiba hakujibu chochote zaidi ya kukohoa kwa nguvu, askari wakamsaidia kumtoa eneo hilo na kumsogeza pembeni ambapo alizungumza kwa taabu na kuwaeleza kwamba chini ya gari kulikuwa na majambazi wengine walionasa.
Ilibidi askari mmoja aingie ndani ya gari na kujaribu kuliwasha, likawaka ambapo alilirudisha nyuma, wote wakapigwa na butwaa kugundua kwamba kumbe kulikuwa na watu aliowagonga wakiwa na bodaboda yao.

Kutokana na jinsi alivyowabamiza ukutani, hakuna aliyekuwa anatamanika, kuanzia wao wenyewe mpaka bodaboda yao. Harakaharaka askari waliwatoa eneo la tukio na kuwaingiza kwenye gari moja la polisi, wakawakimbiza hospitali wakiwa chini ya ulinzi mkali.
“Tukupeleke hospitali mkuu?”
“Hapana, niko salama kabisa, nakohoa kwa sababu ya vumbi lakini hakuna nilipoumia,” alisema Mandiba kwa kujiamini.
Kila mmoja alimpongeza Mandiba kwa ujasiri aliouonesha kwani kama asingefanya vile, huenda siku hiyo ndiyo ingekuwa ya mwisho kwenye maisha yake. Kutokana na tukio lenyewe, ilibidi askari wailinde nyumba ya Mandiba mpaka asubuhi ya siku iliyokuwa inafuatia.

Baada ya kufikishwa hospitalini, ilibainika kuwa mmoja kati ya wale watu amefariki dunia lakini mwingine bado alikuwa hai ingawa hali yake ilikuwa mbaya.
“Inabidi mfanye kila kinachowezekana kuhakikisha anapona, huyu ndiyo atatueleza kwa nini walikuwa wanataka kumuua Mandiba na wametumwa na nani,” alisema mkuu wa upelelezi, kauli iliyoungwa mkono na kila mtu.
Akalazwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi lakini mkononi akiwa amefungwa pingu, madaktari wakawa wanahangaika kuhakikisha anapona.
Upande wa pili, tukio la kuvamiwa kwa Mandiba lilileta mshtuko mkubwa hasa kwa wenzake waliokuwa wakifanya naye kazi, wakahisi huenda kuna uwezekano mkubwa kuna mtu alikuwa anavujisha taarifa za uchunguzi wao kumhusu waziri mkuu, ikabidi kazi ya ziada ianze kufanywa kubaini ni nani aliyekuwa akivujisha taarifa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment
  1. herieth says

    nzuri sana

Leave A Reply