The House of Favourite Newspapers

Dunia uliyoiacha nyuma yako – 63

1

Ufisadi mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, ukiwahusisha viongozi wakuu wa nchi, unamsababishia matatizo makubwa waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa. Inatengenezwa ajali ambayo kama isingekuwa msaada mkubwa wa jasusi wa kimataifa, Grace, huenda huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yake.

Anaokolewa kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu na kuwafanya watu wote waamini kwamba amekufa. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kutokana na upelelezi huo inabainika kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bandundu Musyoka, alikuwa akihusika kuanzia kwenye ufisadi mpaka kwenye kupanga njama za vifo vya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mwampashi pamoja na Magesa.

Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinakuwa ngumu kutokana na nguvu aliyonayo serikalini. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba aliyekuwa akiongoza uchunguzi wa sakata hilo, anabambikwa kesi ya mauaji na kukamatwa na kabla hilo halijaisha, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jordan Ngai naye anaanza kuwindwa.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jordan Ngai aliamua kwenda kujiliwaza kwenye Hoteli ya Coral Cliff kwani alihisi kichwa chake kimeelemewa na mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea kwenye sakata la Magesa, likiwemo tukio la kiongozi wao kwenye upelelezi huo, Mandiba kubambikiwa kesi ya mauaji.

Kwa kawaida, anapokuwa na msongo wa mawazo, Ngai alikuwa akipenda kuogelea na kuendesha boti maalum za kwenye maji zinazofanana na pikipiki, akapanga kwamba siku hiyo akifika kwenye hoteli hiyo, atakula, kunywa na kisha kuelekea baharini mpaka jioni kabisa ndiyo arudi nyumbani kwake.
Hakumuaga mtu yeyote, hata mkewe hakuwa akijua yupo wapi zaidi ya kuamini kwamba anaendelea na shughuli zake za kikazi kama kawaida.

Akiwa anaendesha gari lake kwa mwendo wa wastani, alishtuka kuona gari dogo jeusi likija kwa kasi kubwa nyuma yake huku dereva akipiga honi na kuwasha taa na kuzizima kama anayemhimiza aongeze kasi. Kutokana na jinsi alivyokuwa na msongo wa mawazo, Ngai hakutaka kufanya kama yule dereva wa gari lililokuwa nyuma yake alivyokuwa anataka kwani alihisi anaweza kusababisha ajali.

Alichokifanya, aliwasha ‘indiketa’ ya upande wa kushoto akimpa ishara yule dereva apite na kuendelea na safari zake, akalisogeza gari lake mpaka pembeni kabisa ya barabara na kusimama lakini tofauti na alivyotegemea, gari lile halikupita na badala yake nalo likasimama nyuma yake.

Kwa kuwa tayari alishahisi hali ya hatari na kwa muda huo hakuwa akijua nani wa kumuamini, harakaharaka alitoa simu yake na kutuma meseji kwenye namba ya Grace.

“Nipo matatizoni, kuna watu wananifuatilia,” ulisomeka ujumbe huo, harakaharaka akautuma kisha akabonyeza kitufe kwenye simu hiyo cha kutoa sauti kwamba simu ikipigwa au meseji ikiingia, isitoe mlio wowote, akaisukumia chini ya siti ya dereva aliyokuwa amekalia. Akashusha pumzi ndefu na kutulia kwenye siti yake.
Mwanaume mwenye mwili mkubwa alishuka kwenye lile gari lililokuwa limepaki nyuma yake na kuanza kulisogelea gari la Ngai, akawa anamtazama mwanaume huyo akija kibabe kupitia vioo vya pembeni (side mirrors), akawa anajiuliza maswali yaliyokosa majibu.

Kingine alichokifanya, aliingiza mkono kwenye ‘dashboard’ ya gari lake na kutoa bastola, harakaharaka akaikoki na kuiweka tayari kwa chochote, akatulia nyuma ya usukani. Ghafla alisikia kioo cha upande wake kikigongwa kwa nguvu, alipogeuka kumtazama aliyekuwa anagonga, aligundua kuwa ni yule mwanaume aliyetoka kwenye gari la nyuma yake akimtaka ashushe kioo, akashusha.

“Leseni yako tafadhali,” alisema mwanaume huyo kwa sauti nzito. Ngai hakuwa mbishi, akatoa leseni yake na kumpa ingawa kwa kumtazama tu, aligundua kwamba hakuwa askari kwa sababu kwanza hakuwa amevaa sare za askari wa usalama barabarani na pia alikuwa na ndevu nyingi na tatuu shingoni, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi.

“Kwa nini unaendesha gari kizembe na kusababisha foleni? Umejifunzia wapi udereva wako?” alisema mwanaume huyo, Ngai akageuza shingo na kumkazia macho, naye akamuuliza yeye ni nani wa kumhoji swali kama hilo. Kabla hajajibu, Ngai alishtuka kuona wanaume wengine watatu waliokuwa wamevalia makoti marefu meusi wakija kwa kasi kutokea kwenye lile gari.

“Unataka kujua mimi ni nani si ndiyo? Haya teremka kwenye gari haraka kwa usalama wako,” alisema mwanaume yule huku akimgusisha bastola Ngai kwenye paji la uso wake.

Japokuwa na yeye alikuwa na bastola lakini alipoona wale wanaume wengine wakija huku kila mmoja akichomoa bunduki kutoka kwenye makoti marefu waliyokuwa wamevaa, alijua ubishi wa aina yoyote unaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi. Ikabidi ainue mikono na kutii alichoambiwa.

Mlango wa dereva ukafunguliwa ambapo yule mwanaume alimkwida juujuu na kumvurumisha chini huku akimsindikiza na teke zito lililotua barabara kwenye mbavu zake za upande wa kulia, Ngai akapiga kelele kuonesha kwamba alikuwa kwenye maumivu makali.

Tayari wale wanaume wengine walishafika eneo hilo, wakamfunga pingu mikononi na kumfunga kwa kitambaa cheusi machoni, wakamuingiza kwenye siti za nyuma za gari lake, yule aliyekuwa wa kwanza kumfuata akaingia na kukaa nyuma ya usukani, akawasha gari na kuondoka kwa kasi huku yule mmoja aliyesalia chini akikimbilia kwenye gari lao walilokuja nalo, naye akawasha na kuanza kulifuata lile gari alilokuwemo Ngai aliyekuwa akiendelea kuugulia maumivu makali.

“Kwani nimewakosea nini jamani?”
“Utaenda kujua mbele ya safari, leo ndiyo mwisho wako kenge wewe! Hii ndiyo dawa ya vijitu vinavyoingilia dili za watu hapa mjini,” alisema yule mwanaume aliyekuwa nyuma ya usukani huku akizidi kukanyaga mafuta na kulifanya gari likimbie kwa kasi kubwa mno.

Ngai hakuelewa tena wanampeleka wapi, safari yake ya kwenda hotelini Coral Cliff iliishia mikononi mwa watu hao walioonesha waziwazi kuwa na dhamira ovu.
*   *   *
Baada ya ndege aliyopanda kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, abiria walianza kuteremka, Grace akiwa miongoni mwao. Baada ya kukamilisha taratibu zote uwanjani hapo, Grace alibeba begi lake la ukubwa wa wastani na kutoka hadi kwenye maegesho ya teksi, akakodi teksi moja na kumuelekeza sehemu ya kumpeleka.

“Hyatt Regency Hotel, itakuwa shilingi ngapi?”
“Elfu ishirini tu sista! Tena gari yangu ina full kiyoyozi na muziki wa nguvu, haikai kwenye foleni hii, si unaona mwenyewe,” dereva teksi alimjibu Grace kwa mbwembwe huku akifungua milango ya nyuma na kumsaidia mteja wake kuingiza mizigo. Grace hakuwa na cha kusema zaidi ya kutabasamu tu kutokana na uchangamfu wa dereva huyo.

Muda mfupi baadaye, safari ilianza kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam ilipokuwepo hoteli hiyo. Baada ya kufika kwenye taa za kuongozea magari za Tazara ambapo taa nyekundu ilikuwa imewaka ikiyazuia magari yanayotokea uwanja wa ndege na maeneo mengine, Grace alitoa simu yake kwani tangu ashuke kwenye ndege hakuwa ameiwasha.

Alipoiwasha tu, meseji ya kwanza kuingia ilikuwa ni kutoka kwa Ngai iliyosomeka: “Nipo matatizoni, kuna watu wananifuatilia.” Alipotazama muda iliyotumwa, aligundua kwamba hazikuwa zimepita hata dakika saba tangu ilipotumwa.
Harakaharaka aliwasha laptop yake na kufungua program ya kisasa ya GPRS Satellite Tracer, akabonyezabonyeza na muda mfupi baadaye, ramani ya satelaiti ikionesha jiji zima la Dar es Salaam ilifunguka huku kukiwa na kidoa chekundu kilichozungushiwa alama nyekundu kikiwaka na kuzima.

Akaikazia macho laptop yake na kabla hata taa za kuongozea magari hazijaruhusu, alimuelekeza dereva kubadilisha uelekeo na kukata kuelekea upande wa Buguruni.

“Sista kwa nini tupite huku? Tutazunguka sana,” alisema dereva huyo lakini Grace akamtaka kutokuwa na wasiwasi, amepatwa na dharura na yupo tayari kumlipa kiwango chochote ambacho atataka ilimradi afuate alichokuwa anamueleza.
Kwa kuwa alikuwa na ‘njaa’ ya pesa, dereva huyo alikubali, akapenyepenya na kufanikiwa kuingia Barabara ya Mandela, akakanyaga mafuta kama Grace alivyomuelekeza na kuifanya teksi ikimbie kwa kasi kubwa. Akawa anaendelea kumhimiza kuongeza kasi huku akiendelea kubonyezabonyeza laptop yake pamoja na simu. Alishajua mchezo mzima ulivyokuwa unaendelea na akajua huo ndiyo muda muafaka wa kuwadhihirishia watu wote aliyekuwa nyuma ya matukio hayo ya kihalifu.

“Kata kulia hapo halafu ongeza kasi,” alisema Grace lakini alipomuona dereva huyo hamuelewi, alimuamuru kusimama, akatii alichoambiwa ambapo kwa kutumia ubabe, Grace alimtoa kwenye siti ya dereva na kumkalisha pembeni, akakaa mwenyewe nyuma ya usukani na kuliondoa gari hilo kwa kasi ambayo ilimshangaza sana dereva huyo wa teksi. Mwonekano wa Grace na mambo aliyokuwa akiyafanya vilikuwa vitu viwili tofauti kabisa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne kwenye Gazeti la Uwazi.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

1 Comment
  1. abubakari makumbusya says

    Hadithi tamu sana jamani

Leave A Reply