The House of Favourite Newspapers

“Euthanasia”: Mauaji ya Kumpunguzia Mgonjwa Maumivu, Mateso!

liver-cancer_cambodian-patients2

WIKI zilizopita, aliyekuwa mmoja wa wapiganiaji  utawala wa wengi  Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu,  wa Kanisa la Anglikana,  akiadhimisha mwaka wa 85 wa kuzaliwa kwake, alisema anategemea kutoa maombi ya kufanyiwa ‘mauaji ya huruma’ kwa madaktari iwapo hali yake ikitokea kuzorota kadri umri unavyozidi kusonga mbele.

“Ninataka kuyamaliza maisha yangu kwa kifo cha kusaidiwa.  Watu wanaokabiliwa na kifo wana haki ya kuchagua jinsi ya kumwacha Mama Dunia kwa heshima,” aliandika katika gazeti moja akiisifia Canada na Jimbo la California (Marekani) ambako wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa yenye maumivu na mateso  makali huruhusiwa kifo cha heshima.

‘Mauaji ya huruma’ aliyokuwa akiyamaanisha Tutu ni yale yatolewayo kwa watu wanaougua magonjwa yenye maumivu na mateso makali na ambayo mwisho wake ni kifo.  Mauaji hayo kwa Kiingereza huitwa ‘Euthanasia’ (hutamkwa Yuthenazia).  Euthanasia ni neno lenye asili ya Kigiriki ambalo humaanisha ‘Kifo Kizuri”.

a

Vifo vya Euthanasia viko makundi makuu matatu: Euthanasia ya Hiari (yenye kibali cha mgonjwa na ndugu zake), Euthanasia Isiyo ya Hiari (inayofanyika kwa  kukosekana  kibali cha mgonjwa, hususan mtoto mdogo asiyeweza kusema au kujieleza) na Euthanasia ya Lazima (inayofanyika bila kibali cha mgonjwa au dhidi ya utashi wake).

Euthanasia ya Lazima — ni haramu duniani kote na huchukuliwa kama mauaji ya kukusudia.  Njia kuu za ‘mauaji’ hayo ni pamoja na kutompa tiba mgonjwa au kumdunga sindano ya sumu.   Hata hivyo, kuna migongano kuhusu Euthanasia duniani  ambako wapinzani hutetea maisha  ya mtu lazima yaheshimiwe hadi mwisho, wakati wanaounga mkono husema ni lazima mtu anayeteseka kwa ugonjwa aruhusiwe kufa kwa heshima.

Miongoni mwa nchi ambako Euthanasia ni halali ni pamoja na  Netherlands (Uholanzi), Colombia, Belgium, na Luxembourg.  Nchini Marekani, Euthanasia ni haramu, lakini kuna njia wanazoruhusiwa madaktari, katika majimbo kadhaa,  kuzitumia katika kumsaidia mgonjwa ‘kujiua’.

 

Comments are closed.