The House of Favourite Newspapers

Fahamu matatizo mazito ya kiafya kwa watoto wachanga

MTOTO mchanga mwenye afya hupumua kwa urahisi, bila msukumo. Anapaswa kunyonya kila baada ya saa mbili hadi 4 na kuamka peke yake bila kuamshwa anaposikia njaa au kujilowesha.

Ngozi yake inakuwa safi au inakuwa na wekundu mdogo kwa mbali au na upele mdogomdogo ambao hutoweka baada ya siku chache. Mtoto ambaye haonyeshi mambo hayo anaweza kuwa na matatizo na anahitaji msaada wa haraka.

MAAMBUKIZI

Maambukizi kwa mtoto mchanga ambaye amezaliwa siyo muda mrefu uliopita yanaweza kuwa hatari sana na huhitaji tiba kwa kutumia antibiotiki mara moja.

DALILI ZA HATARI

Kupumua harakaharaka: zaidi ya pumzi 60 kwa dakika wakati amelala au akiwa amepumzika.

Kupata hewa kwa shida: Kifua kuvuta ndani, mtoto kukoroma, pua kulazimika kutanuka na kufunguka wakati wa kulala au kupumzika.

Homa, zaidi ya nyuzi joto 37.5º sentigredi, au joto la mwili kushuka chini ya nyuzi joto 35.5º sentigredi.

Upele mkali ukiandamana na vipele vikubwa vingi au malengelenge (upele mdogo ni jambo la kawaida.)

Mtoto kuacha kunyonya.

Mtoto kuamka kwa nadra kutoka usingizini, au kuonekana kutokuitikia kwa njia yoyote ili.

Dalili zinazofanana na kifafa: kupoteza fahamu na kurusha viungo vya mwili.

Dalili yoyote kati ya hizo humaanisha kuwa mtoto anahitaji matibabu.

MATIBABU

Kama unadhani mtoto ana maambukizi ingawa siyo makali, mpeleke kwa daktari ambaye atampa ampisilini au amoksilini, lakini kwa maambukizi makali atachomwa sindano ya ampisilini na jentamaisini mara moja. Kiwango cha dawa kitategemea uzito na umri wa mtoto, daktari anajua.

Mtoto anapaswa kuanza kupata nafuu ndani ya siku mbili. Kama hatapata nafuu katika muda huo, dawa tofauti za antibiotiki zinahitajika kuponya maisha yake.

Kama mama alipatwa na homa wakati wa uchungu wa uzazi, daktari atakuwa mwangalifu zaidi kwa ajili ya dalili za hatari kwa mtoto.

Vilevile, mtoto ambaye aliyejisaidia kinyesi angali tumboni wakati mwingine anaweza kuvuta ndani kinyesi hiki wakati wakuzaliwa kupitia pumzi.

Hii inaweza kusababisha maambukizi kwenye mapafu katika siku za mwanzo. Hivyo, mtoto anatakiwa kutibiwa haraka mara dalili za maambukizi zinapojitokeza.

MTOTO KULIA

Baadhi ya watoto wachanga hulia sana kuliko wengine. Mtoto anayelia sana anaweza kuwa salama iwapo dalili zake nyingine za kiafya ni za kawaida.

Mama angalia iwapo anapumua vizuri anapokuwa halii. Hali ya kulia karibu muda wote, na kuzidi hasa usiku, wakati mwingine husababishwa na tumbo kusokota.

Hali hii kawaida hupungua baada ya miezi 3. Mama ambaye amejifungua anatakiwa apate muda wa kupumzika na kupewa kila msaada anaouhitaji. Kama mtoto atakuwa analia muda mrefu mchana na pia hanyonyi, ana homa, au ana matatizo katika kupumua, hii inaweza kuwa dalili ya maambukizi.

MTOTO KUTAPIKA

Watoto wachanga hucheua maziwa. Wakati mwingine yanakuwa mengi na kuweza kupita mdomoni au puani. Kucheua maziwa siyo tatizo kama mtoto atakuwa ananyonya mara kwa mara na kuongezeka uzito. Jaribu kumbeba wima baada ya kunyonya. Mtoto atakuwa anatapika iwapo atatumia nguvu-badala ya maziwa kuwa yanatoka yenyewe na kumwagika nje.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.