The House of Favourite Newspapers

Fahamu tatizo la shinikizo la damu!

SHINIKIZO la damu ni miongoni mwa matatizo yanayoathiri watu wengi. Nini maana ya shinikizo la damu?  Ni ile hali inayotokea pale msukumo wa damu katika mishipa yake unapokuwa juu kwa muda mrefu kuliko inavyotakiwa. Katika hali ya kawaida, msukumo wa damu uhitajika mwilini ili kusambaza chakula, hewa safi ya oksijeni na kutoa hewa chafu ya kabon’diokside.

Hata hivyo, inapotokea msukumo huu kuwa juu isivyo kawaida, huleta usumbufu na madhara ambayo kama yasipotibiwa, husababisha kifo kwa baadhi ya watu. Shinikizo la damu hupimwa kwa kutumia kifaa kinachoitwa sphygmomanometer.

Shinikizo la damu husababishwa na nini? Takriban asilimia 90 hadi 95 ya kesi za shinikizo la damu hazina visababishi vinavyojulikana. Hii ni aina ya kwanza ya shinikizo la damu ambayo kitaalam huitwa primary or essential hypertension.

Pamoja na kuwa sababu halisi zinazosababisha aina hii ya shinikizo la damu hazijulikani, kuna vitu kadhaa ambavyo vinahusishwa kwenye kusababisha mtu au watu kupata aina hii ya shinikizo la damu.

Vitu au mambo hayo ni pamoja na uvutaji wa sigara, unene (visceral obesity), unywaji wa pombe, upungufu wa madini ya potassium, upungufu wa Vitamin D, kurithi, umri mkubwa, chumvi na madini ya sodium kwa ujumla. Pia kuna ongezeko la kemikali kwenye figo (renin) na kushindwa kufanya kazi kwa kichocheo kiitwacho insulin.

Karibu asilimia 5 ya wagonjwa wanaopata tatizo hili la shinikizo la damu huwa na sababu zinazosababisha kupata aina hii ya shinikizo la damu.

Aina hii ya shinikizo la damu kwa lugha nyingine hujulikana kama secondary hypertension. Sababu hizi ni pamoja na hali ya kukosa hewa mtu awapo usingizini (sleep apnea), matatizo ya kimaumbile ya tangu kuzaliwa kwenye mshipa mkubwa wa damu (coarctation of aorta), saratani za figo (wilm’s tumor, renal cell carcinoma) na saratani ya tezi ya adrenal (pheochro-mocytoma).

Sababu nyingine ni ujauzito –wapo akina mama wajawazito ambao hupata shinikizo la damu na huwa hatarini kupata kifafa cha mimba (eclampsia) na magonjwa ya figo (renal artery stenosis, glomerulonephritis).

DALILI

Kundi kubwa la wagonjwa wa shinikizo la damu huwa hawaoneshi dalili zozote (asymptomatic). Hata hivyo, mgonjwa atakuwa na dalili (symptomatic). Dalili hizo zinaweza kuwa kujisikia mchovu, kuhisi maumivu ya kichwa, kuhisi mapigo ya moyo kwenda haraka (palpitations), kichefuchefu, kutapika, damu kutoka puani, kutoona vizuri (blurred vision), kusikia kelele masikioni na mara chache kuchanganyikiwa.

Ili daktari aweze kufikia majumuisho kuwa mgonjwa ana tatizo la shinikizo la damu, uhitaji kumpima mhusika angalau mara tatu kwa vipindi tofauti vya wiki mojamoja. Upimaji huu hufanywa kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia msukumo wa damu au sphygmomanometer.

MATIBABU

Lengo la matibabu ya shinikizo la damu ni kuzuia madhara yanayosababishwa na ugonjwa huu. Matibabu ya shinikizo la damu hutumia dawa mbalimbali kama daktari atakavyoona.

Ifahamike kuwa, matibabu ya shinikizo la damu la aina ya kwanza (primary hypertension) ni ya kudumu (life-long) wakati yale ya aina ya pili (secondary hypertension) yaweza kuwa ya kudumu au la kutegemea na kisababishi cha aina hii kimeshagundulika na kimeshatibiwa.

Kwa mfano, kama mgonjwa ana aina hii ya shinikizo la damu inayotokana na mshipa wa damu unaopeleka damu safi kwenye figo kuziba (renal artery stenosis) amefanyiwa operesheni ya kuzibua mshipa huu wa damu, uwezekano wa kuacha kutumia dawa ni mkubwa kwa vile chanzo cha shinikizo la damu tayari kimeshatibiwa.

Madhara yanayoweza kuletwa na shinikizo la damu ni mengi kama vile moyo kushindwa kufanya kazi (congestive heart failure) Madhara katika mshipa mkubwa wa damu (aorta) ambapo ukuta wa ndani huchanika na damu hukusanyika katika ukuta wa mshipa huo (aortic dissection), kushindwa kuona, kupata athari katika ubongo nk.

Njia za kuzuia au kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu ni pamoja na kula chakula cha afya kisicho na mafuta yenye lehemu (cholesterol) nyingi na chenye madini ya potassium ambacho kitaalam hujulikana kama dash diet (dietary approaches to stop hypertension).

Pia kufanya mazoezi mara kwa mara, angalau nusu saa kila siku. Wavuta sigara, inashauriwa kuacha kabisa kuvuta sigara, wanywaji pombe kupunguza au kuacha unywaji wa pombe. Pia kupunguza utumiaji wa chumvi hasa ya kuongeza mezani (usitumie zaidi ya gramu 1.5) na kujitahidi kuondoa msongo wa mawazo. Wale wanene wajitahidi kupunguza uzito uliopitiliza na hasa wenye vitambi.

Comments are closed.