The House of Favourite Newspapers

Faida za kula karanga ni zaidi ya unavyojua!

SIKU hizi biashara kubwa ya vijana na akina mama ni karanga za kukaanga au mbichi au za kuchemshwa, lakini wengine hawajui kwamba karanga ni muhimu sana katika afya ya mwili wa binadamu. Kiukweli karanga siyo chakula cha kupuuzwa iwapo utajua faida zake kama nitakavyokujuza leo katika safu hii. Kwanza kabisa karanga husaidia katika kutibu magonjwa ya moyo. Kama ilivyokuwa kwa korosho, karanga nazo ni chanzo kizuri cha mafuta mazuri aina ya monounsaturated fats ambayo yanatiliwa mkazo kutumiwa kwa afya ya moyo. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, watu wanaokula karanga mara kwa mara hupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kitaalamu uitwao cardiovascular heart disease.

Aidha, katika taarifa iliyochapishwa kwenye jarida moja la Uingereza la ‘Journal of Nutrition’ ambako kuna matokeo ya taarifa nne za utafiti, imeonesha pia watu wanaotumia karanga mara kwa mara, angalau mara nne kwa wiki, hujipa kinga nyingine dhidi ya ugonjwa wa moyo uitwao coronary heart disease kwa zaidi ya asilimia 37.

Mbali ya kuwa na mafuta mazuri yanayotoa kinga kwenye moyo, karanga pia, ukizitafuna mlaji anapata kiwango kikubwa cha virutubisho vinavyotoa kinga ya mwili kuliko hata kile kinachopatikana kwenye tunda la epo na karoti.

Ili kupata kinga hiyo dhidi ya aina hizo mbili za ugonjwa wa moyo, ambao unatesa watu wengi duniani na kugharimu pesa nyingi kwa matibabu, unashauriwa kula karanga pamoja na bidhaa zake kama vile peanut butter, angalau kijiko kimoja cha chakula, mara nne kwa wiki.

KINGA YA KIHARUSI

Ugonjwa mwingine hatari unaowasumbua watu wengi hivi sasa ni kiharusi yaani stroke. Ugonjwa huu hatari unaweza kujikinga nao kwa kuwa na mazoea ya kula karanga tu, hii ni faida nyingine kubwa ya kula mbegu hizi. Utafiti umeonesha kuwa karanga ina kirutubisho aina ya Resveratrol ambacho hupatikana pia kwenye zabibu na mvinyo mwekundu (red wine).

Utafiti uliofanywa maabara na kuchapishwa kwenye Jarida la Kilimo na Kemia ya Chakula (Journal of Agricultural Food Chemistry), umeonesha kuwa kirutubisho hicho cha karanga huimarisha utembeaji wa damu kwenye mishipainayokwenda kwenye ubongo kwa kiasi cha asilimia 30.

KINGA KWA MAGONJWA YA SARATANI

Faida nyingine inayoweza kupatikana kwenye mwili kutokana na ulaji wa karanga, ni kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya tumbo  Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, unaonesha kuwa virutubisho vya folic acid, phytosterols, phytic acid’ na resveratrol’ vinavyopatikana kwenye karanga, huweza kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya tumbo.

Jarida la Kilimo na Kemia ya Chakula katika utafiti wao umeonesha kuwa ulaji wa karanga hata mara mbili tu kwa wiki, una uwezo wa kupunguza uwezekano wa kupatwa na saratani ya tumbo kwa asilimia 58 kwa wanawake na asilimia 27 kwa wanaume.

Hivyo kula karanga sio tu kwamba unafanya watu wafurahie mbegu hiyo, bali kiafya kuna faida zaidi. Kwa maelezo hayo hapo juu kuhusu faida za karanga mwilini bila shaka chakula hiki kinapaswa kupewa kipaumbele katika orodha ya vyakula tunavyokula kila siku katika familia zetu.

Comments are closed.