The House of Favourite Newspapers

FANYA MAMBO HAYA KUMFURAHISHA MUWAPO FARAGHA- 2

WIKI iliyopita tulianza kujadiliana kuhusu mambo ambayo ukiyafanya kwa ukamilifu muwapo faragha, utamfurahisha mwenzi wako na kumfanya kila siku awe anatamani kuwa na wewe. Tulizungumzia kwa upana kuhusu namna ya kumuandaa mwenzi wako kihisia na leo, tunaendelea na mambo mengine muhimu.

KAULI ZAKO

Watu wengi huwa wanakosea kuhusu kauli wanazozitoa wanapokuwa faragha na wenzi wao. Unaweza kuzungumza jambo halafu bila mwenyewe kujua ukajikuta umemtoa mchezoni mwenzi wako.

Mambo hayatakiwi kuwa mengi, hutakiwi kuwa mzungumzaji sana bali pangilia maneno yako vizuri na zungumza kwa sauti ambayo kweli inaonesha unafurahia kinachoendelea kati yenu.

Msifie kwa lugha laini, mweleze jinsi unavyofurahia hicho mnachokifanya, mueleze jinsi alivyobarikiwa mambo mengi mazuri na mhakikishi kwamba unampenda yeye tu na hakuna kinachoweza kuwatenganisha.

Wataalamu wa masuala ya kimapenzi, wanaeleza kwamba kauli nzuri na tamu muwapo katika tendo, humsaidia mwenzi wako kufika haraka mwisho wa safari yake, kwa hisia za hali ya juu kabisa! Kwa hiyo kuwa makini, wakati mwingine kauli zako zisindikizwe na miguno ya hapa na pale ambayo itazidi kunogesha safari yenu.

ONESHA KUZIJALI HISIA ZAKE

Huu ni wakati ambao hisia za kila mmoja zinapanda na kuwa katika kiwango cha juu kabisa. Unapaswa kuwa makini kuhakikisha unaziheshimu hisia zake kwa kufanya kile anachokitaka na kuachana na kile kinachoonesha kutomfurahisha.

Wanaume wengi huwa wanakosea kwa kutaka wao ndiyowafanye wanachokitaka na wakishakidhi haja za miili yao, wanakuwa hawana tena muda wa kusikiliza hisia za wenzi wao. Hili ni kosa kubwa. Safari nzuri ni ile ambayo kila mmoja anafika mwisho, bila kujali nani ambaye atatangulia.

Wanaume wengi huwa wanakuwa na ‘kaudhaifu’ ka kuwahi kufika kabla ya wenzi wao na kwa bahati mbaya, wengi huwa hawaelewi inapotokea hali hiyo, wanatakiwa kufanya nini. Ndiyo maana nilikusisitiza kwamba unatakiwa kuyasaka maarifa kwa nguvu zako zote kwa sababu yapo!

MSHUKURU KWA DHATI

Baada ya kumaliza kile kilichowakutanisha na kila mmoja akawa amefurahia na kuridhika kwa asilimia mia moja, unatakiwa kumshukuru mwenzi wako na hii inawahusu wote.

Hakuna mahali palipoandikwa kwamba ni lazima mwanaume ndiyo amshukuru mwanamke au mwanamke ndiyo amshukuru mwanaume, hili ni suala la pande mbili, mwanaume amshukuru mwanamke na mwanamke amshukuru mwanaume!

Mkijenga utaratibu huu, mtajikuta kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, mnazidi kulifurahia tendo na kila mmoja anajitahidi kadiri ya uwezo wake kumfurahisha mwenzake.

USAFI NDIYO KILA KITU

Hapa kwenye namna ya kuhitimisha kuna mambo ya muhimu sana ambayo unatakiwa kuyafanya! Wazee wa zamani wana nahau yao wanayopenda sana kuitumia kwamba ‘ukimaliza kusonga ugali lazima uoshe mwiko’ na ‘ukimaliza kula lazima uoshe vyombo!’

Hii ni hatua muhimu sana kwa wote wawili na kwa wanaume, inatajwa kwamba kuoga maji ya baridi au ya uvuguvugu baada ya kumaliza shughuli, inakusaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha nguvu mpya zitakazokufanya uendelee na ngwe ya pili au ya tatu kwa urahisi zaidi.

Kwa hiyo unatakiwa kuwa makini, usafi wa mwili na uwanja wa tukio ni muhimu sana baada ya kumalizika kwa tukio na hiyo itawasaidia wote wawili kupumzika vizuri lakini itaongeza msisimko kati yenu.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba ili safari yenu iwe nzuri, lazima kila mmoja wenu azingatie usafi wa mwili na mavazi hata kabla ya kukutana! Hakikisha umeoga vizuri, umepiga mswaki, kama una manukato basi jipulizie na hakikisha hauwi kero kwa mwenzi wako muwapo faragha.

Makala:Hashim Aziz  +255 719401968

Comments are closed.