The House of Favourite Newspapers

Frederick Sumaye Atajwa Mahakamani – Video

0

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye,  ametajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wa usikilizwaji wa kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Sumaye ambaye ametangaza leo kung’atuka katika masuala ya kisiasa ametajwa na shahidi wa sita wa upande wa utetezi, Dkt. Vincent Mashinji.

 

Mashinji ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema ametoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili Peter Kibatala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

 

Dkt. Mashinji amedai kuwa yeye hakuwa sehemu ya itifaki ya mkutano wa Chadema uliofanyika viwanja vya Buibui, jijini Dar es Salaam, Februari 16, 2018.

 

Amedai kuwa alikwenda kwenye mkutano huo akitokea ofisini na alipofika alimkuta  Fredrick Sumaye akiwa anahutubia.

 

Amedai kuwa Sumaye alimkaribisha mkutanoni ili aweze kusalimia ndipo alipotumia muda mfupi kuzungumza na wananchi waliofika katika mkutano huo, kisha akarudi ofisini kwake kwa kuwa kulikuwa na kazi nyingine ambazo alikuwa anapaswa azishughukilie.

 

Baada ya kutoa maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alimuonyesha Dkt. Mashinji barua iliyoonyesha ilitoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, kwenda kwake ikitoa ufafanuzi wa sheria na kanuni za uchaguzi na kumtaka kuithibitishia mahakama kwamba anaitambua na aiombe mahakama iipokee kama sehemu ya kielelezo.

 

Baada ya maelezo hayo, Dkt. Mashinji akaiomba mahakama iipokee barua hiyo kama kielelezo ambapo upande wa mashtaka ulikubali na mahakama ikaipokea kama kielelezo.

 

Pia Kibatala akamwambia kuna barua ambazo zinatoka kwa Katibu wa Chadema  Wilaya kwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ambapo alimtaka Dkt.Mashinji azitambue na kisha aiombe mahakama izipokee kama ushahidi.

 

Kabla ya Mahakama kuzihakiki na kupokea barua hiyo, uupande wa mashtaka kupitia Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon, wameiomba mahakama kutopokea barua hizo kwa sababu hakukuwa na sehemu yoyote inayoonyesha nakala kwenda kwa Katibu Mkuu wa chama ambaye ni Dkt. Mashinji.

 

Pia hakukuwa na nyaraka yotote inayoonyesha makabidhiano, hivyo ni wazi shahidi ameshindwa kutoa maelezo ya wazi ni namna gani nyaraka zimefika.

 

Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, amedai kuwa hata kama Dkt.Mashinji ni mwekaji wa nyaraka hizo bado haitoshi mahakama kupokea vielelezo hivyo, ameshindwa kuiaminisha mahakama.

 

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Simba ameahidi kutoa maamuzi kuhusu barua hizo kupokelewa ama kutopokelewa kesho Desemba 5, 2019.

 

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa chama hicho,Freeman Mbowe; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

 

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, yakiwemo ya kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.

BAADA YA SUMAYE KUSEPA, KIGOGO CHADEMA AMTAJA MAHAKAMANI

Leave A Reply