The House of Favourite Newspapers

HATARI YA UTI WA MGONGO (Meningitis)

UGONJWA wa mgongo huathiri sehemu inayofunika ubongo na uti wa mgongo, yaani utandu. Ubongo unafunikwa na sehemu au tandu tatu nyembamba za seli ili kuitenganisha na fuvu la kichwa. Tandu hizi zinaweza kuathirika na kusababisha hali inayojulikana kama uvimbe wa utandu wa ubongo na uti wa mgongo.

Kwa sababu tandu zilizoathirika ziko karibu na ubongo, uvimbe wa utandu wa ubongo huwa na athari kwenye ubongo na kuathiri kuona, kusikia, kukumbuka, uwezo wa kutembea, uwezo wa kuzungumza na uwezo wa kukumbuka.

NI NINI HUSABABISHA UGONJWA HUU?

Aghalabu husababishwa na bacteria, lakini pia huweza kusababishwa na viumbe hai kama virusi na fungas. Bakteria hupumuliwa ndani na hupenya kupitia damu na kuathiri ubongo na uti wa mgongo. Huambukiza haraka sana/ husambaa haraka sana katika maeneo ambapo kuna msongamano mkubwa na hii inaweza kugeuka kuwa mlipuko wa magonjwa. Ugonjwa huu hutajwa kuwa ni wa mlipuko kutokana na ukweli kuwa huambukiza haraka na huathiri watu wengi kwa wakati mfupi sana.

Mara nyingi hulipuka katika makazi ya watu wengi kama vile kwenye kambi za wanajeshi, wakimbizi, katika shule za bweni na kadhalika. Kutokana na hilo, kila mtu yupo katika hali ya hatari kuambukizwa na kuugua ugonjwa huu. Huambukiza kirahisi na haraka kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine.

Ugonjwa wa uti wa ubongo huathiri sana watoto walio chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wakongwe. Wale walio na kinga duni kama vile wanaougua ugonjwa wa sukari, saratani, ukimwi, pia wapo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu wa utandu wa ubongo na uti wa mgongo.

DALILI ZA UGONJWA

Dalili za ugonjwa huu ni kuwa mgonjwa huwa na joto la hali ya juu, tatizo la kuona au kuepuka mwangaza, kutapika, kuumwa kichwa, kukakamaa na kupinda shingo huwa ni dalili ya mwisho. Watoto walio chini ya umri wa miaka 2 wanaweza kuwa na joto tu pamoja na kulia. Ugonjwa huu unaweza kuua kati ya saa au siku chache. Kinga na tiba Uzuiaji mzuri ni kwa njia ya chanjo. Lazima watoto wote wachanjwe ili kupunguza hatari ya kuugua ugonjwa wa utandu wa ubongo na uti wa mgongo.

Kwa sababu ugonjwa huu huambukiza kutokana na kukaribiana kwa watu, ni muhimu kuzingatia usafi na kuwa mbali na waathirika wa ugonjwa wakati wa kuwatazama, kuwajulia hali ama kuwaliwaza. Msongamano wa watu ndicho chanzo muhimu cha kuenea na kusambaa kwa ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine, hivyo watu wasikae kwa kusongamana.

Kwa kuwa ugonjwa husababishwa na bacteria na kuna dawa za kupambana na magonjwa yasababishwayo na hewa katika hospitali zote, ambazo zinaweza kutiba ugonjwa wa uti wa mgongo. Dawa hizi hutumiwa kupitia sindano mara nyingi kwa siku na lazima sindano hizi ziendelee kwa kipindi cha wiki/ majuma mawili hadi matatu.

Tahadhari, ikiwa mgonjwa atacheleweshwa dawa hizo, haziwezi kumsaidia kutibu mgonjwa huo. Kwa hivyo ni muhimu kwenda hospitalini kwa wakati unaofaa kila dalili zinapoonekana. Kila ambaye ataona dalili hizi anashauriwa kuwahi hospitali iliyo karibu haraka iwezekanavyo. Hii ni kwa sababu ugonjwa huu huambukizwa kwa kasi sana.

Wagonjwa wote wa uti wa mgongo au utandu wa ubongo lazima walazwe hospitalini kwa sababu huzingatiwa kuwa dharura ya kimatibabu. Haushauriwi kumtunzia mgonjwa wa uti wa mgongo au utandu wa ubongo nyumbani. Hii ni dharura ya kimatibabu inayostahili kutatuliwa hospitalini kati ya wiki 2-3.

Wagonjwa wote sharti chakula chao kiwe chepesi chenye virutubishi, wape kiasi kidogo kila baada ya saa mbili. Hii ni kwa sababu hamu yao ya kula chakula hupotea. Watie moyo wagonjwa ambao wana madhara kutokana na ugonjwa huu. Kwa ushauri zaidi wasiliana nami kwa simu hiyo hapo juu.

Comments are closed.