The House of Favourite Newspapers

Heche Azungumzia Migogoro ya Ardhi Tarime

0
MBUNGE wa Jimbo la Tarime (Chadema) John Heche, (kulia) akizungumza na wanahabari.

MBUNGE wa Jimbo la Tarime (Chadema) John Heche, amezungumzia hofu iliyoibuka miongoni mwa wananchi wa Tarime baada ya ardhi yao kuporwa na kugawiwa kwa anayeitwa mwekezaji kinyume na utaratibu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, amesema kuwa kumekuwepo na sintofahamu na hofu kubwa ya kupoteza ardhi kwa wakazi wa eneo la bonde la mto Mara katika vijiji vilivyoko kata za Matongo ,Kemambo, Kibasuka na Manga.

Amesema kuwa hofu hiyo ya kupoteza ardhi imesababishwa na kiongozi mmoja wa serikali na baadhi ya watu waliojificha nyuma ya mtu anayedaiwa kuwa mwekezaji ambao wanataka kutumia mabavu, vitisho na kukandamiza watu ili kujipatia eneo la kuweka mradi wa ujenzi wa kiwanda cha miwa.

Amesisitiza kuwa makubaliano yaliyofanyika kupitia kiongozi huyo wa serikali yamemshitua karibu kila mtu kwa kuwa yameonekana kupitia vyombo vya habari pasipo wawakilishi wa wananchi kwa maana ya mbunge, madiwani na wananchi wenyewe.

Ameongeza kuwa tayari suala hilo limeibua mgogoro wa chinichini kwa wakazi wa jimbo lake Tarime na kuwakumbusha watu wa Tarime historia ya athari za uwekezaji unaoletwa kwa njia zisizozingatia taratibu na maslahi ya wananchi.

Amefafanua kuwa suala la uwekezaji ni jambo jema  na kwamba halipingi bali ni vyema viongozi wilayani humo  kushirikisha wananchi katika ngazi zote husika kuhusu mikataba ya uwekezaji katika ardhi ili kuepusha migogoro.

Denis Mtima/GPL.

Leave A Reply