The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi 56

1

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa. Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Baada ya kuwa DCP, Dickson anakutana na msichana aitwaye Pamela, anatokea kuvutiwa naye, anafanya naye mapenzi kwa kumnunua Kinondoni. Kupitia changudoa huyo aliyetoka Arusha, anajikuta akianza kuwaua wanawake wengi jijini Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Pamela alikosa amani, pale alipokaa, muda wote mapigo ya moyo yalikuwa yakimdunda kwa nguvu, usiku wa siku hiyo ulikuwa na joto jingi lililosababisha kuwa na mbu wengi huku msongamano wa machangudoa ndani ya sero aliyokuwepo kuwa mkubwa.

Moyoni mwake alijuta, hakujua ni nini kingefuata baada ya hapo, hakujua kama angepelekwa mahakamani na wenzake kisha kufungwa gerezani, alipolifikiria hilo, akashindwa kuvumilia, akajikuta akitokwa na machozi.

Usiku mzima hakulala, alikuwa mtu mwenye majonzi makubwa. Ilipofika saa moja asubuhi, machangudoa hao wakaambiwa wajiandae kwani asubuhi ya siku hiyohiyo wangepelekwa mahakamani na hivyo kushtakiwa.

“Mungu nisaidie….” alijisemea moyoni.
Saa mbili asubuhi, polisi mmoja akafungua mlango wa sero ile na kumtaka msichana aliyeitwa Pamela atoke, kwa harakaharaka akatoka na kwenda kaunta ambapo aliambiwa achukue vitu vyake na kuondoka mahali hapo.

“Kuna nini?” aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Wewe nenda tu, hiyo ni amri.”
“Kutoka wapi?”

Hakukuwa na polisi aliyemjibu, kila mmoja akajifanya kuwa bize, Pamela hakutaka kuchelewa, hapohapo akachukua kila kilicho chake na kuondoka, tena kwa kasi pasipo kuangalia nyuma.

Pamela alipofutika kabisa kituoni pale, Kamanda Dickson akatokea, kilichofuata ni kuingia ndani ya sero ile na kuanza kumtafuta mtuhumiwa wake, alimkariri kwa kuwa na chunusi nyingi usoni na miguu iliyokuwa na matege, kama ilivyokuwa katika vituo vingine, napo humo hakufanikiwa kumuona.

Kamanda Dickson akaagiza machangudoa wote watolewe ila waonywe kutokurudia tena kwani kazi aliyokuwa ameifanya haikuwa imekamilika, hivyo maaskari wakafanya kama walivyotakiwa.

Baada ya kukaa kwa kipindi cha siku tatu ndipo alipokuwa na wazo moja kwamba ili kumpata msichana huyo, ilikuwa ni lazima atumie simu yake iliyoibwa siku hiyo hivyo moja kwa moja kuelekea katika ofisi za mtandao wa simu za mkononi wa Wintel.
Alipofika huko, akatoa maelezo yake na kwa sababu alikuwa mtu mkubwa, wafanyakazi wakaanza kuitafuta simu yake kupitia kompyuta zao.

“Hapa inaonesha kwamba simu yako yenye kodi namba YT7853 ilizimwa kwa mara ya mwisho juzi, laini iliyoingizwa ilikuwa ni yenye namba 0462-227 768, laini hiyo ilidumu ndani ya simu hiyo kwa saa nne kisha kutolewa na kuingizwa laini nyingine yenye namba 0468-256 730,” alisema mfanyakazi aliyekuwa akimsaidia.
“Nataka niwapate wote wawili, itawezekana kufanyika leo?” aliuliza Kamanda Dickson.
“Bila shaka.”

Ilikuwa ni amri ambayo wafanyakazi wa kampuni hiyo wakafanya kama walivyotakiwa. Kitu cha kwanza ilikuwa ni kuwafungia huduma zao za kifedha ili wahitaji kufunguliwa na kama wangehitaji kufunguliwa ilikuwa ni lazima waende ofisini hapo na kukamatwa, kama hiyo ingeshindikana basi ilikuwa ni lazima watraki simu zao, wajue walipo na waanze kuzifuatilia.

Zoezi la kuzifunga akaunti zao za fedha likafanyika. Baada ya kuzifunga, wala hazikupita dakika nyingi, simu kutoka kwa watu hao zikaingia, zilikuwa simu za malalamiko kuhusu akaunti zao kufungiwa, hivyo walihitajika ofisini kwa ajili ya kufunguliwa.

“Ila mnazingua sana, siku hizi mmekuwa magumashi sana, kila siku mtandao unasumbua tu,” alisikika mwanaume kwenye simu, aliongea kwa jazba.
“Tunaomba utusamehe, tunajitahidi kuboresha huduma kila siku, unaweza kufika kwenye ofisi zetu hapa Mwenge kwa ajili ya kufunguliwa akaunti yako,” alisema mfanyakazi huyo kwa sauti ya upole yenye kumhamasisha mtu kufanya kile alichotakiwa kufanya.

Kamanda Dickson alikuwa pembeni, muda wote uso wake ulikuwa wenye hasira, kila alipokuwa akimwangalia dada yule aliyekuwa akimsaidia kuwasiliana na watu ambao aliamini kwamba walifahamu simu yake ilipokuwa, alionekana kumkasirikia.

Baada ya saa mbili, mwanaume mmoja akafika ofisini hapo, alipojitambulisha na kusema kilichomleta, akaambiwa asubiri kitini. Dada yule akaingia ndani, alipotoka, akatoka na wanaume watatu waliovalia mavazi ya kiraia na kumuweka chini ya ulinzi.
“Upo chini ya ulinzi,” alisema polisi mmoja, Kamanda Dickson alikuwa pembeni akiangalia mchezo mzima, muda wote alikuwa na hasira.

“Nimefanya nini jamani?”
“Utakwenda kujua kituoni.”
“Ila niambieni kwani ni haki yangu kujua kinachonifanya niwe chini ya ulinzi,” alisema jamaa huyo.

“Kosa ni kutumia simu ya wizi.”
“Simu ya wizi. Hapana! Ipi?”
“Hiyo unayoitumia.”
“Afande… mimi mwenyewe nimeuziwa tu, sikuambiwa kama ya wizi,” alijitetea jamaa yule.

“Uliuziwa na nani?”
“Hadija!”
“Sawa. Twende, naye atakufuata hukohuko kituoni,” alisema polisi mmoja, wakamchukua, wakamfunga pingu na kuondoka naye huku Kamanda Dickson akisimama na kuwafuata. Muda wote alionekana kuwa na hasira, aliyemtaka zaidi ni huyo Hadija.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

1 Comment
  1. ahady kidehele says

    mlolongo wa kusoma hadithi ni mkubwa mnoo

Leave A Reply