The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi – 69

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa amehamishia fedha zake zote katika akaunti yake ya siri, hakuna aliyejua fedha zimehamishwaje kwani aliyefanya kazi hiyo ni mtaalam sana katika mambo ya kompyuta, anachokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Mwanza.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

 

Mzee yule hakutaka kuondoka, bado akili yake ilimwambia kwamba mtu yule aliyemsaidia ni kweli alifiwa na hivyo kuondoka mahali hapo na kumuacha na wakati alikuwa na tatizo, halikuwa jambo la busara.

Aliambiwa kwamba kama zingepita dakika kumi na kuona kimya, basi aondoke zake lakini hakufanya hivyo, alikaa mpaka dakika arobaini, Dickson hakutokea hali iliyomfanya ahisi kulikuwa na tatizo.

“Mmh! Isije ikawa amepata tatizo!” alijisemea.

Alichokifanya ni kuvuta subira. Sekunde ziliendelea kwenda mbele, dakika zikakatika mpaka kutimia saa moja, bado Dickson hakutokea. Hakutaka kusubiri zaidi, kama kujitoa, alijitoa sana, alichokifanya ni kuwasha gari lake na kuanza kuondoka huku moyo wake ukiwa na huruma nyingi juu ya Dickson.

“Atanisamehe tu, nimesubiri sana,” alijisemea huku akipiga gia na safari yake kuendelea.

Safari iliendelea, mzee yule hakujua kama ndani ya gari lake kulikuwa na maiti ya polisi, hakuwa na wasiwasi kabisa, kitu alichofikiria ni kufika mkoani Dodoma salama na kufanya mambo yake.

Baada ya dakika kadhaa, akawa anaingia maeneo ya Chalinze, mbele yake aliona magari mengi yakiwa yamepaki pembeni huku mbele kabisa kukiwa na magari ya polisi waliokuwa wakifanya msako wa kumtafuta Dickson ambaye mpaka wakati huo hawakujua alikuwa wapi, ila pamoja na hayo, walijua kwamba inawezekana angekimbilia nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Alichokifanya mzee yule naye ni kupanga foleni huku polisi wakiendelea na kazi yao kama kawaida. Foleni ilisogea na baada ya dakika thelathini, gari lake likawa mbele kabisa.

“Naomba uteremke mzee,” alisema polisi mmoja huku akimmulika kwa tochi usoni, mzee akateremka.

“Unakwenda wapi?” aliuliza polisi mmoja.

“Dodoma…”

“Kufanya nini?”

“Napeleka mzigo mkuu!”

“Sawa! Huogopi kutembea usiku sana?”

“Hapana! Nimeshazoea, namshukuru Mungu kwa miaka ishirini niliyofanya kazi hii, sijawahi kukutwa na balaa,” alijibu mzee huyo huku akionesha tabasamu pana.

“Upo na nani ndani ya gari?”

“Peke yangu!”

“Una uhakika?”

“Asilimia mia moja!”

“Basi sawa, naomba tufanye upekuzi kidogo, kuna mtu tunamtafuta,” alisema polisi huyo.

“Sawa! Hakuna tatizo.”

Hakuwa na wasiwasi hata kidogo, alikuwa na uhakika kwamba ndani ya gari hakukuwa na mtu yeyote yule zaidi yake, hakujua kuhusu maiti ile ya polisi iliyokuwemo na hata yule mtu aliyempa lifti alionekana kuwa mtu mzuri kitu ambacho hakikuwa sahihi kabisa.

Polisi mmoja mwenye tochi akaanza kuimulika mizigo ile. Zilikuwa mbao nyingi ambapo polisi hao wala hawakuwa na wasiwasi kwani kama kungekuwa na mtu aliyejificha, asingeweza kukaa kwenye mbao.

Walipoona kwamba hakukuwa na mtu yeyote katika mbao zile ndipo polisi mmoja akaufungua mlango na kuingia ndani. Muda wote mzee yule alikuwa akiwaangalia polisi wale, hakuwa na hofu hata kidogo ndiyo kwanza alisogea pembeni, akatoa sigara yake na kuanza kuvuta taratibu.

Ghafla, yule polisi aliyeingia ndani ya gari akatoka, alionekana kubadilika, alipofika chini tu, akatoa bunduki yake na kumuweka yule mzee chini ya ulinzi. Polisi wengine hawakujua kitu gani kilitokea, ila nao wakatoa bunduki zao na kumuweka chini ya ulinzi.

“Upo chini ya ulinzi…” alisema polisi yule.

“Chini ya ulinzi? Nimefanya nini?”

“Kwa mauaji!”

“Mauaji ya nani tena jamani?” aliuliza mzee yule huku akionekana kupigwa na mshangao.

Hata kabla hajapewa jibu, akaamrishwa alale chini na kuweka mikono yake kichwani, hakuwa mbishi, akafanya hivyo ndipo polisi yule alipoanza kuwaambia wenzake juu ya kile alichokiona ndani ya gari.

“Hapana! Sijamuua yeyote yule,” alisema mzee yule wakati maiti ya polisi yule ikitolewa ndani ya gari.

“Nyie wauaji huwa hamsemi ukweli, utakwenda selo sasa hivi,” alisema polisi mwingine huku akionekana kuwa na hasira.

Pingu ikatolewa na hapohapo akafungwa. Muda wote mzee huyo alikuwa akijitetea kwamba hakuwa amemuua mtu yeyote yule na hakujua maiti ile ilifikaje ndani ya gari lake.

Huo haukuwa muda wa kumsikiliza tena, walijua kwamba kwa jinsi tukio hilo lilivyotokea, angeweza kusema neno lolote ili kujitetea, walichokifanya ni kumpakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka naye huku polisi wengine wakibaki mahali pale kuendelea na msako.

“Sijamuua mtu yeyote jamani, haki ya Mungu sijamuua mtu yeyote yule,” alijitetea mzee huyo huku machozi yakimtoka.

“Utasema ukweli tu.”

Baada ya dakika kadhaa, wakafika katika kituo cha polisi ambapo mzee huyo akaanza kuhojiwa maswali kadhaa. Akatoa maelezo yake juu ya safari yake ilipoanza mpaka pale alipofika Chalinze ambapo alikamatwa.

“Unasema ulimpakiza mtu?”

“Ndiyo!”

“Unasema alikuwa na kofia kama ya Marlboro?”

“Ndiyo! Alishuka Mlandizi, nilishangaa kuona anaelekea porini, sikuuliza sana, sikujali, baadaye nikaondoka,” alisema mzee huyo.

“Na ulimzungumzia polisi, ulisema alivyoingia garini, hukumuona akitoka na ulipomuuliza, alisema alitokea upande wa pili?”

“Ndiyo!”

“Huyo atakuwa Dickson…. atakuwa Dickson huyo tu,” alisema mkuu wa kituo.

Hawakutaka kuendelea kubaki kituoni hapo, tayari walikuwa na uhakika kwamba mtu huyo alikuwa ni Dickson kwani hata maelezo ya mzee huyo yalionesha kwamba muuaji huyo alikuwa yeye. Walichokifanya ni kuingia ndani ya gari na mzee huyo, wakawachukua mbwa wao, bunduki zao na kuanza kuelekea kule aliposhukia Dickson, yaani piga ua hata kama angekuwa amekwenda wapi, ilikuwa ni lazima atafutwe na kukamatwa usiku huohuo.

“Tumefika…alielekea huku,” alisema mzee yule mara baada ya kufika eneo husika, wote wakateremka, bunduki mikononi na kuanza kuelekea kule alipoelekea Dickson, walikuwa na uhakika kwamba hakuwa amefika mbali.

Umbali kama hatua ishirini, wakaona mbwa wao wakibweka sana na kutaka kusonga mbele, hapo walikuwa na uhakika kwamba hawakuwa mbali na mtu huyo, hivyo wakaongeza kasi kwani kadiri sekunde zilivyokatika, mbwa walizidi kubweka.

Dickson alisonga mbele, hakutaka kusimama, hakutaka kurudi alipotoka, alitaka kufanya kila liwezekanalo mwisho wa siku afike Mwanza. Alitembea kwa mwendo wa kasi lakini baada ya umbali fulani, akahisi kuchoka hivyo kukaa chini ya mti na kupumzika.

Hapo ndipo kumbukumbu za maisha yake ya nyuma zilipomjia kichwani, alikumbuka mambo mengi mpaka kupitiwa na usingizi. Baada ya saa moja, akashtuka, kwa mbali akaanza kusikia sauti za mbwa wakibweka, hiyo ilikuwa saa nane usiku.

Hakutaka kuwa na wasiwasi, alichokifanya kwa sababu ya kuchoka sana, akajigeuza upande wa pili na kuanza kuuvuta usingizi, akili yake ilimwambia kwamba mbwa hao walikuwa ni wa wawindaji waliokuwa wakiwinda kenge, hivyo hakutaka kujali.

Usingizi ukaanza kumjia tena pasipo kugundua kwamba mbwa wale walikuwa ni wa polisi waliokuwa wakimsaka kufuatia mauaji aliyoyafanya.

Je nini kitaendelea? Au Dickson atakamatwa? Ungana nami wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply