MFULULIZO wa mauaji yanayotokea kila siku nchini, mengine yakiwa ya kutisha mno, yamenifanya nimkumbuke aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya awamu ya pili, Augustine Mrema, aliyejipatia umaarufu mkubwa enzi hizo, kutokana na ufuatiliaji wake wa mambo.
Alifanya mambo yaliyoshangaza wengi, vigogo wabadhirifu wakimchukia huku akipendwa na wanyonge. Alikuwa mtu wa kutoa maagizo na kufuatilia kiasi ambacho watu walijenga naye imani kubwa, wakiamini ndiye mkombozi wao waliyemsubiri kwa miaka mingi.
Rais Ali Hassan Mwinyi alimuenzi kwa kazi yake kubwa, akampatia nafasi ambayo kikatiba haikuwepo, ya unaibu waziri mkuu. Kama binadamu, alifanya pia makosa.
Katika mengi makubwa aliyoyafanya, yaliyokuwa na faida kwa wananchi wa chini, ni uimarishaji wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Kwanza alianzisha vituo vidogo vya polisi vilivyotapakaa nchi nzima (police post) ili kuwafanya watu kupata huduma za kiusalama mapema, tofauti na wakati ule ambapo kituo cha polisi kilikuwa kimoja tu huenda mji mzima.
Pili, alilazimisha watu kushiriki ulinzi shirikishi, maarufu enzi zile kama sungusungu. Ilikuwa ni lazima, bila kujali cheo wala hali ya mtu kifedha, watu wote kulinda usiku kwa zamu katika maeneo yao kwa mujibu wa makubaliano.
Na akasimamia utekelezaji wa suala hilo, akiagiza mwenyekiti wa mtaa na balozi wa nyumba kumi, kuwa watu wa kwanza kukamatwa na polisi endapo tukio la ujambazi litafanyika katika maeneo yao, kwani kwa vyovyote hawakuwa wamesimamia vyema ulinzi wa sungusungu.
Hii ilisaidia sana kupunguza uhalifu na tuseme ukweli, ilifikia wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam walikuwa wakilala milango wazi bila hofu yoyote ya kuvamiwa au kuibiwa.
Lakini pengine katika kumpuuza, mpango huu ukafa kifo cha kawaida mara tu baada ya kutimuliwa kwake serikalini. Uhalifu ukarejea kwa kasi ya kutisha na hivi sasa tunavyoongea, matukio ya kihalifu yanayosababisha vifo yanaendelea kana kwamba hatuna vyombo vya ulinzi.
Kuna wakati yatupasa kuwa wakweli. Vijana wetu wa polisi ni wachache, hawawezi kuwepo kila eneo kwa wakati. Ulinzi wa sungusungu ungerejeshwa kwa lazima.
Watu lazima walinde maeneo yao, iwe mijini au vijijini. Hata kama haitafanya kazi kwa asilimia mia moja, lakini angalau inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa matukio haya ya kutisha ya kihalifu.
Pia, watendaji wa serikali katika ngazi za mitaa na vijiji, walazimishwe kuwajua watu wa maeneo yao, ikibidi kupata na picha zao hasa wageni, ili wanapofanya uhalifu, picha hizo zitumike kuwatafuta popote wanapokimbilia.
Vinginevyo, tutaendelea kuuawa kila siku na polisi hawatachoka kutuambia kuwa mtu mmoja, au wawili au watatu wamekamatwa kwa tukio fulani, lakini hakuna mabadiliko.
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za dhati katika kukabiliana na vitendo hivi kwa sababu inao uwezo mkubwa wa kuvikomesha! Nachochea tu kuhamasisha amani!