The House of Favourite Newspapers

Kange Lugola na wenzake wafutiwa mashtaka

0

lugolaDar es Salaam,

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amewagwaya wabunge watatu; Kangi Lugola wa Mwibara na wenzake wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa baada ya kuwafutia mashtaka   yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Licha ya Lugola, wabunge wengine ni Suleiman Ahmed Saddiq (Mvomero) na Victor Mwambalaswa (Lupa).

Wakati DPP akiwafutia mashtaka hayo na kuwaachia huru, wabunge hao wamesema wanatafakari hatua za kuchukua dhidi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kile walichokiitwa kuwadhalilishwa kwa kuwafungulia kesi hiyo, waliyoiita ya kisiasa.

Wabunge hao ambao wote wanatoka Chama cha Mapinduzi (CCM), walikuwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipandishwa kizimbani Machi 31.

Walikuwa wakikabiliwa na shtaka la kuomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Mbwana Magote.

Hata hivyo washtakiwa hao wote walikana shtaka hilo huku Lugola baada ya kusomewa shtaka hilo na kesi kuahirishwa akisema kuwa hiyo ni vita ya kisiasa ambayo haitawazuia kuendelea kutumbua majipu.

Awali, kabl ya kesi hiyo kuitwa jana mahakamani hapo, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo tayari umeshakamilika na ukaomba mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali.

Kufuatia taarifa na maombi hayo ya upande wa mashtaka, mahakama hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali ufanyike jana, ambapo washtakiwa walitarajiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo kabla ya kuendelea na ushahidi.

Hata hivyo baada ya kesi hiyo kuitwa jana kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo hayo ya awali, Wakili wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa aliyekuwa akisaidiana na Wakili wa Takukuru, Emmanuel Jacob, aliieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya kuenedelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili Mutalemwa alisema kuwa DPP ameamua kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Hakimu Respicius Mwijage aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alikubaliana na maombi hayo ya DPP na kuamuru washtakiwa hao waachiwe huru.

“Shauri hili linaondolewa kama DPP alivyoomba na washtakiwa mnaachiwa huru.”, alisema Hakimu Mwijage.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa huru, kwa niaba ya wenzake, Lugola alisema kuwa tangu walipofikishwa mahakamani hapo walianza na Mungu na wamemaliza na Mungu, na kusisitiza kauli aliyoitoa siku walipandishwa kizimbani kuwa kesi hiyo ni ya kisiasa.

“Kimsingi tangu mwanzo tulipofikishwa mahakamani hapa moyoni mwetu tulianza na Mungu na tuliahidi kumaliza na Mungu na tumemaliza na Mungu.”, alisema Lugola na kuongeza:

“Leo Mungu amejibu, tumeachiwa huru. Tunawaambia Watanzania kwamba kesi tuliyofunguliwa ilikuwa ni ya kutunga na ilitengenezwa kwa sababu za kisiasa.”

Lugola aliendelea kueleza kuwa kutokana na uamuzi huo Serikali kupitia Takukuru hawakuwa na ushahidi dhidi yao na kwama ndio maana wamebadilika hivyo kama kinyonga.

“Walisema kwamba wamekamilisha upelelezi na kuomba tarehe ya kutusomea maelezo ya awali, leo wanafuta kesi.”, alisema Lugola.

Alisema baada ya uamuzi huo sasa wataendelea kuwatumia wananchi waliowachagua katika majimbo yao huku wakiweka wazi kuwa wanakwenda kukaa na mawakili wao ili wajadili hatua za kuchukua dhidi ya Takukuru.

“Tutakaa na mawakili wetu tutafakari ni cha kufanya kutokana na udhalilishwaji huu tuliofanyiwa na baada ya hapo ndio tutajua  nini cha kufanya, lakini tunasikitishwa sana na udhalilishwaji huu tuliofanyiwa na Takukuru.”, alisisitiza Lugola.

Akiwasomea washtakiwa hao shtataka hilo, siku ya kwanza walipopandishwa kizimbani, Wakili wa Takukuru, Magela Ndimbo alisema kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo, Machi 15, 2016, kinyume cha kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Takukuru.

Alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo wakiwa katika Hotel ya Golden Tulip, iliyoko eneo la Masaki, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, na kwamba waliomba rushwa hiyo ili waweze kutoa mapendekezo mazuri ya Taarifa ya Hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.

Hakimu Mkazi Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo aliwaachia huru washtakiwa hao kwa dhamana kwa  masharti ya kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh5 milioni na kutakiwa kuwafikisa mahakamani hapo washtakiwa kwa tarehe na saa itakayopangwa.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa na hakimu kutoka nje ya mahakama, washtakiwa hao wakingali bado kizimani, walionesha kufurahia huku Saddiq na Lugola wakishangilia kwa kunyanyua juu mikono yote miwili wakionesha ishara ya ushindi.

Sambamba na kushangilia huko, Lugola pia aliwashukuru waandishi wa habari lakini akasema kuwa kesi hiyo ni virta ya kisiasa tu ambayo haitawakatisha tamaa wale walio tayari kutumbua majipu kuendelea kutumbua majipu hayo.

Nawashukru sana waandishi wa habari kwa coverage yenu. Licha ya vita hii ya kisiasa lakini wale tulio tayari kutumbua majipu tutaendelea kutumbua majipu.

Leave A Reply