The House of Favourite Newspapers

Kesi ya Mauaji ya Mwangosi… Hukumu Kutolewa Julai 21

0
mwangosi Daudi Mwangosi enzi za uhai wake.
Hukumu ya kesi ya mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel 10, Daudi Mwangosi itatolewa Julai 21 baada ya Mahakama Kuu kusikiliza majumuisho na maoni ya Baraza la Wazee. Kesi hiyo inamkabili askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Iringa, Prisifius Simon.
Akitoa majumuisho ya kesi hiyo jana, Jaji Paul Kihwelo alisema ni wajibu wake kutoa majumuisho kwa kuangalia mazingira na ushahidi uliomgusa moja kwa moja mtuhumiwa.
Jaji Kihwelo alieleza mahakama kuwa askari huyo anatuhumiwa kufanya mauaji hayo kwa kukusudia Septemba 2, 2012.
Alieleza kuwa jukumu la kuthibitisha kosa kwa mtuhumiwa ni upande wa mashtaka na wanatakiwa wathibitishe bila kuacha wasiwasi wowote na si jukumu la upande wa pili kuthibitisha kuwa mtuhumiwa hakutenda kosa.
Alitaja vielelezo ambavyo vilitolewa mahakamani bila kupingwa kuwa ni pamoja na ramani ya tukio, taarifa ya uchunguzi ya kifo cha marehemu, ungamo la mtuhumiwa na kitabu cha kuchukilia silaha ofisi za FFU.
mwangosi 2Vurugu zilizopelekea kifo cha Daudi Mwangosi
Akisoma majumuhisho kwenye upande wa ungamo, Jaji Kihwelo alisema maungamo yanayofanywa mbele ya mlinzi wa amani, yanaweza kutumika kutoa ushahidi.
Mtuhumiwa huyo alieleza mahakama wakati akitoa ushahidi wake kuwa kabla ya kufika kwa mlinzi wa amani, aliitwa kuhojiwa na RPC na RCO ndipo akaenda kufanya ungamo na kwamba hakufanya chochote zaidi ya kuambiwa asaini.
Akitoa maoni yake mmoja wa wazee wa mahakama, Khadija Husein alisema baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote kuanzia mwanzo hadi mwisho, wamegundua kuwa mtuhumiwa alienda kufanya ungamo kwa mlinzi wa amani akiwa huru na kusaini.
Khadija alisema si rahisi mtu kusaini kitu ambacho  hajakitolea maelezo, hivyo alichokisaini ndicho alichokitenda na alitoa ungamo akiwa huru bila kupigwa wala kutishiwa
MwangosiDaudi Mwangosi akiwa kazini.
Alisema endapo maelezo hayo yalikuwa si yake, yangepingwa mbele ya mahakama na wakili wake au yeye mwenyewe, lakini kwa kuwa yalipokelewa bila kupingwa hivyo ana hatia ya kutenda kosa bila kukusudia.
Mzee mwingine, Said Mbaga alipingana na maelezo hayo, akisema mtuhumiwa hana hatia kwa sababu shahidi wa kwanza hakuthibitisha kuwa alitenda kosa kwa sababu hakumuamuru kupiga bomu.
Mzee wa tatu, Sophia Ng’anguli alisema mtuhumiwa alitenda kosa bila kukusudia licha ya ushahidi wa upande wa mashtaka kuacha mashaka.
Alidai kitu cha msingi kinachomfunga mshitakiwa ni ungamo alilolitoa kwa mlinzi wa amani, ambalo aliandika na kusaini huku akikiri na kujutia kusababisha kifo cha Mwangosi.
Leave A Reply