The House of Favourite Newspapers

Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 2)

 

ILIPOISHIA WIKIENDA…

“Kama unakwenda kazini si ninaweza kwenda peke yangu?” Nikamwambia.

“Kwa nini uende peke yako wakati kadi yako imeandikwa bwana na bibi? Nakushauri ulale.”

“Si vizuri. Huyu mtu ni rafiki yangu na nimemthibitishia kuwa nitahudhuria.”

“Sawa. Tutaonana hapo asubuhi nikitoka kazini.”

Mke wangu alipotoka kwenda kazini kwake, nikaanza kujiandaa. Nilivaa ile suti yangu niliyokwenda kuolea, nikafunga kikuba cha rangi nyekundu na kutoka.

 

SASA ENDELEA…

NILIKODI teksi ya kunipeleka kwenye Hoteli ya Mkonge ilikokuwa inafanyika tafrija.

Teksi ilisimama mbele ya mlango wa hoteli. Wakati nashuka kwenye teksi nikakumbuka kwamba nilisahau kuchukua ile kadi ya mwaliko.

Ilinichukua kama sekunde thelathini kujipekua kwenye mifuko yangu yote nikiwa mbele ya mlango wa teksi. Nikaamini kwamba kadi yangu niliiacha nyumbani.

Kadi hiyo ilikuwa kama tiketi yangu ya kuingilia kwenye ukumbi huo. Bila kadi hiyo nisingeweza kuingia.

 

Nilifikiria kurudi nyumbani kuchukua kadi hiyo na kuja tena hoteli hapo. Niliona utakuwa ni mzunguko usio na maana. Kulikuwa na teksi nyingine iliyokuwa ikisimama nyuma ya teksi iliyonileta..

Nilitoa pesa, nikamlipa dereva wa teksi. Teksi iliondoka. Mimi nikabaki nimesimama nikiwaza. Ndani ya teksi iliyosimama, alishuka msichana mmoja, akanitazama kama mtu aliyekuwa akinifahamu, lakini mimi sikumpatiliza kwa sababu nilikuwa simjui.

 

Alinitolea tabasamu kabla kunisalimia.

“Habari ya siku?”

“Nzuri,” nilimjibu kwa mkato kwa sababu nilikuwa nimefadhaika baada ya kugundua nilikuwa nimesahau kadi yangu.

“Mbona umesimama kama uliyefadhaishwa na kitu?” Akaniuliza.

“Ni kweli,” nilimwambia na kuongeza;

 

“Nimesahau nyumbani kadi yangu ya kuingilia.”

“Oh si tatizo. Unaweza kuingia kwa kadi yangu. Kadi yangu imeandikwa bwana na bibi, lakini niko peke yangu. Tunaweza kuingia pamoja,” akaniambia.

“Nashukuru sana kwa sababu nilikuwa nimeshachanganyikiwa.”

Msichana huyo aliitoa kadi yake kwenye pochi akawa anatabasamu.

“Unasahauje kadi nyumbani. Una mawazo gani?” Akaniuliza.

“Kusahau ni kitu cha kawaida kwa binadamu, nilisahau tu,” nikamwambia.

“Twen’zetu.”

 

Nikaingia ndani ya hoteli hiyo na msichana huyo niliyekuwa simfahamu, lakini wakati wote alikuwa akinitolea tabasamu. Tulikwenda katika eneo la ukumbi ambako tafrija hiyo ilikuwa inafanyika, tukaingia ndani ya ukumbi huo kwa kutumia kadi ya msichana huyo.

Mara tu baada ya kukaa kwenye viti, msichana huyo aliniuliza.

“Msami umekuwa wapi siku nyingi?”

Nikashtuka kidogo kisha nikamuuliza.

 

“Nani…mimi…?”

“Ndiyo, nakuuliza wewe.”

“Mimi nipo hapahapa Tanga, lakini isije ikawa umenifananisha. Mimi siitwi Msami.”

“Una maana umenisahau mimi niliyekuwa mpenzi wako halafu ukanitoroka bila kosa?”

“Hapana. Siye mimi. Labda umenifananisha tu.”

“Sijakufananisha. Ninakufahamu wewe ni Msami. Sijui nilikukosea nini. Unakumbuka kwamba dada yangu alifariki dunia?”

“Simfahamu.”

 

“Msami mbona uko hivyo! Una maana hata shemeji yako, Ester humfahamu?”

Nikahisi huenda msichana huyo alikuwa amenifananisha na mtu aliyekuwa mpenzi wake.

Mimi nilikuwa nimefanana sana na ndugu yangu Charles aliyekuwa amefariki dunia. Angeniita kwa jina la Charles ningejua amenifananisha naye, lakini jina alilotumia lilikuwa geni kwangu.

Msichana alipoona ninakana kufahamiana naye akanyamaza kimya na kubaki kunitazama.

 

Nilibadilisha mazungumzo, tukawa tunazungumza mazungumzo mengine huku tukinywa vinywaji. Muziki ulipomkolea msichana huyo aliniomba twende tukacheze, nikaenda kucheza naye. Alikuwa hodari sana wa kucheza na kwa kweli alinifurahisha.

Nilikwenda kucheza naye karibu mara nne. Mtu aliyekuwa akishughulika kupiga video alikuwa akimrikodi sana msichana huyo kwa jinsi alivyoonesha umahiri wa kucheza.

Sherehe ilimalizika saa nane usiku. Tukatoka. Tulipanda teksi moja na yule msichana.

 

“Unaishi wapi?” Nikamuuliza.

“Kwa sasa ninaishi Kwaminchi. Nilihama kule Sahare.”

“Basi acha teksi ikupeleke wewe kwanza.”

“Ni vizuri ili upajue nyumbani kwangu.”

Teksi ikatupeleka Kwaminchi. Msichana huyo ambaye sikutaka kumuuliza jina lake wala kumtambulisha jina langu alimuelekeza dereva wa teksi nyumba aliyokuwa anaishi.

Teksi iliposimama mbele ya nyumba hiyo msichana aliniambia.

 

“Karibu ndani.”

“Kwa vile nimeshaijua nyumba tunaweza kutembeleana siku nyingine.” Nikamwambia.

“Lakini kwa leo si umeshafika? Kwa nini uishie nje? Ingia ndani upumzike kidogo tu halafu utarudi kwako. Teksi ziko nyingi hapa.”

Msichana alinishawishi mpaka tukashuka pamoja kwenye teksi.

Nilitaka kumlipa dereva, lakini yeye ndiye aliyewahi kutoa pesa. Alimlipa mwenye teksi. Teksi ikaondoka.

“Karibu.”

 

Tukaelekea kwenye mlango wa nyumba wa upande wa kushoto. Nyumba yenyewe ilikuwa na milango miwili. Mlango wa upande wa kulia na mlango wa upande wa kushoto.

“Tuko wakazi wawili, lakini kila mtu ana upande wake,” msichana huyo aliniambia.

Kitu ambacho kilionesha kuwa alikuwa akiishi peke yake alitoa ufunguo kutoka kwenye pochi yake akafungua mlango huo na kunikaribisha ndani.

Tulipoingia ndani tulitokea kwenye sebule pana na nadhifu.

 

“Karibu ukae.” Akaniambia.

Nikakaa kwenye kochi. Msichana aliingia ndani zaidi. Baada ya muda kidogo alirudi tena akiwa amevua zile nguo zake na kujifunga khanga kifuani akiwa ameshika chupa mbili za bia na bilauri mbili. Aliziweka kwenye kochi, akavuta meza ya kioo karibu na kochi kisha akaweka zile chupa pamoja na bilauri.

Alikaa karibu yangu, akazibua chupa zote mbili na kumimina kilevi kwenye bilauri zote mbili.

 

“Karibu ujichangamshe kidogo.” Akaniambia huku akinisogezea bilauri moja. Sikuhitaji kuendelea kunywa muda ule, lakini nilishindwa kumkatalia. Nikaipokea ile bilauri na kupiga funda kilevi hicho kisha nikairudisha bilauri juu ya meza.

Niseme ukweli kwamba katika kuingia kwenye nyumba ya msichana huyo ambaye nilikuwa simfahamu na kukubali kunywa naye kilevi humo ndani sikutumia kabisa taaluma yangu ya ukachero.

Kweli wanawake ni watu wepesi sana kumzuga mtu, pengine ni kutokana na maumbile yao na mvuto wao kwa wanaume.

 

Nakumbuka nilipiga mafunda matatu tu ya bia halafu sikuweza kufahamu tena kilichoendelea. Nilipitiwa na usingizi mzito, nikalala palepale. Sikujua aliniwekea kitu gani kwenye pombe.

Nilipokuja kuzinduka, nilijiona nilikuwa nimelala kitandani chumbani kwa msichana huyo, lakini mwenyeji wangu hakuwepo kitandani. Nilikuwa peke yangu na taa ilikuwa inawaka.

 

Nikainuka na kukaa. Kichwa changu kilikuwa kina mawengemawenge kama mtu niliyekuwa nimelewa sana. Suti yangu bado nilikuwa nayo mwilini. Sikuwa nimeivua. Miguu ilibaki na soksi. Viatu vyangu vilivuliwa na kuwekwa kando ya kitanda.

Kumbukumbu zangu ziliniambia kwamba nilikuwa nimekaa sebuleni na msichana aliyenikaribisha mle ndani, tukinywa bia, lakini sikuweza kufahamu niliendelea kunywa hadi muda gani na nini kingine kilitokea. Fahamu zilinipotea.

 

Nikajiuliza iwapo fahamu zilinipotea baada ya kulewa sana. Lakini mimi mwenyewe sikukumbuka kama niliendelea kunywa sana. Nikajiuliza tena kama fahamu zilinipotea nikiwa nimekaa sebuleni, ni nani aliyeniingiza chumbani na kunilaza kitandani au niliingia na kulala mwenyewe nikiwa sijifahamu?

 

Maswali yote niliyojiuliza yalikosa majibu. Ilikuwa vigumu kupata majibu kwa sababu mambo yote hayo yalipokuwa yakitokea nilikuwa sijielewi. Kama kulikuwa na majibu yalikuwa ya kukisia tu yasiyo na usahihi. Inawezekana nilikunywa sana. Yule msichana alipoona nimelala alinishika na kuniburuza chumbani mwake na kunilaza kitandani.

 

Nikaitazama saa yangu iliyokuwa mkononi. Ilikuwa saa kumi na dakika kumi alfajiri. Nikashuka kitandani na kuvaa viatu vyangu. Baada ya kuvaa viatu nikaenda kwenye mlango. Nilijaribu kuufungua nikaona unafunguka. Nikatoka. Nilitokea kwenye sebule mahali ambapo nilikuwa nimekaa awali na yule msichana.

Juu ya ile meza kulikuwa na chupa moja tu ya bia iliyokuwa upande niliokuwa nimekaa mimi. Chupa hiyo ilikuwa imebaki na pombe. Kiasi kilichonywewa kilikuwa kidogo, hali iliyoonesha kuwa sikuwa nimekunywa sana.

 

Nikayazungusha macho yangu huku na huku. Macho yalipokwenda kwenye mlango wa nje nilishtuka. Mlango ulikuwa wazi uliofunguka kidogo. Kando ya mlango kwa ndani msichana aliyenikaribisha ndani alikuwa amelala chini kichalichali, mwili wake ukiwa na khanga aliyokuwa amevaa.

Upande wa kichwani kwake alikuwa amelalia dimbwi la damu nyeusi iliyoganda!

Macho yake yalikuwa wazi, lakini yasiyoona chochote.

“Nini tena?” Nikajiuliza.

 

Nilisogea karibu na mlango huo, nikainama na kumtazama msichana huyo vizuri.

Kutokana na uzoevu wangu wa kutazama nyuso za maiti, niligundua mara moja kuwa msichana huyo hakuwa hai. Alikuwa ameuawa.

Pembeni mwa kichwa chake kulikuwa na vipande vya chupa ya bia iliyovunjika ambavyo navyo vilikuwa na damu. Nilishuku kwamba chupa hiyo ndiyo iliyokuwa na bia aliyokunywa msichana huyo.

“Sasa hili ni balaa!” Nikawaza.

 

Kutokana na mbinu zetu za kazi ya upolisi, mimi niliyekuwa na msichana huyu ndiyo ninakuwa mtuhumiwa namba moja. Lazima nikamatwe na kuwekwa ndani kwa tuhuma za mauaji. Balaa limeshaniangukia mimi wakati msichana mwenyewe hata simjui ni nani!

Je, nini kiliendelea? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Comments are closed.