The House of Favourite Newspapers

Kilichojificha mgogoro wa Zanzibar -3

0

Kama tulivyoona wiki iliyopita aliyetangaza Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964 ni John Okello, nilipata simu wasomaji wakitaka kujua huyu mtu alitoka wapi? Nilimuelezea.

Bado watu wanataka kujua ilikuwaje uhasama ukazagaa visiwani Zanzibar?
Msomi mmoja anaelezea kuwa, kabla ya Mapinduzi kulikuwa na uchaguzi mwaka 1961 na uligombania siyo nafasi ya kutawala tu, bali maana ya ‘Mzanzibari’ ni nani.

Wakati ASP iliona Zanzibar ni sehemu ya Afrika na watu wake wengi wakiwa ni wenye asili ya bara; ZNP iliiona Zanzibar kama taifa la Kiislamu ambalo ukaribu wake zaidi ni kwa Waarabu wa Mashariki ya Kati na si watu wa Tanganyika.

Baada ya uchaguzi wa 1961 Waafrika waliwashambulia Waarabu kila kona visiwani. Vurugu zilipotulia, watu 68 waliuawa na zaidi ya watu 300 kujeruhiwa. Itambuliwe hii ilitokea kabla ya Muungano na kabla ya mapinduzi ya Zanzibar.

Yalikuwa ni matokeo ya hotuba za kinasaba zilizokuwa zinachochewa na pande mbili za ASP na ZNP. Vurugu zile zilikuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya sera za kibaguzi ambazo Mwalimu Nyerere hakuzipenda na wote aliuona ni ukaburu.
Hata Abdurahman Mohammed Babu alipoamua kujitenga na ZNP na kuunda Umma, madhara yalikuwa tayari yameshafanyika. Uchaguzi wa 1963 kabla ya uhuru, ulitarajiwa kuwa mwamuzi wa nani anashika madaraka baada ya uhuru.

Chama cha ASP kilipata kura nyingi za watu asilimia 54.2 (popular votes), lakini ni ZNP na ZPPP vikipata viti vingi. Na kama ilivyohofiwa, serikali ikaja na sera ya kukipiga marufuku chama cha Umma (Umma hakikushiriki uchaguzi wa 1963), lakini zaidi ya hivyo ikafukuza polisi wenye asili ya bara (ikumbukwe ilikuwa ni kabla ya Muungano) na kuwaajiri watu wenye asili ya uarabuni.

Leave A Reply