The House of Favourite Newspapers

Kilichonitokea Baada ya Kubakwa na Kaka Yangu-34

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipomaliza kuwasimulia yule mama na wengine waliokuwemo kwenye gari wakasikitishwa na mkasa wake na kumshauri akawafungulie mashtaka Evance na mama yake, ambapo msichana huyo aliwaambia hakuwa tayari kufanya hivyo akaanza kulia. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Kufuatia kulia, wote wakaanza kunisihi ninyamaze nikawaambia ingawa sikupenda kuwafungulia kesi na kumuachia Mungu, kitendo walichonifanyia kiliniumiza sana.

“Hata sisi tumeguswa na unyama uliofanyiwa ndiyo maana tunakushauri ukawashtaki ili sheria ichukue mkono wake,” dereva aliniambia.

Nilimwambia sawa lakini siku moja Mungu angewahukumu kwa sababu yeyote anayewafanyia wengine ubaya, malipo yake yapo hapahapa duniani.

Walipoona sikukubaliana na ushauri wao, waliniacha tukaendelea na safari huku kila mmoja akiwa ananionea huruma, kabla ya kufika Nzega yule mama aliniita jina langu na kunipa pole kwa yote yaliyotokea na kuwalaani mama na Evance.

Mama huyo ambaye tayari alijua hata Mbeya kwa mama mkubwa nilikokuwa nakwenda hakukuwa kwa ndugu zangu wa damu, aliniambia kama sitajali niongozane naye kwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

“Mwanangu, mkasa wako umenigusa sana, kama hautajali naomba twende tukaishi wote nyumbani kwangu Dar es Salaam, nitakutafutia shule ili uendelee na masomo na utakuwa miongoni mwa watoto wangu,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.

Kwa kuwa nilijua hakuna kitu kitakachonikomboa maishani mwangu kama elimu, nilifurahi sana kupata nafasi hiyo adimu ambayo nilikuwa naamini ilipotea, nikamkubalia yule mama.

“Nashukuru sana mwanangu kukubali kwenda kuishi nami, hata mume wangu nikimwambia habari zako atasikitika na kukupokea bila kinyongo,” Dorcas anasema yule mama alimwambia.

Nilimshukuru sana kwa ukarimu wake, hata yule dada alimuunga mkono ambapo safari iliendelea na kuwasili Nzega mapema.

Tulipofika tukaenda nyumbani kwa ndugu yao, katika maongezi yao waliambiwa mama aliyekuwa mwenyeji hakuwepo alikuwa amekwenda Igunga.

Kufuatia taarifa hiyo, tuliondoka Nzega kwenda Igunga kwa ndugu yao mwingine ambako tulimkuta yule mama, baada ya maongezi waliamua kuelekea Dar.

Njiani tulikuwa tukizungumza mambo mengi utafikiri tulifahamiana muda mrefu, yule dada niliyemkuta mle kwenye gari kumbe naye alikuwa abiria.

Katika maongezi alitusimulia mateso aliyowahi kupata kutoka kwa mama yake wa kambo namna alivyokuwa akilala bila kula huku akiwa amefanyakazi kutwa nzima.

Alitueleza kuwa kila alipomweleza marehemu baba yake mambo aliyofanyiwa na yule mama, alimgeuzia kibao na kumchapa na kumtuhumu alikuwa muongo.

Mkasa wake ulituhuzunisha sana ambapo aliniambia nisihuzunike sana kwani kila kinachotokea katika maisha yetu kinakuwa na sababu.

Alisisitiza kama nitarudi shuleni nisome kwa bidii kwani elimu pekee ndiyo ingeweza kunikomboa na kunifanya nisahau yote yaliyonitokea, akaniambia nimshukuru yule mama aliyeamua kunichukua niende kwake Dar kwa ajili ya kusoma.

Nilimshukuru yule dada kwa kunipa moyo, tulipofika Singida alituaga kwani alikuwa amefika, kwa jinsi tulivyozoeana tulihuzunika lakini hatukuwa na la kufanya zaidi ya kutakiana heri. Baada ya yule dada kuteremka, yule mama ambaye mpaka muda huo sikuelewa kama lile gari lilikuwa lake au la nani alimwambia dereva akipata abiria amchukue ili tupate pesa ya matumizi njiani.

Dereva aliondoa gari hadi maeneo ya stendi kuu ya Singida akawaeleza akina mama f’lani kwamba alikuwa akielekea Dar na kulikuwa na nafasi ya mtu mmoja.

Mama mmoja mwenye asili ya Kiarabu aliyekuwa na pochi alichangamka akaingia kwenye gari, safari ikaanza huku kila mmoja akiwa kimya hadi dereva alipoyumbisha gari wakati akiwakwepa mbuzi waliokatiza ghafla barabarani.

Kufuatia kuyumba huko kwa gari, yule mama wa Kiarabu alipata mshtuko akaangukia upande wa kulia wa kiti alichokuwa ameketi na kupoteza fahamu.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni nicheki kupitia namba hizo hapo juu.

Leave A Reply