The House of Favourite Newspapers

Kipi Bora, Kumfuatilia Au Kutomfuatilia Mwenzi Wako!

0

Love.jpgMUNGU ni mwema sana. Amenikutanisha na wewe msomaji wa safu hii ili niweze kukupa kile ambacho nimekuandalia katika suala zima la uhusiano.

Niwashukuru wote waliotuma pongezi kwa mada iliyopita iliyohusu umuhimu wa wapendanao kuzungumza ukweli. Naamini kupitia meseji zenu mlizonitumia, inadhihirisha mlijifunza kitu. Karibuni katika mada mpya ya leo yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu.

Kizazi cha sasa kimegawanyika katika suala hili. Wapo wanaoamini kwamba mapenzi hayana haja ya kuchungana. Mwanaume anampa uhuru mwanamke, ajichunge mwenyewe. Hahitaji kumfuatilia mkewe kwamba, uko wapi? Unafanya nini achilia mbali  kuhoji ‘mbona leo mke wangu umechelewa sana kurudi kazini?’

Mwanaume wa aina hiyo hana muda wa kutilia shaka urafiki wa mkewe na vijana wa mtaani. Mkewe anajiachia anavyotaka ili mradi tu muda fulani anajua atahitajika kwa mumewe. Hapo mwanamke ni rahisi sana kuwasiliana na mpenzi wake wa zamani, wakakumbushiana stori na hata kuonana pasipo kuharibu ratiba yake kwa mumewe.

Vivyo hivyo kwa mwanamke. Anampa uhuru mumewe. Hamfuatilii. Hamtilii shaka kumhoji kwamba kwa nini leo mume wangu umechelewa kurudi. Hamuulizi mbona umebadilika tabia au kwa nini mara nyingi unaonekana na mtu fulani katika mazingira hatarishi, hiyo si kazi yake.

Anachoangalia yeye ni kutimiziwa mahitaji yake ya nyumbani. Mwenzi wake hana habari naye. Anachoamini ni kwamba, mwanaume anajichunga mwenyewe. Mwanaume wake anakuwa huru hata kuwasiliana na mpenzi wake wa zamani ili mradi asitibue ndoa yao.

Kwa tafsiri ya wengi, mwanamke au mwanaume anayempa uhuru mwenzi wake, huwa anaamini kwamba si rahisi kumchunga. Ukiwauliza wanawake kwa nini hawawachungi waume zao, watakuambia hawafanyi hivyo kwani si jambo rahisi. Hawawezi kutembea nao kila watapokwenda.

Bahati mbaya sana, mtu anapopewa uhuru mkubwa, mianya zaidi ya kushawishiwa inaongezeka. Wengi hujikuta wakisaliti kwa sababu tu, wana uhuru mpana. Kumchungachunga mpenzi wako si jambo zuri hususani pale linapozidi kipimo lakini upo umuhimu mkubwa wa kumchunga mke au mumeo.

Kumchunga mtu wako kwa maana nyingine ni kumjali. Kuna tatizo gani ukimjali mpenzi wako? Kuna tatizo gani ukijua ratiba ya mwenzi wako na hata pale anapochelewa kurudi ukamuuliza, ‘mbona leo umechelewa mpenzi wangu?’

Kauli ya mbona leo umechelewa kurudi inaweza kuwa mbaya kama yule anayeulizwa anakuwa ana madhambi yake. Kama hana madhambi, kauli hiyo hugeuka kuwa faraja kwamba mwenzangu ananijali. Ndiyo maana amepatwa na wasiwasi wa kwa nini siku hiyo amechelewa.

Watu wengi huwa wanachukia kuulizwaulizwa kila wakati. Wanasema wanakereka kufuatiliwafuatiliwa. Tengeneza mazingira ya kuaminika ili mwenzako akuamini. Kama umeshatengeneza mazimngira hayo na kweli huna madhambi na ukaona bado mwenzako ana shaka na wewe zungumza naye ili umuondoe shaka.

Ukichunguza kwa makini, hakuna mtu ambaye hapendi kujaliwa. Huwa inageuka kero pale inapozidi. Pale ambapo kila wakati mtu anakuwa na shaka na mwenzake. Anahisi anaibiwa. Kila sehemu mke au mumewe anapokwenda, naye anahakikisha anamfuatilia.

Anamkataza kuongea na watu fulani. Hilo ndiyo tatizo. Mpe uhuru mwenzi wako lakini usizidi kipimo. Mpe uhuru wa kuongea na marafiki zake lakini wakati mwingine unapaswa kumueleza namna ambavyo anapaswa kutovuka mipaka.

Wapendanao lazima wajiheshimu. Waheshimiane. Huwezi kuwa mke au mume wa mtu halafu ukataka usiulizwe uko wapi. Au mbona leo umechelewa kurudi. Tengeni muda mzuri wa kulijadili suala hilo. Msioneane aibu na muwekeane mikakati mizuri ya kuishi.

Elezaneni kwamba mkitaka kuishi kwa upendo, kila mmoja anapaswa kujilinda mwenyewe lakini pia kumlinda mwenzake. Kila mmoja anapaswa kumjali mwenzake. Kufuatiliana ni suala la kawaida lakini tu lisizidi kipimo na kugeuka kuwa kero.

Uhusiano mzuri ni ule wa kujaliana. Kama mtu hakujali, anakuacha huru ufanye unalotaka, hapo lazima utilie shaka. Uhoji kuna mapenzi ya dhati? Yawezekana hakupendi au anatumia uhuru huo kufanya mambo yake mabaya.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply