The House of Favourite Newspapers

Kiungo Simba afanya mazoezi Yanga SC

0

MSUVA MDOGO James Msuva.

Wilbert Molandi na Nicodemus Jonas
UONGOZI wa Yanga upo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mdogo wake, Simon Msuva ambaye ni James Msuva wa kuichezea timu hiyo.

James anayecheza nafasi ya winga ya kulia na kushoto, kabla ya kutua Yanga alikuwa akiichezea timu ya vijana ya Simba chini ya Kocha Nico Kiondo.

Kiungo huyo, juzi Jumatatu asubuhi alionekana kwenye mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba, kiungo huyo licha ya kuichezea kwa muda mrefu timu hiyo, hakuwa na mkataba kutokana na yeye mwenyewe kugoma kusaini kuichezea timu hiyo.

Kiliongeza kuwa, kiungo aligoma kusaini mkataba kutokana na kushindwa kufikiana makubaliano mazuri kati na viongozi wa Simba kabla ya kutua Yanga kwenye msimu huu wa ligi kuu.

“Ni kweli kabisa mdogo wake Msuva alikuwa akiichezea Simba kwa muda mrefu, lakini akiwa na Simba alikataa kusaini mkataba kwa kile alichodai hajaridhika na ofa aliyotangaziwa na viongozi.

“Na kingine katika makubaliano yake yalikuwa ni kufanya mazoezi na timu kubwa ili apate nafasi ya kucheza kwenye ligi kuu ili kiwango chake kionekane uwanjani.

“Hivyo uongozi umeshtuka na taarifa za James kuanza kufanya mazoezi na Yanga, baadhi ya viongozi wamempigia kumuita aje kufanya mazungumzo na viongozi, lakini mwenyewe amekataa,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa James kuzungumzia hilo, alisema: “Ni kweli nipo Yanga hivi sasa, hivyo nisingependa kulizungumzia hilo kwa sasa kama ulivyoniona kwenye mazoezini, nilishindwa kujiunga mapema na Yanga kutokana na majeraha.

“Sasa sipo tena na Simba, nimejiunga na Yanga hivi karibuni kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwa kuanza kwenye kikosi cha vijana cha U20 kinachofanya mazoezi ya pamoja na kikosi cha wakubwa akina Kamusoko (Thabani) na Ngoma (Donald).”

Akizungumza na Championi Jumatano, kocha Kiondo alisema muda umepita tangu nyota huyo ahamie Yanga ambayo katibu wake, Dk. Jonas Tiboroha amesema James ni mchezaji wao halali kwa sasa.

“James hayupo kikosini mwangu muda mrefu sasa, nasikia kwa sasa yupo Yanga amemfuata kaka yake (Simon),” alisema kwa ufupi Kiondo.

Dk Tiboroha alisema: “Ni kweli James kwa sasa ni mali yetu na yupo wenye kikosi chetu cha vijana chini ya miaka 20 na anaendelea na mazoezi ya kipindi hiki ambapo kikosi cha vijana kimeunganishwa na cha wakubwa.”

Leave A Reply