The House of Favourite Newspapers

KUMRUHUSU MKE AFANYE KAZI, BIASHARA CHANZO CHA USALITI ?

NI Jumatatu nyingine Mungu ametukutanisha hapa kwenye kilinge chetu cha kupeana elimu ya masuala ya uhusiano na maisha kwa jumla. Hapa kila wiki tunajifunza masuala mbalimbali ambayo yanahusu maisha yetu ya kila siku, ugomvi, migogoro ya kila mara na hata furaha.

Kama mada ya leo inavyojieleza, ukizungumza na wanaume wengi waliooa kwa sasa watakuambia kitendo cha kumruhusu mwanamke afanye kazi au biashara mahali fulani ni kichocheo kikubwa cha usaliti.

Watakupa hoja zao kama vile mwanamke ni dhaifu. Ni wepesi kushawishika na hoja nyingine kadha wa kadha. Ndiyo maana baadhi ya wanaume wamekuwa na misimamo yao kwamba hawataki wanawake wao wafanye kazi au biashara.

Wanataka wanawake wao wawe wa kukaa nyumbani, wakiwa wamejisitiri na kuwahudumia. Ukiwauliza kwa nini, watakupa hoja kibao na wengine wakikupa hata hoja za kidini kwamba imani yao inawataka wanawake wakae nyumbani waletewe na wanaume zao.

Wenye imani hiyo kwa namna moja au nyingine, wanaweza kuwa na hoja hasa kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo hili. Ni ukweli usiopingika kwamba, ni wanawake wachache mno wanaweza kuhimili vishawishi

vya wanaume wakware ambao kwa namna yoyote wanataka penzi la wake za watu.

Mathalan, mke wako anafanya biashara ya grosari, wateja wake wanaokuja pale ni watu ‘wazito’ kidogo. Mmoja kati yao anapokuja, anamfanya mkeo faida ya siku hiyo ionekane bila hata ya kumulika kwa ‘tochi’. Gharama anazotumia zinatosha kabisa mkeo kutowahudumia watu wengine wote na akapata faida ya siku.

Kwa maana nyingine, anaweza kumuambia mkeo kwa siku hiyo asifungue grosari na akampa faida ya siku nzima bila kufanya kazi yoyote. Sasa mtu wa aina hiyo unadhani anaweza kumpoteza kirahisi? Anaweza kuwa na ujasiri wa kumuwekea mipaka  atakapomfanya rafiki wa karibu?

Vivyo hivyo kwenye ajira, wapo mabosi ambao kwa gharama yoyote wapo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanawateka wake za watu. Mke wako atapewa promosheni nyingi zikiwemo za kupandishwa cheo, ofa mbalimbali ambazo kimsingi ni nadra sana kuzikataa.

Anapewa mtaji wa kufanya biashara, anapewa fedha ambayo pengine wewe kama mumewe ni adimu sana kuweza kuipata pengine hata ukijikusanya kwa miezi sita au mwaka mzima. Anapewa pesa hiyo kama msaada bila kuambiwa lolote, unadhani siku akiambiwa suala la kuchepuka ataweza kuruka kihunzi?

Kumbe basi, suala hili ni mtambuka. Tunapaswa kila mmoja kujitafakari na kuchukua hatua. Wewe kama mke au mume wa mtu, usijirahisi. Unapaswa kujitambua wewe ni nani na unapaswa kusimama kwenye msimamo gani kama mke au mume wa mtu.

Kujiheshimu ni silaha kubwa ya kukwepa usaliti. Dhamira yako ikiwa ni kuingia kwenye ndoa, hakikisha kwamba nafsi yako inakuwa imesharidhika. Ridhika na kile kidogo ulichonacho, ridhika na mtu wako maana huyo ndiye ambaye Mungu amekupa.

Yule anayekushawishi si wako, amekuja kwa bahati mbaya na ataondoka wakati wowote pindi atakapojisikia. Hana cha kupoteza maana ni tamaa tu imemuongoza, kesho na keshokutwa atamtamani mwingine, atakutupa wewe akiwa ameshakutumia vya kutosha na hana hamu na wewe.

Acha kujirahisisha kwa sababu utadharaulika sana pale ambapo jamii yote itajua kwamba umetumiwa na kuachwa solemba, dunia utaiona chungu. Ni hatari pia kusaliti maana unaweza kuhatarisha afya ya mwenzako kama si familia yako.

Kikubwa ni kujiheshimu, kuwa na msimamo. Huwezi kumzuia mwenza wako kufanya biashara au kazi kwa sababu ya kuhofia usaliti. Kila mmoja ajue usaliti ni dhambi kubwa, usaliti unaharibu uhusiano na unaweza kusababisha hata mauaji!

Nifuate kwenye kuraza zangu za mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Comments are closed.