The House of Favourite Newspapers

Kwa Mwanangu Nitakayemzaa – 44

0

Destiny anasafiri hadi Mwanza, Kundi la WAB lilikokuwa linatarajia kufanya shambulio kwenye Hospitali ya Rufaa Bugando.

Akiwa huko, amebanisha mahali fulani eneo la tukio alimuona Mtima na Abdulrahman wakiendelea kuua watu ovyo, Shauku ya kuwasogelea walipo ikapanda, akatoka alipokuwa na kukimbia kuwafuata lakini ile anavuka barabara bila kutarajia lori kubwa la mizigo lilitokea nyuma na kumgonga akagalagala kwenye barabara ya lami, damu ikatapakaa kila kona.     

Teremka Nayo…

 

 

DENIS Boti alikuwa mshona viatu maarufu jijini Mwanza. Tangu anaianza shughuli hiyo miaka ishirini ilishapita, aliianza akiwa na miaka 31 wakati huo alikuwa na miaka 51, watu wengi walimfahamu kwa jina la mzee wa Kiatu na Sindano.

Shughuli hiyo kwa mzee Boti ilikuwa ndiyo kila kitu. Ilimsaidia kumudu kujikimu kimaisha, akimhudumia mkewe, watoto wake watano pia alifanikiwa kuwa na makazi ya kawaida huko katika Mtaa ya Kirumba.

Kila siku asubuhi, majira ya saa mbili ilikuwa ni kawaida kwa mzee huyo kufungua kijiwe chake kilichokuwa karibu kabisa na ilipo Hospitali ya Rufaa Bugando.

Siku hiyo kama kawaida yake alikuwa kijiweni kwake hapo akiendelea na kazi huku akipiga porojo na baadhi ya wateja waliyokuwa wamekusanyika katika kijiwe hicho.

Maongezi yalikuwa yamenoga huku kwa kiasi kikubwa yakitawaliwa na ubishi wa kutabiri matokeo ya pambano la timu zenye utani wa jadi, Simba na Yanga ambalo lilitarajiwa kufanyika jioni ya siku hiyo, wakiwa wanaendelea na maongezi yao hayo mara ilisikika milio ya risasi kutoka karibu na pale walipokuwa.

Kila mmoja akahisi kuchanganyikiwa, hakuna kati yao aliyethubutu kukimbia zaidi ya kulala chini huku wakitetemeka kwa woga.

“Tumekwisha!” mzee Boti alimwambia kijana aliyekuwa jirani yake.

“Funga domo mzee,” kijana huyo alimjibu akizidi kujikunjia chini kwa woga.

Milio ya risasi iliendelea kurindima, watu walipoteza maisha baada ya kupigwa risasi na watu waliovamia eneo hilo wakiwa ndani ya gari aina ya Land-Rover Discover.

Akiendelea kukazia macho kilichokuwa kinaendelea mzee Boti alimshuhudia mwanamke mmoja akigongwa na lori kisha akaanguka kwenye lami na kugalagala mpaka mtaroni.

“Mungu wangu!” alisema mzee huyo.

“Nini?” kijana aliyekuwa pembeni yake alimuuliza.

“Mwanamke!”

“Amekuwaje?”

“Amegongwa na gari.”

“Sasa unataka kufanya nini?”

“Kumsaidia.”

“Hujipendi eeh!”

“Hata ikiwa najipenda, lazima nimsaidie.”

“Kivipi?”

“Ngoja uone.”

Kwa ujasiri mkubwa bila kujali hali ya hatari iliyokuwa inaendelea mahali pale, mzee Boti aliinuka na kwa tahadhari kubwa akaelekea hadi katika mtaro aliokuwa ameangukia Destiny kwa ajili ya kumsaidia.

Hali aliyomkuta nayo mwanamke huyo ilikuwa inatisha mno maana alikuwa na majeraha mengi mwilini mwake pia alikuwa amepoteza fahamu.

Mzee Boti alimtazama kwa macho ya huruma akifahamu Destiny alikuwa amepoteza maisha lakini baada ya kumchunguza kwa makini na kwa kutumia muda mrefu baada ya wauaji kuondoka, aligundua bado alikuwa anapumua. Akasaidiana na wasamaria wema ambao tayari walikuwa wamekwishafika eneo hilo kumfanyia huduma ya kwanza kisha wakamkimbiza katika Hospitali ya Agha Khan iliyoko kilometa chache kutoka mahali hapo.

Destiny akapokelewa na manesi kisha haraka akakimbizwa hadi kwenye chumba kilichoandikwa mlangoni Intensive Care Unit (ICU), kisha jopo la madaktari sita likaingia kazini, saa moja ikakatika wakimshughulikia maana baada ya vipimo iligundulika fuvu lake lilipasuka na damu kuvilia ndani.

Jambo hilo lilimaanisha hatari kubwa kwa msichana huyo, madaktari walimwambia mzee Boti mwanamke huyo asipopooza kutokana na tatizo hilo alilolipata basi ni lazima atapoteza kabisa kumbukumbu.

“Hakuna namna yoyote ya kumsaidia?” mzee Boti alihoji.

“Hakuna.”

“Maskini!”

“Huo ndiyo ukweli.”

Mzee Boti hakuwa na neno la kuongeza, alionekana kukata tamaa kiasi cha kudondosha machozi akimhurumia mwanamke aliyeamua kumsaidia kwa uwezo wake wote, alijaribu kuwashawishi tena madaktari kujaribu kumchunguza kwa mara nyingine, lakini waliendelea kusisitiza kuwa vipimo havikudanganya!

*    *    *

Baada ya kufanya shambulio la kutisha katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mtima na Abdulrahman walikimbilia hadi maeneo ya Jiwe Kuu walikojichimbia tangu waingie jijini humo.

Baada ya kufika mafichoni huko Abdulrahman alimshangaa rafiki yake Mtima baada ya kuchukua nyundo na kuanza kuzivunjavunja bunduki zake.

Alijiuliza ni kwa nini alifanya hivyo lakini hakupata jibu, alipomsogelea na kumuuliza, Mtima alimjia juu!

Je, nini kitaendelea? Usikose wiki inayokuja hapahapa!

Leave A Reply