The House of Favourite Newspapers

Kwanini Mapenzi Ndani ya Ndoa Zetu Yanapungua?

 HIVI mpenzi wako anapokuambia anakupenda, unafikiri nini zaidi kichwani mwako? Hapo ndipo kwenye msingi mzima wa mada yetu ya wiki hii. Wengi huishia kufikiri kirahisirahisi tu, kuwa anampenda fulani au mwenzi wake anampenda!

Je, umewahi kujiuliza, unampenda mpenzi wako kwa kiwango gani? Je, yeye anakupenda kwa kiasi gani? Upendo wake unamaanisha nini hasa? Upendo wako kwake una maana gani? Ni pendo la ndani kweli au tamaa za mwili?

Unaweza kujiuliza, inawezekana vipi ukampenda mtu hadi mkafikia kuingia kwenye ndoa, bado ikawa ni tamaa ya ngono tu? Hapa namaanisha kuwa yawezekana vipi, mpendane halafu muingie ndani maelewano yaondoke?

Heshima itoweke? Upendo utoweke? Inawezakana vipi? Wengi wanajiuliza: “Tumependana na mume wangu kwa miaka mingi, tumeingia kwenye ndoa na tumeishi humo kwa siku nyingi lakini kwa nini leo hii amebadilika?” Wasomaji wengi wananiuliza maswali yanay­ofanana na hayo (hasa wanawake). Ngoja nikupe kisa cha msomaji mmoja mwanamke, kisha tuingie kwa undani zaidi katika mada yetu.

KUTOKA KWA MSOMAJI:

Mimi nipo kwenye ndoa kwa miaka sita sasa, mimi na mume wangu tumejaliwa kupata watoto wawili – wa kike na wa kiume. Miaka mitatu ya mwanzo tuliishi kwa amani na upendo, nilipojifungua mtoto wa pili ndipo mabadiliko yakaanza.

Nimejikuta sina msisimko kabisa na mume wangu. Yaani nikimwangalia namuona wa kawaida tu, hanishawishi kwa chochote. Tatizo ni nini? Naomba ushauri wako. Rahima R, Arusha.

TUJIFUNZE KUTOKA KWA RAHIMA

Naamini wanawake wengi wana tatizo kama la Rahima. Si wanawake tu, hata wanaume nao wapo ambao hawana mvuto tena kwa wake zao. Wanawaona wa kawaida kabisa, hakuna msisimko wala ushawishi.

Wanatazamana kama magogo tu, maana hakuna jambo jipya linaloonekana mbele ya uso wa macho yao. Ni kweli, tatizo hili lipo, tena linatafuna sana ndoa nyingi. Swali la msingi hapa, kama Rahima anakiri alimpenda mumewe kwa dhati, wakafunga ndoa, iweje leo abadilike?

Ikiwa Rahima alikubali kwa hiyari yake kuunganishwa na mumewe, tena hadi wamefikia hatua wamezaa, mapenzi yamekwenda wapi? Hapo ndipo kwenye somo lenyewe ambalo bila shaka ndiyo itakuwa tiba ya wote wanaosumbuliwa na tatizo hili.

KUPENDA NA KUPENDWA

Kitu cha msingi ambacho unatakiwa kujifunza hapa ni kwamba, pendo la dhati huishi ndani. Penzi huwa haliishi, halina muda maalum wa kuishi ndani ya mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba, kama ulimpenda miaka 20 iliyopita kwa dhati ya moyo wako, basi leo huwezi kumchukia.

Upendo ukishaingia ndani ya moyo wa mtu hubaki humo milele, ila kuna mambo madogomadogo au pengine yanaweza kuwa makubwa, yanayoweza kusababisha kuuahirisha upendo kwa muda.

Nasema kuuahirisha kwa sababu hauwezi kuondoka. Rafiki zangu, ujue wazi kuwa, hadi mwenzi wako ameamua kuungana na wewe katika ndoa, si bahati mbaya. Hajabahatisha, bali amekuchagua kutoka kwa wengi.

Kama ndivyo, kwa nini penzi liondoke ghafla? Haiwezekani. Kwa maana hiyo, sasa ni wazi kuwa, penzi huharibiwa na sisi wenyewe. Kuna mambo ambayo yakifanyika hupunguza nguvu ya mapenzi na mwisho wake kusababisha matatizo kama nilivyoeleza hapo juu.

Itaendelea wiki ijayo.

#EXCLUSIVE: QUEEN MASANJA AFUNGUKA KUTOVAA STARA – ”MWANAMKE USIOGOPE KUANZA UPYA”…

CHOTA MAPENE ndiyo mchongo mpya town! Kwa shilingi 1,000 tu, yaani BUKU unajichotea mapene kibao au kupata nafasi ya kujishindia ZAWADI MBALIMBALI KILA SIKU, KILA WIKI kupitia Global TV, Global Radio na mitandao ya kijamii! ======================== Ingia kwenye simu yako📲, sehemu ya kufanyia malipo, andika namba ya kampuni 553111, kumbukumbu namba 255 au andika neno GLOBAL. Weka kiasi cha shilingi 1,000, weka namba yako ya siri, thibitisha na tuma.👍 PEASA UTATUMIWA MOJA KWA MOJA KWENYE SIMU YAKO!🤝👍💰

Comments are closed.