The House of Favourite Newspapers

Aliyepania Kumng’oa Mbowe Uenyekiti Chadema Afunguka – Video

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe(Chadema), ametangaza azma ya kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa ambayo kwa sasa inashikiliwa na, Freeman Mbowe, anayemaliza muda wake.

 

Mwambe ametangaza azma yake hiyo leo Jumanne Novemba 26, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema anaamini kuwa yeye ni mtu sahihi kuongoza jahazi hilo, tofauti na watu wasio na nia njema na chama hicho wanavyosema, ikiwamo kumsema vibaya.

 

Amesema anajua Mbowe amefanya mengi ila kama binadamu huchoka na kuhitaji usaidizi hivyo ameamua kujitokeza kumsaidia.

“Niwashukuru wale wote walioniunga mkono licha ya masimango na matusi waliyoelekezewa,” amesema Mwambe.

 

Amesema uchaguzi usio na ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kwanza sikutaka au nilishurutishwa.

Mbunge huyo amesema alianza kuona haja ya kugombea baada ya kumshuhudia Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akitishia kuachia nafasi hiyo kwa zaidi ya mara tatu.

 

“Nilianza kuona nina haja ya kugombea baada ya kumshuhudia Mwenyekiti wa chama chetu Mh Mbowe akituambia kwamba, asingependa aendelee kuwa Mwenyekiti wetu na kwamba anatamani angeacha nafasi hiyo kwa mtu mwingine ili aendeleze yale mazuri aliyafanya, nikaona ipo haja ya kumpokea kijiti hasa baada ya kueleza kwa kina madhira ambayo amepitia kwa vipindi vilivyotangulia nikaingiwa na huruma” amesema Mwambe.

 

Uchaguzi ndani ya chama hicho unatarajiwa kufanyika Desemba 18 mwaka huu ambapo kwa nafasi ya Mwenyekiti, ni Mwambe pekee amiejitokeza kuchuana na Mbowe ambaye anatetea nafasi hiyo.

 

Comments are closed.