The House of Favourite Newspapers

Lowassa Amewaponza Warithi wa Mbowe?

0

WINGU zito limetanda ndani ya Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kufuatia makada maarufu waliochukua fomu kuwania nafasi ya uwenyekiti ndani ya chama hicho, kuangushwa katika uchaguzi wa kanda.

 

Makada hao, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye aliyekuwa anatetea kwa mara ya pili uwenyekiti Kanda ya Pwani na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe ambaye pia alikuwa anatetea nafasi hiyo Kanda ya Kusini, wamezusha minong’ono mingi kutokana na anguko hilo.

 

Sumaye na Mwambe, wote walikuwa wajumbe wa kamati kuu ya Chadema kutokana na nafasi walizokuwa nazo za uwenyekiti wa kanda.

 

Aidha, Uchaguzi huo wa Chadema, sasa umetafsiriwa kuwa wa kihistoria kutokana na Mwenyekiti aliyeko madarakani sasa, Freeman Mbowe kupata upinzani kutoka kwa makada ambao ni wajumbe wa kamati kuu, tofauti na chaguzi zote zilizopita ambazo walijitokeza wagombea wasiokuwa na ushawishi katika kuwania uwenyekiti.

 

WALIVYOANGUKA

Sumaye ambaye alikuwa anawania nafasi ya uwenyekiti kanda ya Pwani, alishindwa baada ya kupigiwa kura nyingi za hapana.

Mgombea huyo alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, lakini alipata kura za NDIYO 28 sawa na asilimia 36.3 wakati kura za HAPANA zikiwa 48, sawa na asilimia 62.3.

 

Hata hivyo, Sumaye alisema alilifahamu anguko lake mapema, ingawa hakuwa ameamini.

“Niliambiwa ndani ya chama chetu hakuna demokrasia. Kwamba, ukigusa uwenyekiti wa Mbowe, basi utashughulikiwa. Mimi nimeamua kugombea na niko tayari kuadhibiwa kwa kutumia haki yangu hiyo ya kikatiba.”

 

“Kama kuchukuwa fomu ya uwenyekiti wa taifa, ndiyo niadhibiwe. Niko tayari kwa hilo,” alisema.

Vivyo hivyo, kwa upande wa Mwambe, alishindwa kutetea nafasi yake baada ya kuangushwa na mchezaji wa zamani wa soka, Suleiman Mathew.

 

LOWASSA ATAJWA

Anguko hilo la Sumaye na Mwambe katika nafasi zao, limeelezwa kuchochewa na vuguvugu la hamahama ambalo liliwakumba madiwani, wabunge na makada maarufu wa Chadema kuhamia CCM.

Sumaye ambaye alikuwa CCM na kuhamia Chadema, vivyo hivyo Mwambe alikuwa mgombea ubunge CCM katika jimbo la Ndanda kabla ya kuenguliwa na kuhamia Chadema.

 

Baadhi ya makada hao maarufu, awali walikuwa CCM lakini wakahamia Chadema na kupewa nyadhifa mbalimbali lakini baadaye wakarejea CCM kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Mmojawapo ni Edward Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais ndani ya Chadema ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

 

Kuondoka kwa Lowassa pamoja na wabunge zaidi ya watano ndani ya Chadema, kuliwanyong’onyesha wanachama wa chama hicho jambo ambalo limedaiwa kutowaamini makada wa chama hicho waliokuwa wametoka CCM.

 

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala ambaye pamoja na mambo mengine anasema wanachadema, wamepoteza imani na makada waliotoka CCM.

 

Prof. Mpangala anasema pamoja na mambo mengine, Chadema kimeonesha ukomavu kidemokrasia.

“Mimi naamini hao watu waliotoka CCM kwenda Chadema, hususan mtu mzito kama Lowassa kutoka Chadema na kurejea CCM, ni jambo ambalo limewapotezea imani wanachadema kwa makada wa CCM waliokuwa wamebaki Chadema.

 

“Sababu ya kugombea uwenyekiti, nadhani haina mashiko kwa sababu mwenyekiti mwenyewe Freeman Mbowe, aliruhusu kiti kiwe wazi watu washindane. Mbowe aliridhia kushindana na katiba imeruhusu, hili ni jambo linaloonesha demokrasia sahihi,” anasema.

 

Aliongeza kuwa ukomavu huo wa demokrasia pia umedhihirika kwenye nafasi ya Sumaye katika kanda ya Pwani, ambapo licha ya kuwa mgombea pekee lakini chama kiliruhusu kura za ndiyo na hapana.

 

Kutokana na hali hiyo, wapo wanaoeleza kuwa sababu ya kuanguka kwa Sumaye na Mwambe ni kitendo cha kuchukua fomu kuwania nafasi ya uwenyekiti wa Taifa wa Chadema katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Disemba 18 mwaka huu.

 

Aidha, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ni mmoja wa wanasiasa wanaoshadidia hoja hiyo na kubainisha kuwa anguko hilo lilikuwa limepangwa.

 

“Ni kama ilivyokuwa kwa Yesu alipopelekwa kwa Pilato kwa ajili ya kusulubiwa. Kilichofanyika, ni watu kumchagua Baraba badala ya Yesu. Kwamba Pilato aliwauliza baada ya kuona huyu mtu (Yesu) hana hatia. Badala ya mwizi na jambazi Baraba kufungwa, watu wakataka Yesu ndiyo aadhibiwe,” alisema.

NA GABRIEL MUSHI

Leave A Reply