The House of Favourite Newspapers

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Leo

1
lowassa na mboweViongozi waandamizi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana walikamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiwa katika kikao cha ndani katika Hoteli ya Giraffe mkoani Dar es Salam. 

Lowassa, ambaye alikaa kituoni hapo kwa takribani saa tatu anaweza kuwa kiongozi wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kuhojiwa na polisi.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako baadhi ya wajumbe na wabunge waliwafuata na kuwasubiri nje ya kituo hicho kujua hatima yao.

Viongozi hao walionekana wakiingia Polisi saa 10.30 jioni na kutoka saa 1.25 usiku, jambo ambalo liliwafanya wakae kituoni hapo kwa saa tatu.
Lissu alisema polisi walivamia kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 170, wakiwamo baadhi ya wabunge wa chama hicho na kuwakamata viongozi hao kwa maelezo kuwa wamekaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa.
Imeelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema walikuwa na mkutano uliotanguliwa na kikao cha viongozi wakuu na kufuatiwa na cha viongozi hao kikijumuisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri.
Wakiwa katika kikao hicho, ilielezwa kuwa watu wanne waliingia wakiwa wamevalia kiraia na kuwaeleza kuwa viongozi wao wanahitajika kituo kikuu cha polisi kutokana na kufanya mkutano kinyume cha sheria.
Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza ambaye  alikuwa kwenye mkutano huo alisema pamoja na mambo mengine ya chama, walikuwa wakijadili suala la operesheni Ukuta la Septemba Mosi kama liendelee au lisiendelee kutokana na hali ilivyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi hao walikamatwa kwa kukukaidi amri ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa na kuchochea wananchi kuandamana kinyume cha sheria Septemba Mosi.

Alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi hao wametakiwa kuripoti kituoni hapo leo.

Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishana wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijani lilipiga marufuku mikutano ya ndani likisema inatumika kuhamasisha watu kuvunja sheria za nchi na kupambana na askari.

Hatua hiyo ilikuja huku jeshi hilo likiwa limepiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kufuatia uamuzi wa Rais John Magufuli kuzuia shughuli  za kisiasa hadi 2020.

1 Comment
  1. IBRAHIM says

    HAKUNA ALIYE JUU YA SHERIA, BILA SALAM SOTE TUNAJUA BILA USALAMA HAKUNA MTU YOYOTE ATAEKUWA NA UWEZO WA KUFANYA CHOCHOTE AU JAMBO LA MAENDELEO, PIA KUMBUKENI WAHARIFU WENGI HUJIINGIZA KTK FUJO. MIKUTANO NA MAANDAMANO YASIYO NA MAADILI KWA NIA YA KUFANYA UHALIFU. TUSISAHAU TANZANIA NI YETU SOTE, HATUNA PENGINE PA KWELI, FUJO ZA UKUTA N. K NI KWA FAIDA YA NANI?? KAMA KUNA WATU WANATUMIWA NA MATAIFA YA NJE, TUNAWAOMBA MUACHE MARA MOJA, TUACHIENI TANZANIA YETU ILIYO SALAM A PA HAMKATAZWI KUHAMA NC I, KATAFUTENI URAIA SEHEMU ZINGINE, MAANA HAINGII HAKILINI MTU MTANZANIA MZALENDO WA KWELI AANDAE FUJO KWA VISINGIZIO VYA DEMOKRASIA. TUACHE UBABAISHAJI HAUWEZI KUTUFIKISHA POPOTE KATIKA DUNIA HII LEO, PA TUSISAHAU SOTE TUNAJUA JUKUMU LA KUJENGA MAADILI NA NIDHAMU BORA KWA VIJANA WA NCHI YETU, MIPANGO KAMA YA UKUTA N. K, JE INAWAFUNDISHA NINI VIJANA NA WANANCHI KWA JUMLA KTK KUWAJENGA KI MAADILI ? HIVI MNAJISAHAU KUNA SIKU NCHI ITATAWALIWA NA CHAMA KINGINE, KWA JINSI HII KILA MTU ANAWAJIBIKA KUJENGA TAIFA LENYE MAADILI MEMA, NA MAADILI MEMA NDIYO KILA KITU KTK USTAWI WA TAIFA LOLOTE DUNIA, SASA UNAPOTENGENEZA TAIFA LENYE MLENGO WA UOVU NI KWA FAIDA YA NANI? HEBU TUTULIE TUJITASIMINI UPYA, NIDHAMU HAMPO SAHIHI KABISA KWA HAYO MNAYOYAFANYA, MNASHABIKIWA NA WATU WANAOPENDA MAASI TU KWA FAIDA ZAO BINAFSI JAMBO LA HATARI SANA, HATA KWA NYINYI WENYEWE.

Leave A Reply