The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 83

ILIPOISHIA…
MABILIONEA wasio na huruma, Dk Viola na Injinia Vanessa, wamekamatwa kwa mara nyingine tena, baada ya kukikimbia kifo cha kunyongwa kwa muda mrefu. Sasa hawana ujanja tena na inaonekana adhabu ya kifo kwa mauaji waliyoyafanya ili wapate utajiri, haiepukiki.

Bado wakili wao Crapton ana uhakika wa kupata utajiri wa mabinti hao walioitikisa dunia mara baada ya kuyongwa kwao, lakini wenyewe wamemuita wakili wa serikali na kumtajia jina la mrithi wa mali zao zote. Mwanasheria huyo anashangaa. Je, ni nani aliyetajwa kurithi mali hizo? Je, watanyongwa na nini hatima ya wakili Crapton?
SONGA NAYO…

WAKILI Raymond Mapili alitayarisha wosia wa kisheria ambao ulimtaja mrithi wa fedha zote zaidi ya dola milioni tatu zilizokuwa kwenye akaunti zao mbalimbali, fedha hizo zilitokana na kuuza vitega uchumi vyao vyote nchini Tanzania wakijulikana kama Padri Silvanio na Sista Mariastela kabla hawajatoroka na kukamatwa.

Hapakuwa na maisha tena mbele yao, hata wangefanya kitu gani wasingeweza kutoroka na kukimbia kifo! Uamuzi walioufikia ulikuwa ni kukubali mauti ili waende zao ahera, hata hivyo walitaka utajiri wao ubaki mikononi mwa mtu sahihi, hawakupenda kabisa Wakili Denis Crapton afanye udanganyifu tena na kujipatia urithi ambao hakustahili.

Wakati anasaini nyaraka zote na kumtaka wakili Raymond ahakikishe jina la mtu waliyemtaja liendelee kubaki siri, naye akaahidi kufanya hivyo akidai kwa taaluma yake hakutakiwa kuvujisha siri za mteja wake bila ridhaa. Kilichofuata baada ya hapo kilikuwa ni maisha ya jela, Dk. Viola na Vanessa wakisubiri siku ambayo wangetaarifiwa juu ya kifo chao kwa sindano ya sumu.

Novemba 6, miezi mitano baadaye, siku iliwadia wakapewa taarifa kuwa wafanye maandalizi kwani Novemba 9, zoezi lingetekelezwa! Kwao haikuwa habari mpya wala ya kusikitisha, walishajiandaa kwa muda mrefu na kutubu dhambi zao zote wakijutia unyama walioufanya, sababu tu ya kutaka utajiri.

Kama ilivyotokea katika tukio la mwanzo la kudungwa sindano ambalo walifanya udanganyifu na kukitoroka kifo, ndivyo ilivyotokea siku ya Novemba 9, mamia ya watu walijaa nje ya Gereza la Gontwa, wengi wakiwa ni ndugu wa marehemu ambao Dk. Viola na Vanessa waliwaua, hamu yao ilikuwa ni kushuhudia watu hao wanakufa kabisa sababu ya unyama walioufanya.

“You won’t escape this time!”(Hamtatoroka safari hii!) lilisomeka bango la mama mmoja wa Kizungu nje ya gereza.

Muda ulikuwa ni saa moja kamili, baadhi ya ndugu waliotaka kushuhudia Dk. Viola na Vanessa wakidungwa sindano walikuwa ndani ya chumba maalum kilichotenganishwa na kioo kilichowawezesha kuona kwenye kitanda cha utekelezaji wa hukumu, watu wengi zaidi walikuwa nje wakifuatilia kwenye runinga kwani tukio hilo kama lile la mwanzo lilikuwa likionyeshwa dunia nzima.

Saa mbili kamili Dk. Viola na Vanessa waliingizwa kwenye chumba hicho na kulazwa juu ya vitanda, ulinzi siku hiyo ulionekana kuwa mkali kupita kiasi na jenereta iliwekwa ili kusudi umeme ukikatika liwake mara moja! kila kitu kilifanyika kuhakikisha hawatoroki tena, mtaalam wa kutafuta mshipa akiwa amejifunika uso kwa kitambaa cheusi ili asionekane, alionekana akichoma sindano kwenye mkono wa Dk. Viola na kubandika plasta, akafanya hivyo kwa Vanessa pia.

Alipomaliza zoezi hilo, alikwenda kwenye ukuta na kubonyeza swichi maalum, mabomba yakaanza kusukuma dawa yenye sumu kuingia kwenye mishipa ya Dk. Viola na Vanessa, nyuso zao zilikuwa zimejawa tabasamu, baadaye wakaanza kuzikunja na kuonyesha wako kwenye maumivu makali, kisha kuanza kutikisika kama vile wanapatwa na degedege, hatimaye wakatulia!

Je, wamekufa? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

Comments are closed.