The House of Favourite Newspapers

Madai ya Kuazima Vyombo… Mama Asuta Mtaa Mzima – Video

USWAHILINI kuna vituko! Mama mmoja anayejulikana kwa jina la Mama Shamira Mkazi wa Jeti Lumo Mtaa wa Masizi jijini Dar es Salaam, amewashushia kichambo cha kuwasuta watu mtaa mzima. 

 

Kisa cha kufanya hivyo kwa mujibu wa chanzo chetu ni kwamba, mama huyo alizushiwa maneno pale mtaani kwamba vyombo alivyomtunza binti yake Shamira Mashaka, siku ya ndoa yake aliviazima dukani.

 

Maneno hayo ya umbea ambayo hayajulikani yalianzia kwa nani hadi kuenea mtaa mzima, ndiyo yaliyomfika shingoni mama Shamira ambapo Novemba 23 mwaka huu mchana kweupe aliamua kutoka nyumbani kwake na kuanza kusuta watu bila kutaja majina yao. “Haya… mliokuwa mnasema vyombo hivi niliazima dukani liwashuke, vyombo hivyo hapo na hakuna hata kimoja kilichopungua,” alisema mama Shamira kwa sauti ya juu.

 

Hata hivyo, kabla ya kuanza kutoa maneno hayo ya msuto mtaani, alivitoa nje vyombo alivyomtunza mwanaye siku ya harusi yake ikiwemo kitanda, kabati la vyombo na nguo, king’amuzi, sofa, redio, mabegi ya nguo na viatu ili atakapokuwa akiwasuta watu wawe wanaviona.

 

Kama ujuavyo Uswahilini hakuna jambo dogo, ingawa Mama Shamira alikuwa hataji jina la mtu anayemsuta, watu kadhaa hasa wanawake walitoka majumbani kwao kusikiliza na wengine wakimshangilia msutaji.

 

Kwa kuwa mwandishi wetu alikuwepo mtaani hapo siku ya tukio, ‘msuto ulipopungua sauti’ na hali kurejea katika utulivu, alimuuliza Mama Shamira ni kipi kilichompa ujasiri wa kufanya jambo hilo mtaani kwake? “Sikia nikwambie, Jumamosi iliyopita ilikuwa Novemba 16, mwanangu alifunga ndoa.

“Mimi na familia yangu tulimfanyia sherehe siku tatu kuanzia siku ya Alhamisi, watu walikula na kunywa mpaka siku ya tukio lenyewe. “Huyu ni mwanangu wa kwanza, kwa hiyo sikutaka kumfanyia sherehe ndogo, nilikodi ukumbi wa maana na nilifanikiwa kumtunza mwanangu zawadi nyingi tu.

 

“Sasa sijakaa sawa nikaanza kusikia manenomaneno mtaani kwamba vile vitu nimeazima dukani ili nijionyeshe tu kwa watu. “Mimi nina uwezo wa kununua vitu kwa sababu nina hela na kazi yangu ni kukopesha watu hela nao wananilipa kwa riba, hiyo siyo kazi ndogo,” alisema Mama Shamira.

 

Aliongeza kuwa, aliamua kufanya hivyo ili kuwaziba midomo wale waliokuwa wanaeneza umbea mtaani kuwa, vyombo hivyo alikuwa ameazima.

“Leo ndiyo wanatakiwa kunifahamu vizuri, mimi si mtu wa kufanya bosheni na kuanzia sasa wanikome, atakayerudia kunitangazia ujinga kazi yangu itakuwa ni hii ya kichambo na msuto kwa kwenda mbele,” alisema Mama Shamira.

 

Kwa upande wake Shamira ambaye bado ananukia marashi ya harusi yake, aliwataka watu waache kufuatilia maisha ya familia yao na badala yake kila mtu afanye kazi.

“Maneno mengi sana yameongelewa kuhusu hizo zawadi ambazo mimi nimetunzwa kwenye harusi yangu, wanasema mama yangu pamoja na familia yangu wamenipa vitu bosheni. Ndugu zangu ambao wameshirikiana kwa pamoja kunipa zawadi hizo watajisikiaje wakisikia maneno haya?” alisema Shamira.

 

Naye jirani ambaye alijitambulisha kwa jina la Mama Shabani alisema, baadhi ya watu kwenye mtaa wao wamekuwa na maneno ya umbea na kuwataka waache tabia hiyo.

 

“Kitu ambacho hao watu wameumia ni zawadi ambazo Shamira ametunzwa, vimewauma kwa sababu haijawahi kutokea mtaani kwetu mtu kumtunza mwanaye vitu kama vile, ndiyo maana wanaeneza manenomaneno,” alisema jirani huyo ambaye ni mpambe wa Mama Shamira.

Comments are closed.