Man Fongo; Hainaga ushemeji, msosi wa magengeni silagi!
Amani Hamisi ‘Man Fongo’ na mwanaye.
Hainaga ushemeji, tunakula zama ya nani leo, zamu ya Man Fongo usijali kesho itakuwa yako, bodaboda kapita, muuza pipi kapita…
Wimbo huo wa mwanamuziki wa miondoko ya Singeli, Amani Hamisi ‘Man Fongo’ uitwao Haina Ushemeji ndiyo habari ya mjini sasa, safu hii haikupoteza muda, imemtafuta mkali huyo anayeishi maeneo ya Legho-Ubungo, Dar.
Nyumbani kwake anaishi na mkewe, katika mahojiano na safu hii mambo yalikuwa hivi:
Mpaka Home: Wapenzi wa Mpaka Home wangependa kufahamu ratiba yako ya siku nzima huwa unaipangaje?
Man Fongo: Mara nyingi naamka saa tatu, kwanza nafungua kinywa na maziwa ya moto kwa ajili ya kurekebisha sauti si unajua tena.
Man Fongo akiwa na mkewe
Mpaka Home: Kutokana na kazi zako za muziki kuna wakati unarudi usiku vipi mkeo haimsumbui?
Man Fongo: Hapana, anajua wazi kazi yangu ila siku kama yuko vizuri tunatoka wote.
Mpaka Home: Kuna tofauti gani kabla ya kuwa staa na sasa?
Man Fongo: Tofauti ipo kubwa, zamani niliweza kuibuka kitaa nikachukua muhogo na kutafuna huku natembea lakini sasa siwezi kwani mambo yamebadilika sana.
Mpaka Home: Nimetonywa kwamba ulikuwa maarufu sana kwenye vibanda vya mama ntilie, vipi bado unaenda au ilikuwa kabla hujavuta jiko?
Man Fongo: Siku hizi nimeacha hata nibanwe vipi chakula changu kikubwa ni kwa mke wangu tu.
Mpaka Home: Hapa ulipo umezungukwa na majirani, inakuwaje unapofanya mazoezi ya sauti?
Man Fongo: Najua kabisa nikipaza sauti sana nitawasumbua lakini najua jinsi ya kuitengeneza na kuwa vizuri.
Mpaka Home: Wanaume wengi wanajua kuwa kumsaidia mke kazi ni ushamba vipi kwa upande wako?
Man Fongo: Hata mimi najua kazi za nyumbani ni wajibu wake lakini mimi namsaidia.
Mpaka Home: Kuna gari aina ya Brevis nimeliona hapo nje ni la kwako?
Man Fongo: Ninatumia tu nimepewa na meneja wangu.
Mpaka Home: Ni wageni wa aina gani unapenda waje nyumbani kwako?
Man Fongo: Napenda sana kutembelewa na vijana wenzangu kwani huwa tunaimba na kufurahi.
Mpaka Home: Namba gani ya simu ni muhimu kwenye simu yako?
Man Fongo: Duuh! Unafikiri hapo nitajibu nini tena? Ni ya mke wangu tu maana yeye anajua nahitaji nini kwa muda gani.
Mpaka Home: Nakushukuru sana kaka.
Man Fongo: Karibu sana.