The House of Favourite Newspapers

Marekani: Kura Zaanza Kupigwa Jimbo la Florida

marekani-2Upigaji kura wa mapema umeanza katika jimbo muhimu linaloshindaniwa la Florida, ambapo Hillary Clinton na Donald Trump wanaendelea kushindana.

Bw Trump amekuwa akitafuta uungwaji mkono katika jimbo hilo na ameratibiwa kuwa na mikutano mitano ya kampeni. Bi Clinton pia anaangazia kampeni zake katika jimbo hilo.

Bi Clinton anaongoza kwa alama tatu kwa mujibu wa kura ya maoni ya CBS/YouGov.

marekani-1Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje ana 46% ya kura akilinganishwa na mpinzani wake Bw Trump aliye na 43%, kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni.

Kura ya maoni ya taifa ya CNN/ORC inaonyesha Bi Clinton yupo alama sita mbele ya mpinzani wake miongoni wa wapiga kura watarajiwa, akiwa na 51% dhidi ya Bw Trump 45%.

Kura za maoni katika ngome za Republican katika majimbo ya Arizona, Georgia na Utah zimeonesha ushindani ni mkali kuliko ilivyotarajiwa.

Lakini akihutubu katika mkutano wa kampeni St Augustine Jumatatu, Bw Trump, alisema: “Jamaa, tunashinda. Tunashinda. Tunashinda.”

Kwa mara nyingine amewalaumu wanahabari.

Amewashutumu pia wanaofanya utafiti wa kura za maoni.

Bw Trump amesema barua pepe za John Podesta zilizofichuliwa zinaonyesha mwenyekiti huyo wa kampeni wa Bi Clinton “anatumia udanganyifu kwenye kura za maoni kwa kuhakikisha wafuasi wengi wa Democratic wanashirikishwa”.

 Umuhimu wa kura zinazopigwa mapema

  • Zaidi ya Wamarekani 6m tayari wamepiga kura
  • Inakadiriwa kwamba 46m watakuwa washapiga kura kufikia siku ya uchaguzi, 40% ya wapiga kura wote
  • Katika jimbo muhimu la Carolina Kaskazini, wapiga kura wafuasi wa Democratic waliojiandikisha kupiga kura wameitisha karatasi za kura za mapema kushinda wenzao wa Republican.

Licha ya kashfa zinazomkabili kuhusu udhalilishaji wa wanawake, Bw Trump aliidhinishwa na gazeti la kwanza kuu Jumapili, gazeti la The Las Vegas Review-Journal jimbo la Nevada.

Nini kinafuata?

  • Wagombea wanatarajiwa kutumia siku 15 zilizosalia kujipigia debe. Wanatarajiwa kupiga kampeni sana majimbo yanayoshindaniwa kama vile Ohio, Carolina Kaskazini, Florida na Pennsylvania
  • Uchaguzi utafanyika Jumanne 8 Novemba kuamua Rais wa 45 wa Marekani.
  • Rais mpya ataapishwa 20 Januari 2017

Comments are closed.