The House of Favourite Newspapers

Mch Msigwa Asema Hajui Akwilina Aliuawa Lini

0

MBUNGE wa Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mchungaji, Peter Msigwa amesema kuwa taarifa za kifo cha Akwilina Akwiline kilichotokea Februari 16, 2018 katika maeneo ya Mkwajuni jijini Dar es Salaam alizipata kupitia taarifa ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwamba Polisi wanapaswa kujitathmini kutokana na kifo hicho.

 

Msigwa amesema hafahamu siku ya tukio la kifo hicho kwani yeye hajui majina ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam kutokana na yeye kuishi mikoani.

 

Hayo ameyaeleza leo wakati wa utetezi wake alipokuwa akihojiwa na wakili wa serikali, Jackline Nyantoli mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na utetezi ambapo wakili huyo alitaka kujua eneo la tukio hilo lilipotokea.

 

Msigwa amehojiwa mambo mbalimbali likiwemo swali iwapo wananchi wanaruhusiwa kutembea na mapanga siku ya uchaguzi.

 

Katika majibu yake, Msigwa amesema wananchi hawaruhusiwi kuwa na mapanga eneo la kituo cha uchaguzi, lakini siku hiyo ya uchaguzi hawazuiliwi kuwa na mapanga kwani wanaweza kuwa wanaelekea kuchanja kuni ama kukata mapori.

 

Katika Kesi hiyo Msigwa na wenzake nane wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

 

Mbali na Msigwa wengine wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

 

Wengine ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Leave A Reply