The House of Favourite Newspapers

MENEJA WA HARMONIZE APASUA JIPU

WAKATI madai yakiendelea kuwaka moto kwa memba wa Lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’ Rajabu Abdul Kahali ‘Harmonize’ kujitoa kwenye lebo hiyo, meneja anayemsimamia msanii huyo anayetambulika kwa jina moja la Mjerumani amepasua jipu na kuanika ukweli wa mambo.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juzi Jumatatu, meneja huyo (pichani) alisema ni kweli kwamba msanii wake katika siku za hivi karibuni amekuwa akifanya mambo yake binafsi lakini hayamaanishi kwamba amejitoa Wasafi.

Kwa muda mrefu sasa, madai yamekuwa yakiibuka na kusambaa kuwa bwa’mdogo huyo kutoka Umakondeni, Mtwara amejitoa lebo hiyo na hii ilichochewa zaidi na msanii huyo kutoonekana katika siku ya ufunguzi wa shoo ya Wasafi Festival iliyoanzia kwenye Viwanja vya Zimbihile, Muleba, mkoani Kagera.

Vyanzo mbalimbali vinaeleza licha ya yeye mwenyewe kutokea katika shoo nyingine ya Wasafi Festival ndani ya Rock City Mall, jijini Mwanza haijapunguza madai ya kuachana na lebo hiyo iliyomlea na kuwa msanii wa kwanza aliyepata mafanikio makubwa miongoni mwa wasanii waliopo WCB.

Kabla ya kumtafuta meneja wa msanii huyo chanzo chetu kililifungukia Risasi Mchanganyiko kwa kirefu kuhusu madai ya Harmonize kujitoa WCB ambapo kilisema: “Kwa upande wa shoo haina maana atakuwa akijitenga na Wasafi, atakuwa akijiunga nao lakini nyuma yake tayari ana watu wake na kila kitu anacho. Kwa mfano sasa hivi ana Konde Boy Gang ambayo ni kama ilivyo lebo ya Wasafi ikiwa na kila kitu ndani yake, ni timu kubwa inayoshiriki katika kuandaa kazi za Harmonize kila anapokwenda.

“Madai mengine ya kujitoa kwake ni kutokana na suala zima la masilahi ambapo akiangalia ameshakuwa msanii mkubwa anayetambulika ndani na nje ya nchi, hataki kuwa analipwa kwa mafungu sawa na wasanii wenzake katika lebo hiyo. “Ukiangalia katika muziki wake, amekuwa ni msanii ambaye anaweza kwenda Nigeria, Kenya, Uganda au nchi yeyote Afrika na kufanya shoo kivyake, akajaza kama anavyofanya Diamond.

“Hata nchini Marekani kuna utaratibu wao kwenye lebo kubwa. Kuna Lebo ya Cash Money ambayo mmiliki wake ni rapa Birdman (Bryan Christopher Brooks) ndani yake alikuwemo Lil Wayne, Drake, Nicki Minaj na Tyga lakini baada ya Lil Wayne kujitoa alianzisha yake ya Young Money na kuwachukua Drake, Tyga na Nicki ambao wote wanakimbiza hadi sasa.

“Kwa hiyo anachokifanya Harmonize kwa sasa ni suala la muda tu kutimia kwani kwa upande wa pesa ameonekana anazo, kujisimamia mwenyewe anaweza, studio anayo na tayari ameshaanza kuitangaza lebo yake ya Konde Gang.” Kutokana na madai hayo kuzidi kupamba moto, Risasi Mchanganyiko lilifanya mawasiliano na meneja wa Harmonize, mwanamama Mjerumani na haya ndiyo yalikuwa majibu yake.

Risasi Mchanganyiko: Habari yako meneja Mjerumani.

Meneja: Salama tu.

Risasi Mchanganyiko: Mimi naitwa (mwandishi anajitambulisha) Kumekuwa na madai ambayo bado yanaendelea kusambaa kama moto wa kifuu juu ya Harmonize kujitoa WCB, hii imekaaje meneja?

Meneja: Hakuna kitu kama hicho. Harmonize bado ni msanii kutoka Wasafi.

Risasi Mchanganyiko: Madai mengine yanasema kutokana na kuwa na pesa ameamua kujitoa katika lebo hiyo. Unazungumziaje hilo?

Meneja: Msanii kama msanii, kazi yake ni biashara na biashara ina muda. Kama msanii anakuwa katika sehemu yenye masilahi mazuri hawezi kuondoka lakini kama masilahi yanakuwa madogo hawezi kukaa.

Risasi Mchanganyiko: Lakini meneja Mjerumani, inadaiwa kuwa kwa sasa Harmonize ana Lebo ya Konde Gang na hii ni mwanzo tu wa kuwa na lebo yake kubwa ya muziki kama ilivyo Wasafi.

Meneja: Ngoja nikuambie kitu ambacho wengi hawaelewi. Ndani ya WCB kila msanii anaruhusiwa kutengeneza timu yake na watu wake. Mfano Lava Lava ana BITE Gang, ukienda Rayvanny na Mbosso nao hivyohivyo wana timu zao kubwa na watu wao.

Risasi Mchanganyiko: Sasa hapo kwenye mgawanyo wa pesa upoje maana Harmonize yupo chini ya WCB na analipwa na WCB kwa hiyo ndiyo akipata awalipe watu wake wa Konde Gang?

Meneja: Iko hivi, ndani ya WCB kila msanii ana meneja wake, Diamond peke yake ndiyo ana mameneja watatu (Babu Tale, Fella na Sallam) lakini Mbosso ana meneja wake mmoja, Harmonize nipo mimi na Rayvanny naye ana meneja wake mwingine; hakuna tatizo katika mgawanyo wa pesa.

STORI: MWANDISHI WETU, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.