The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni-49

0

ILIPOISHIA

Tulipofika Bagamoyo niligundua kuwa azma yangu ya kurudi Uingereza haraka inaweza kuzuiwa na makubaliano yangu na Faiza. Nilijua kuwa ingenigharimu lakini sikujali sana kwa sababu ya historia iliyotukutanisha mimi na Faiza ambayo tunzo yake adimu ingekuwa ni ndoa kati yetu.SASA ENDELEA…

Usiku wa siku ile Faiza aliniambia nimsindikize dukani.

“Unakwenda kununua nini?” Nikamuuliza.
“Kuna kitu nimetumwa na mama.”
Nilikuwa nimeketi kwenye kiti barazani mwa nyumba yao, nikainuka na kumsindikiza.
Wakati tukiwa njiani tukielekea kwenye duka la chakula lililokuwa mtaa wa pili, Faiza aliniambia.
“Nimeshazungumza na mama kuhusu lile suala letu.”
“Mama amesemaje?” Nikamuuliza.

“Amefurahia tu. Natumaini leo usiku atazungumza na baba.”
“Tumekwenda kinyume na utaratibu wetu. Ilitakiwa mimi nitume ujumbe kwa wazazi wako au niandike barua ya uchumba.”

“Ninajua, lakini si wakati wote mtu unalazimika kufuata utaratibu. Wakati mwingine taratibu zinaweza kukiukwa.”
“Sijui baba atanielewaje!”
“Atakuelewa vizuri tu.”

“Anaweza kujiuliza kama nilikuwa na nia hiyo kwa nini sikutuma mtu kwake, badala yake ninakutumia wewe.”
“Hayo ni mawazo yako tu, si mawazo ya baba. Nimemueleza mama kila kitu na ninaamini hatamficha baba. Mimi najua kuwa baba atafurahi.”

Faiza hakuwa na nia ya kusindikizwa dukani. Alikuwa akitaka kunieleza yale mnaneno tukiwa mahali faragha. Hivyo alinitoa kihekima pale nyumbani kwa kuniambia nimsindikize dukani.
Tulipofika kwenye hilo duka hakuwa na kitu chochote cha kununua.

“Nilizuga tu ili tuondoke pale nyumbani,” akaniambia.
“Kwa hiyo nitalazimika kuzungumza na baba yako hapo kesho?”
“Nadhani utazungumza naye lakini nitamsikiliza mama atakavyoniambia.”
“Nisingependa nikae sana kabla ya kurudi Uingereza, nimejipa muda wa wiki moja tu.”
“Usijali, wiki moja pia haitatimia, mambo yatakuwa sawa.”

Usiku wa siku ile wakati nipo kitandani, Faiza alinipigia simu akiwa chumbani kwake akaniambia jinsi alivyokuwa ananipenda na jinsi alivyokuwa anataka tuwe wamoja.
“Kwani mama yako hajakuambia kitu?” Nikamuuliza.
“Hajaniambia ni mpaka hapo kesho.”

Pakapita kimya kifupi kisha nikamsikia Faiza akiniita.
“Mume wangu…”
“Mhu…Unasemaje?”
“Nakupenda sana.”

“Mimi pia nakupenda sana.”
“Kama unanipenda kwa nini kila saa unawaza kwenda Uingereza?”
“Ndiyo kwenye kazi yangu.”

“Ukitaja sana Uingereza unaniudhi…”
“Usiudhike mpenzi wangu. Uingereza ndiko kunakonipatia maisha.”
“Tukishaoana mimi nitaishi wapi?”
“Utaishi hapa Tanzania.”
“Ninajua nitaishi Tanzania. Lakini wapi?”
“Popote utakapotaka wewe.”

“Dar es Salaam.”
“Hata Dar es Salaam.”
“Utanipangia nyumba.”

“Nitakupangia lakini ni mpaka niende Uingereza.”
Nilipotaja Uingereza Faiza akanyamaza kimya.
Nikamshtua.

“Hello!”
“Umerudia tena kutaja Uingereza. Si nimekwambia sitaki unitajie hilo jina,” Faiza akaniambia.
Nikacheka.
“Kwa nini hutaki nitaje hilo jina?”
“Sitaki uende huko kwa mke wako, nataka ubaki na mimi.”
“Nimeshakwambia kuwa huko ndiko ninakopatia maisha. Usichukie.”

Asubuhi kulipokucha baada ya kunywa chai baba yake Faiza aliniita.
Tuliweka kikao akaniambia amepata ujumbe kutoka kwa mke wake na amekubali nioane na mwanawe.
“Nimefurahi kusikia kuwa wewe na binti yangu mmefikia uamuzi wa kuoana,” akaniambia na kuongeza.
“Mimi kama mzazi wa Faiza nimekubali umuoe mwanangu bila hata kutoa senti tano yako na hivi ndivyo alivyotaka Faiza mwenyewe.”

Baada ya mazungumzo hayo na baba yake Faiza, siku ya pili yake maandalizi ya harusi yakaanza. Mzee huyo alitaka harusi hiyo ifanyike kimya kimya na isiwe na gharama kubwa.

“Nataka harusi hii ifanyike hapahapa Bagamoyo na kimya kimya, sitaki makuu,” alisema baba mkwe.
“Sawa baba, hata mimi nakubaliana na ushauri wako.”
“Mke wako ana habari hii?”
“Hana.”

“Je, hawezi kuleta tabu tukavuruga ndoa yenu?”
“Hawezi, namuelewa, ananiheshimu nami namheshimu.”
“Sawa lakini haya ni mapenzi.”

“Baba niamini mimi. Nikimpa sababu za mimi kufanya haya, hawezi kunipinga. Ananiheshimu sana na hili siyo jambo la kihuni.”
“Sawa, tuendelee na maandalizi.”

Kama ambavyo ilipangwa harusi hiyo ikafanyika Bagamoyo na ilihudhuriwa na ndugu zangu kutoka Pemba, nikakabidhiwa mke wangu.

Kwa vile nilikuwa na safari ya kwenda Uingereza nilimuacha Faiza nyumbani kwao nikaondoka.
Nilipofika London nilimueleza mke wangu kuwa nimeoa mke wa pili na nikampa sababu ya kufanya hivyo. Mke wangu hakuwa na kinyongo. Akanikubalia kwa moyo mkunjufu.
Baada ya miezi mitatu nikarudi Tanzania na kumpangishia nyumba Faiza jijini Dar ambako anaishi hadi hivi leo.

Mkataba wangu wa kufanya kazi Uingereza utakapokwisha nitarudi Dar es Salaam, nije niishi na wake zangu wawili.

MWISHO.
Umejifunza jambo? Wasiliana nami.

Leave A Reply