The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 38

0

AKIWA jijini Paris kuonyesha mitindo, Catarina anakutana na wakala aitwaye Mario Pizaro, huyu anamtaka wafuatane New York akamtafutie kampuni nyingine ya kufanya nayo kazi, kwa sababu Catarina alishakasirishwa na kitendo cha kuuzwa kwa tajiri Jackson Motown na kubakwa, akapoteza bikira yake aliyomtunzia mchumba wake Kevin, alikubaliana na ushauri huo hivyo kuvunja mkataba na kampuni ya Fonex Modelling.

Akiwa ndani ya ndege ya tajiri aliyedaiwa ndiye angemwajiri, anapewa taarifa kuwa tajiri angeingia chumbani kufanya naye maongezi, alipokuja tajiri huyo, Catarina hakuamini macho yake kumwona Jackson Motown tena akiwa uchi wa mnyama, kilichofuata hapo kilikuwa ni kubakwa mfululizo akiwa amegandamizwa kitandani na baunsa wa Jackson mpaka akapoteza fahamu, wakajaribu kumzindua lakini haikuwezekana.

Baada ya hapo haikujulikana mahali aliko, Mario Pizaro alipofuatwa siku chache baadaye na Afisa wa Balozi wa Tanzania, Washington DC alikanusha kusafiri na Catarina, akidai alibadilisha mawazo uwanja wa ndege, jambo ambalo lilikuwa ni uongo.

Kevin alipopewa taarifa hizo moyo ulimuuma sana, akafikia uamuzi wa kutamka mbele ya wazazi wa Catarina kwamba ilikuwa ni lazima asafiri kwenda kumtafuta mchumba wake huko Paris na New York, ndani ya moyo wake anasikia sauti inayomwambia “Catarina alishauawa” machozi yanambubujika.

Je, nini kitaendelea? Kwa nini Mario Pizaro anaficha ukweli? Catarina yuko hai au amekufa? Je, Kevin atasafiri kumfuata Catarina?

SONGA NAYO…

KULIKUWA na kila dalili kwamba Catarina hakuwa hai, jambo ambalo moyo wa Kevin haukutaka kukubaliana nalo, haikuwa rahisi kwa mtu aliyempenda kiasi hicho kuwa amekufa kabla ndoto yao ya kufunga ndoa haijatimia! Kila wazo kwamba Catarina alikuwa marehemu lilipomwijia kichwani mwake, maneno pekee ambayo kijana huyo aliyasema ni “NO! IT CAN NOT BE POSSIBLE!” Akimaanisha, (Hapana! Haiwezekani!)
Hakuwa tayari kabisa kukubaliana na maneno ambayo Mario Pizaro aliyatoa kwa Ofisa wa Balozi jijini New York kwamba Catarina hakusafiri nao, alibaki Paris baada ya kubadilisha mawazo uwanja wa ndege, maneno hayo ndiyo yalimfanya Kevin aamini kulikuwa na ukweli uliokuwa ukifichwa na huo ndiyo aliotaka kuufahamu kwa gharama yoyote ile.
“Wazazi nisikilizeni, sijui kama kuna mtu kati yenu anaweza kuelewa ninavyoumia moyoni!”
“Tunaelewa.” Baba na mama yake Catarina walijibu.
“Nimeamua kukatisha masomo yangu ili niondoke Tanzania kwenda Paris na baadaye New York, najua watu watanishangaa, kwa sababu hawaelewi Catarina ni kitu gani kwangu, nitakachohitaji kutoka kwenu pamoja na baba na mama yangu ni msaada wa kifedha, kubalini kunichangia fedha za safari na matumizi, hamtajuta kupoteza fedha zenu, nitarejea hapa nikiwa na Catarina, kama watakuwa wamemuua, waliofanya hivyo watakuwa mikononi mwa sheria bila kujali uwezo wao wa kifedha!”
“Kweli?”
“Kabisa, inaniuma mno na nilianza kugundua Catarina ana matatizo kila nilipokuwa nikiongea naye kwenye simu, hakuwa yuleyule niliyemfahamu, sauti yake ilijaa majonzi, nawasihi wazazi wangu kubalini nisafiri.”
“Wazazi wako watakubali?”
“Hawatakuwa na namna isipokuwa kukubali.”
“Basi, twende nyumbani kwenu tukaongee nao!”
Wakapanda gari moja na kuendesha hadi nyumbani, uzuri waliishi jirani, wakitenganishwa na ukuta wa senyenge tu katikati yao. Wazazi wa Catarina waliegesha gari nyumbani kwao kisha kuteremka na kutembea wakimfuata Kevin kwa nyuma, tayari ilishatimia saa kumi na mbili za jioni, wazazi wa Kevin walikuwepo ndani.
“Karibuni, mbona mnaonekana hivyo, kuna nini?” mama yake Kevin aliuliza.
“Kuna tatizo.”
“Tatizo gani tena?”
“Catarina amepotea, hajulikani aliko!”
“Si yupo Afrika Kusini?”
“Alisafiri kwenda Paris kutokea Afrika Kusini kwa ajili ya shughuli za mitindo, akiwa huko alikutana na wakala mwingine aliyemshawishi waende New York akamtafutie kazi kwenye kampuni tofauti akakubali, cha kushangaza huyo wakala amefuatwa na Ofisa wa Ubalozi na kudai Catarina alibadilisha mawazo akiwa uwanja wa ndege jambo ambalo linaonekana kabisa ni uongo, hakika mtoto wetu kama yuko hai basi atakuwa kwenye hatari!”
“Mungu wangu! Habari mbaya hizi.” Baba yake Kevin alisema.
“Baba!”
“Naam mwanangu!”
“Unajua kiasi gani nampenda Catarina.”
“Mimi ni mwanaume mwenzako najua.”
“Nimeamua kufanya maamuzi magumu.”
“Yapi tena mwanangu?”
“Ninaomba mniache tu nifanye nilivyoamua na mniunge mkono.”
“Sema kwanza maamuzi yako!”
“Mkinizuia nitajifanya kitu kibaya halafu mtajuta.”
“Mbona unatutisha! Sema uamuzi wako.”
“Naomba mniruhusu nikatishe masomo yangu nisafiri kwenda Paris na baadaye New York kumtafuta Catarina.”
Wazazi wake waliangaliana bila kusema chochote, mama yake akaanza kububujikwa na machozi, Kevin ndiye alikuwa mtoto wao pekee, kumwachia aende nchi ya ugenini kufanya kazi ya upelelezi ambayo hakuisomea ilionekana ni sawa na kumwingiza kwenye mdomo wa simba, jambo ambalo hawakuwa tayari kulifanya.
“Umetupa mtihani mgumu wewe mtoto,” mama yake aliongea.
“Niacheni tu mama, wala msiwe na wasiwasi Mungu atakuwa na mimi, maisha yangu hayana maana bila Catarina, nimemsubiri kwa muda mrefu mno, siwezi kunyang’anywa dakika za mwisho, hata ninyi mnafahamu jinsi nilivyojitoa kuokoa maisha yake, hata kama yuko hai na ameamua kubadilisha mawazo baada ya kukutana na matajiri wakubwa duniani kwenye masuala ya mitindo, bado nataka nikakutane naye ana kwa ana anitamkie kwamba hanitaki!”
Kwa msimamo aliouonyesha Kevin, kila mtu aliyekuwepo sebuleni aligundua kabisa hapakuwa na chembe ya utani kwenye maneno yake, wazazi wakajikuta hawana la kufanya zaidi ya kukubaliana naye, wote wanne wakanyanyuka na kumwomba apige magoti chini, wakamwekea mikono yao kichwani na kuanza kumwombea Baraka kwa Mungu ili asafiri na kurudi salama, akiwa na mafanikio.
“Amina!” wote wakamaliza kwa kuitikia neno hilo.
Kilichofuata baada ya hapo ni taratibu za safari, Kevin kwanza alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufanya taratibu zote za kuahirisha mwaka, kila mtu alimshangaa, hasa walimu wake, kwani alikuwa na uwezo mkubwa sana darasani kuliko mwanafunzi mwingine yeyote.
Baada ya hapo alitafuta mwaliko kutoka nchini Ufaransa na Marekani kwa rafiki zake walioishi humo, alipopata mialiko yote miwili akaanza kushughulikia taratibu za viza kwenye balozi hizo jijini Dar es Salaam, hakupata usumbufu wa aina yoyote mpaka hati zake zote mbili zikagongwa viza za kumruhusu kuingia nchini Ufaransa wiki mbili baadaye.
Wazazi pamoja na marafiki wakakutana na kufanya changizo la safari hiyo, zikapatikana jumla ya shilingi milioni sabini na tano ambazo zilipobadilishwa katika dola zilitimia kiasi cha Dola za Kimarekani elfu hamsini, zikawekwa kwenye akaunti ya benki ya CRBD na Kevin akapewa kadi iliyomruhusu kuchukua fedha popote duniani.
Siku mbili baadaye akakata tiketi ya Shirika la Ndege la Emirates na kuruka mpaka Dubai ambako aliendelea na safari yake mpaka alipotua Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle jijini Paris, ikiwa ni mara yake ya kwanza kusafiri nje ya mipaka ya Tanzania.
“Do you speak English?”(Unaweza kuongea Kiingereza?)
“je ne parle anglais” Alijibu dereva wa teksi kwa Lugha ya Kifaransa akimaanisha, lugha hiyo siifahamu.
“Hotel! Nearby, cheap!”(Hoteli ya bei rahisi iliyo karibu!) Kevin aliongea kwa maneno ya Kiingereza ambayo ni rahisi kuyaelewa lakini bado dereva wa teksi hakuelewa mpaka dereva mwingine mwenye kuzungumza Kiingereza kidogo alipowasogelea na kumchukua Kevin baada ya kumwelewa.
“Where are you from?”(Unatokea wapi?)
“Tanzania.”
“Ooh! Tanzania? Good country, huh?”(Ooh! Tanzania, nchi nzuri, sivyo?)
“Yes!” (ndiyo!)
“ I am from Algeria, I have lived in Paris for 25 years!”(Mimi natokea Algeria, nimeishi hapa Paris miaka ishirini na tano!)

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply