The House of Favourite Newspapers

Mkuki Moyoni Mwangu – 42

0

Kevin amefika Uwanja wa Ndege wa JF Kennedy akiongozana na Ofisa Ubalozi wa Tanzania pamoja na FBI ambao wanapewa kila aina ya msaada wa kuangalia Kamera ili kuona kama Catarina alitua uwanjani hapo akiongozana na watu wawili, Mario Pizaro na Jackson Motown.
Kamera hizo zinaonyesha kwamba Mario Pizaro na Motown waliingia wenyewe na Catarina hakuwepo, swali ni moja tu kichwani mwake Catarina yuko wapi alipotelea hewani kwani ndege hiyo binafsi haikutua mahali popote.
Upande wa pili wa hadithi hii Motown tajiri mtoto ili kuficha ukweli juu ya Catarina anaongea na meneja wa uwanja baada tu ya ndege kutua na mwili wa Catarina unaweka kwenye mfuko maalum na vijana waliokuwepo kwa kazi hiyo kisha kutolewa mpaka pembeni mwa uwanja na huko ungezikwa bila mtu yeyote kugundua.
Mario Pizaro analishuhudia jambo hilo na moyo wake unamuuma kupita maelezo anajilaumu kwa unyama aliomtendea binti huyo anatamka maneno “Mungu Nisamehe” alitamka maneno hayo moyoni mwake wakati yeye na Jackson Motown wakishuka ndani ya ndege tayari kwa kutoka nje ya uwanja bila mwili wa Catarina.
Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

Hali ya NewYork katikati ya mwezi huo wa Februari ilikuwa ya ubaridi kupita kiasi, joto likiwa nyuzi za sentigredi tano, wakati mwingine ikienda mpaka chini ya mbili! Hapakuwa na watu wengi nje, walijifungia ndani ya nyumba zao na kuwasha joto kwa sababu ya hali hiyo mbaya ya hewa. Juu ya ardhi kila mahali kulikuwa na theluji, ukungu ulitanda kila mahali kiasi cha kumfanya mtu asiwe na uwezo wa kuona mita kumi mbele yake.
Hali hii ilikuwa nzuri sana kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi zima la kumzika Catarina ardhini bila mtu yeyote kugundua, akabebwa na kuzungushwa nyuma ya ndege kisha vijana hao kuambaamba naye kandokando mpaka wakafika pembeni kabisa mwa uwanja ambako hapakuwa na mtu yeyote, huko ndiko liliandaliwa shimo lenye urefu wa mita tatu chini ya ardhi kwa ajili ya mazishi ya Catarina.
Bila huruma wakautupilia mwili shimoni, kisha kuchukua makoleo na kuanza kutupia udongo ndani yake, hakuna aliyeona huruma kwa mtu waliyekuwa wakimzika ili mradi tu waliahidiwa kiasi kikubwa cha fedha. Haya yakiendelea Jackson Motown alikuwa akimshusha Mario Pizaro nyumbani kwake Flatiron District, eneo la watu matajiri jijini NewYork.
“You seem not happy!”(Unaonekana huna furaha!)
“I am super worried!”(Naogopa mno!)
“What are you afraid of?”(Unaogopa nini?)
“Nothing done under the table stays there forever!”(Hakuna kitu kinachofanyika chini ya meza ambacho hubaki huko milele!) aliongea Mario Pizaro akimaanisha kwamba hofu yake kubwa ilikuwa siku moja jambo walilolitenda la kumuua Catarina na kumzika lingekuja kujulikana.
“Forget it, that is gone!”(Sahau, hilo limeshapita!)
“How will you keep it a secret while we have involved so many people?”(Utawezaje kulifanya siri wakati tumehusisha watu wengi kiasi hicho?)
“Leave it to me!”(Niachie mimi!) aliongea Jackson Motown kwa kujiamini.
Wakaagana, Mario Pizaro akaingia ndani ya jumba lake kubwa alimoishi peke yake isipokuwa mbwa wake mdogo mweupe mwenye manyoya mengi aliyeitwa Pogo, huyu ndiye alikuwa kila kitu kwake, siku hiyo wala hakucheza naye, alipitiliza moja kwa moja chumbani kwake na kujitupa kitandani, hakupata usingizi mpaka asubuhi akifikiria ukatili ambao yeye na Jackson Motown waliutenda kwa Catarina, hakika moyo wake ulijaa majuto.
***
“I don’t believe what you are telling me!”(Siamini unachoniambia!) Kevin alifoka mbele ya maofisa wa FBI.
“Why?”(Kwa nini?)
“I have shown you the camera report from Charles De Gaulle Paris Airport, which reveals that Catarina flew with Mario Pizaro in Jackson Motown’s private jet, then why are you telling me she stayed in Paris?”(Nimekwishaonyesha ripoti ya Kamera kutoka uwanja wa ndege wa Charles De Gaulle, ambayo inaonyesha Catarina aliondoka na Mario Pizaro kwenye ndege binafsi ya Jackson Motown, sasa kwa nini mnaniambia alibaki Paris?)
“That is final, FBI is no gonna spoil its resources on this investigation, if you are not satisfied you can see the Director, my advice to you is to go back to Paris where you are sister is!”(Huo ndiyo mwisho, FBI haitaharibu rasilimali zake kwenye upelelezi huu, kama hujaridhika unaweza kumwona Mkurugenzi, ushauri wangu kwako ni kurejea Paris ambako dada yako yupo!)
“Wewe ni mjinga mkubwa, huna maana yoyote, ninakueleza kwamba nitamtafuta Catarina mpaka nimpate, hata kama amekufa niujue ukweli wake na waliomuua wote wafikishwe mbele ya sheria, najua mnaweza kuwa mmehongwa na bilionea Jackson Motown, lakini mwisho wa siku mtaaibika!” Kevin aliongea kwa Kiswahili ili Maofisa wa FBI wasielewe alichokuwa akikisema, hasira ilikuwa imempanda kwani aliamini kabisa kuna jambo lilikuwa linafichwa.
“Tulia! Tulia!” Afisa wa Ubalozi bwana Faida Kalokozi alijaribu kumtuliza Kevin ambaye tayari alikuwa akibubujikwa na machozi.
Waliondoka uwanja wa ndege wakiwa wamevunjika moyo, kila kitu kilionekana kuwa mtihani mgumu maishani, Kevin hakujua mahali pa kuanzia ili kuupata ukweli aliokuwa akiutafuta. Jioni ya siku hiyo katika maongezi yao na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania alishauriwa afuatane naye hadi Washington DC lakini Kevin alikataa katakata.
“Moyo wangu uniambia, Catarina yuko hapa, siwezi kumwacha!”
“Lakini itakuwa vigumu sana kwako wewe kufanikiwa kulifanya jambo hilo!”
“Kaka, naomba usinivunje moyo, acha nijaribu nikishindwa nitakuja Washington DC kuomba msaada wa kurejea nyumbani.”
“Lakini pia hawa watu unaowafuatilia ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha wanaweza kufanya lolote kukudhuru!”
“Mungu atanilinda!”
Afisa wa Balozi alipoondoka Kevin alibaki peke yake, mawasiliano yake na nyumbani Tanzania yakawa ni kuwaambia tu kwamba alikuwa hajafanikiwa lakini pia alikuwa hajakata tamaa, akiamini kabisa kuwa ni lazima angeugundua ukweli kama si kumpata Catarina akiwa hai.
Mpaka mwezi mmoja baadaye alikuwa bado hajampata Catarina, wala kupata fununu zozote juu ya mahali alipokuwa, fedha zilishaanza kupungua, ili kukata matumizi aliamua kuondoka hotelini na kuanza kuishi mitaani na Wamarekani weusi na Wamexico wengi wasio na makazi, lakini kila siku kwake ilikuwa ni lazima afanye jambo fulani katika kumtafuta mpenzi wake, alishalia mpaka machozi yakakauka sasa ilikuwa ni kazi tu.
Mwanzoni mwa mwezi wa pili alianza kusoma habari katika magazeti na kuona kwenye televisheni wafanyakazi sita wa uwanja wa ndege wa JF Kennedy walivyokufa mfululizo kwenye nyumba zao, tena vifo vya kufanana vya kujidunda sindano za dawa za kulevya na kunywa kiasi kikubwa cha pombe kali, suala hilo lilichukua vichwa vya habari kwenye magazeti mengi kiasi cha watu kuanza kuhisi kulikuwa na jambo baya lililokuwa likiendelea.
Kufuatia tukio hili msako ukawa mkali sana mtaani, mara mbili Kevin alikamatwa usiku na kutupwa mahabusu, hata hivyo baadaye aliachiwa alipoonyesha hati yake ya kusafiria na viza iliyomruhusu kuwemo ndani ya mipaka ya Marekani kwa muda wa mwaka mmoja.
“I have to see Mario Pizaro again, probably he knows something right now!”(Inabidi nimwone Mario Pizaro tena, labda anajua kitu fulani hivi sasa!) aliwaza Kevin.
Siku iliyofuata aliondoka mtaani kwake Bronx Street na kwenda moja kwa moja ofisini kwa Mario Pizaro, kilichomshangaza mbele ya jengo hilo kubwa ni ukimya uliokuwepo na mlango ukiwa umefungwa, bango kubwa likiwa limebandikwa mbele ya mlango.
“We are apologize for the inconvenience caused, our director passed away three days ago, we are busy with funeral ceremony!”(Tunaomba msamaha wa usumbufu utakaotokea, Mkurugenzi wetu amefariki siku tatu zilizopita, tunashughulikia mazishi yake!) Kevin aliyasoma maandishi hayo na moyo wake akahisi umeruka mapigo kadhaa, jasho jingi likamtoka.
“Hapa kuna jambo linaendelea, si bure!” aliwaza Kevin.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Leave A Reply