The House of Favourite Newspapers

MPANGO WASAFI KUVUNJWA WAFICHUKA

KUNA mpango mchafu dhidi ya kundi au lebo inayofanya vizuri kwenye Muziki wa Bongo Fleva ya Wasafi Classic Baby (WCB), mpango huo umefichuka.

 

Kundi la Wasafi lililo chini ya mkurugenzi wake ambaye ni mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, linaundwa na vichwa vikali kama Diamond au Mondi mwenyewe, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Lava Lava, Queen Darleen na DJ Romy Jones. Kwa upande wa uongozi linasimamiwa na mameneja watatu ambao ni Babu Tale, Said Fella na Sallam SK.

KUNA MPANGO

Uchunguzi wa gazeti hili ndani ya Wasafi umebaini kwamba, nyuma ya mpango huo kuna kundi hasimu ambalo lengo lake ni kuona kundi hilo linaanguka kama ilivyokuwa kwa makundi mengi ya muziki huo ambayo yalikuwa tishio Bongo, lakini sasa yamekufa kifo cha asili.

VURUGU ZA HARMONIZE

Mpango huo wa hujuma unatajwa kusababisha vurugu zinazoendelea kati ya Harmonize na Wasafi ambapo jamaa huyo anadaiwa kutaka kujitoa na kwenda kuanzisha himaya chini ya lebo yake ya Konde Gang.

 

NDIYO WALE WA RICH MAVOKO

Kuna madai kwamba, watu hao wanaotaka kundi hilo livunjike ndiyo walewale waliomshawishi Rich Mavoko kuondoka Wasafi, jambo ambalo linadaiwa sasa linamtesa jamaa huyo. “Rich Mavoko alijazwa upepo bila kujua kwamba wale watu walikuwa na malengo gani? “Kama utakumbuka, Rich Mavoko alianza vurugu zake hivihivi kama anavyofanya Harmonize.

 

“Walikuwa wakimwambia yeye ni mkubwa, jina lake ni kubwa, lakini haonekani kwani Diamond alikuwa hampi nafasi ya kuonekana. “Matokeo yake na yeye akaamini maneno hayo bila kujua ulikuwa ni mpango wa kulivunja kundi hili linaloonekana kufanya vizuri zaidi ndani na nje ya Bongo.

 

“Nakumbuka walikuwa wanatumia mitandao ya kijamii kuzusha mambo mengi ambayo jamaa (Rich Mavoko) alionekana kuyaamini. “Kuna wengine walikuwa wanamwambia anabaniwa wakati wenzake wanatengeneza maisha ndipo akaona isiwe tabu, akajitoa kundini.

KAMPENI YASHIKA KASI

“Sasa mazingira yaleyale na aina ya stori zilezile zimerudi kupitia kwa Harmonize. Kampeni hii imeshika kasi mitandaoni.

 

“Wanamwambia Harmonize sasa amekuwa mkubwa kuliko bosi wake (Mondi) hivyo ananyonywa kwa sababu ameingia mkataba wa miaka kumi na ndiyo kwanza ana miaka mitatu au minne, sasa anaambiwa hadi hiyo miaka kumi iishe atakuwa amenyonywa vya kutosha.

“Wanamshauri Harmonize bora akavunja tu huo mkataba mapema kuliko kuendelea kutajirisha wengine.

HATA RAYVANNY NA MBOSSO

“Na kama watu hawajui, siyo Harmonize tu ambaye anajazwa upepo, lakini ndivyo ilivyo kwa Rayvanny na Mbosso. “Kama utakuwa unawafuatilia Rayvanny na Mbosso wamekuwa wakilalamika kuwa kuna watu wanaoeneza chokochoko dhidi yao kuwa na nao wanataka kuondoka Wasafi.

 

“Lava Lava wanamuona bado hana impacts (madhara) sana kwa sababu jina lake halijawa kubwa kihivyo. “Watu kama DJ Romy Jones na Queen Darleen hawawezi kutumika kupitisha chokochoko kwani hawa ni watoto wa nyumbani na hawana mikataba kama Harmonize, Rayvanny na Mbosso,” kilihitimisha chanzo hicho cha ndani.

 

TAMKO LA FELA

Kuhusu ishu hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Fella alitoa tamko ambalo liliibua gumzo kwa wadau wa burudani. Fella alisema kuna watu wanaowarubuni wasanii hao wa Wasafi kwa kuwaahidi mambo makubwa ili wajitoe kwenye lebo hiyo bila kujua lengo lao ni kuwasambaratisha.

 

“Kuna kipindi kuna watu walikuwa wanamrubuni Diamond aache kufanya kazi na mameneja wake. Walitaka kumpa dau la Dola za Kimarekani 100,000 (zaidi ya shilingi milioni 220 za Kitanzania),” alisema Fella na kuongeza kuwa watu hao sasa wanapita kwa Harmonize.

WADAU WANASEMAJE?

Baada ya kauli hiyo ya Fella ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kilungule wilayani Temeke, Dar, baadhi ya wadau waliozungumza na gazeti hili waliomba kundi hilo kulindwa kwani lina maadui wengi.

 

“Uchunguzi wenu (Gazeti la Risasi Mchanganyiko) na kauli ya Fella havipishani sana. Kinachotakiwa ni jitihada za kila namna za kulinda kundi hili lisivunjike kwani hakuna asiyejua kwamba ni kundi la mfano Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla,” alisema Mansour Rajab, Mkazi wa Mbezi-Beach, jirani na ofisi za Wasafi.

 

BAADHI LEBO ZILIZOWAHI KUFANYA VIZURI

Baadhi ya lebo zilizowahi kufanya vizuri kabla ya kufa na nyingine kusuasua ni pamoja na Bongo Records, MJ Records, Mawingu Studio, Sound Crafters, Empty Souls, Akili Records na G Records.

Comments are closed.