The House of Favourite Newspapers

MRUNDI ASIMAMISHA USAJILI AZAM FC

AZAM FC wenyewe wala hawatishwi na mbwembwe za usajili zinazofanywa na wapinzani wao Yanga kwani wametulia wakisubiri kwanza wamalizane na Mrundi Etienne Ndayiragije kisha ndiyo waanze balaa la kusajili.

 

Lakini habari ambazo Spoti Xtra ilizipata jana ni kwamba Kocha huyo ameshapewa nakala ya mkataba wa miaka miwili ndiyo anaipitia kisha asaini.

 

Azam kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na kocha Ndayiragije kwa ajili ya kumpa timu kwa msimu ujao baada ya kumtimua kocha wao, Hans van Der Pluijm.

 

Ndayiragije anatakiwa na Azam baada ya kufanya vizuri na klabu yake ya KMC kwa msimu huu huku akimaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

 

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’ amefunguka kwamba watafanya usajili wao wa msimu ujao baada ya kumalizana na suala la kocha huyo.

 

“Kwa sasa tunaendelea na mazungumzo na kocha Ndayiragije kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi ya kocha mkuu hapa. “Tukimaliza suala hilo ndiyo tutakuja na masuala mengine likiwemo hilo la usajili. Kila kitu tutakitangaza wazi baada ya kumalizana naye,” alisema Popat.

Comments are closed.